Watanzania Waongezeka Kutoka Watu 34.4 Milioni Hadi 44.9 huku Rais Kikwete akiwataka kupunguza kasi ya kuzaliana. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Monday, December 31, 2012

Watanzania Waongezeka Kutoka Watu 34.4 Milioni Hadi 44.9 huku Rais Kikwete akiwataka kupunguza kasi ya kuzaliana.

Sensa ya Watu na Makazi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Jakaya Mrisho Kikwete  ametangaza  matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ambapo  Watanzania waongezeka kutoka watu milioni 34.4 hadi kufikia watu milioni 44.9. 

 


Aidha matokeo hayo ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika nchini Agosti 26 hadi Septemba 8 mwaka 2012, yameonyesha kuwa  Tanzania bara kuna Watu  milioni 43.6  na Zanzibar watu Milioni 1.3.



Rais Jakaya Kikwete ndiye alitangaza matokeo hayo jana(Desemba 31) jijini Dar es Salaam na kuwataka Watanzania kupunguza kasi ya kuzaliana.



Ramani ya Tanzania.

Akizungumza katika viwanja vya Mnazi Mmoja wakati wa uzinduzi huo, Rais Kikwete ambaye aliambatana na viongozi mbalimbali wa kitaifa, alisema kuwa matokeo hayo ni ishara kwamba ifikapo mwaka 2016 kuna uwezekano wa idadi hiyo kufikia milioni 51 jambo ambalo linaweza kuwa ni mzigo kwa taifa, jamii na hata katika masuala ya uchumi.



Rais alifafanua kuwa jamii inapaswa kuyachukulia kwa uzito matokeo hayo hasa katika masuala ya kupanga uzazi pamoja na kuongeza bidii ya kufanya kazi.



Rais Kikwete alisema kuwa Watanzania wanapaswa kuongeza nguvu ya kufanya kazi zaidi kwa kuwa idadi imekuwa kubwa na inaongezeka kwa kasi kubwa.



Kupanga uzazi ni jambo la msingi sana na tuzingatie hayo ili kuweza kupiga hatua maana matokeo hayo yanaashiria idadi ya watu milioni 10 imeongezeka tangu sensa ya mwaka 2002 kufanyika,” alisema.



Alisema kuwa matokeo yatakayofuata yatatangazwa Februari ambapo yatatoa idadi ya wanaume na wanawake na matokeo mengine kutolewa Aprili 2013.



Rais Kikwete.
Rais aliongeza kuwa zoezi hilo linagharimu fedha nyingi lakini serikali inalazimika kufanya kutokana na kutakiwa kupanga sera na mikakati ya maendeleo ambapo kwa sensa ya mwaka 2012 imegharimu kiasi cha sh bilioni 140 na zilizotumika hadi sasa ni sh bilioni 124.



Hata hivyo ninapongeza kukamilika kwa zoezi hili la awali kwani kulikuwa na purukushani nyingi na maneno mengi ya kutaka kuvuruga…wapo walioendesha na kuhamasisha wengine wasusie, wapo waliotaka kuendesha maandamano wakati wakijua ni wakati wa sensa lakini pamoja na mitihani yote tumeweza kupata matokeo,” alisema.



Alisema sensa hiyo ni ya tano kufanyika tangu Muungano ambapo ya kwanza ilifanyika mwaka 1967 na idadi ya watu ilikuwa milioni 12,313,469, bara wakiwa milioni 11,958,654 na visiwani 354,400.



Alisema kuwa sensa ya kwanza ilifanyika mwaka 1910. Sensa nne za mwisho zilifanyika baada ya Uhuru katika miaka ya 1967, 1978, 1988 na 2002.



Kulingana na sensa ya mwisho iliyofanyika Agosti 2002, idadi ya watu nchini ilikuwa 34,443,603.




Waziri Mkuu

Mizengo Pinda.

Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya sensa, alisema kuwa mchakato huo ulikabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na watu wanne kupoteza maisha huku wengine wakijeruhiwa.



Alisema kuwa zaidi ya sh bilioni 90 zilitumika kuwalipa vijana walioajiriwa wakati wa sensa ambapo vijana 200,000 waliajiriwa katika kuhesabu na 400 wakati wa uchambuzi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad