Kocha mpya wa Simba Mfaransa Patrick Liewig ametua nchini na kuahidi kuwaletea mafanikio makubwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Monday, December 31, 2012

Kocha mpya wa Simba Mfaransa Patrick Liewig ametua nchini na kuahidi kuwaletea mafanikio makubwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.




Mfaransa Patrick Liewig

Na waandishi wa Habari

kwenye Uwanja wa Ndege

 wa Kimataifa wa Julius

Nyerere jijini Dar es Salaam.


Kocha mpya wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig ametua nchini leo na kupokewa na mamia ya mashabiki wa 'Wanamsimbazi' huku akiahidi kuwaletea mafanikio makubwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.



Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Liewig aliyekuja kutwaa nafasi iliyoachwa wazi na Mserbia Milovan Cirkovic, amesema 'Wanamsimbazi' watarajie mambo mazuri kutoka kwake, lakini kwa sharti la kumpa ushirikiano katika kila hatua wakati atakaposaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo na kuanza kibarua chake.




Katibu wa Simba,

 Evodius Mtawala

 (kushoto) akiongozana

na kocha mpya wa klabu hiyo,

 Patrcik Liewig baada ya

 kuwasili Uwanja wa Ndege

wa Julius Nyerere,

 Dar es Salaam. 


"Nimefurahishwa sana na mapokezi haya... najihisi kuwa nina deni kubwa. Naamini nitapata ushirikiano wa kutosha na baada ya kuzoeana na wachezaji, naamini Simba itafika mbali katika kila michuano," alisema kocha huyo.


Miongoni mwa watu waliofika uwanjani kumpokea kocha huyo ni Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, ambaye aliwaongoza mamia ya mashabiki wa Simba kumpokea kwa maandamano ya magari na pikipiki za bodaboda na bajaji.


Taarifa kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa kocha huyo atasaini mkataba wa kuifundisha klabu hiyo kwa miezi 18 na tukio hilo litakamilishwa kesho.








Wakati kocha huyo akitua ,Kikosi cha Simba SC kiko huko Visiwani Zanzibar  kushiriki  mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwenye Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar, kesho(Januari 2, 2013).


Kwa mujibu wa Msemaji wa Kamati ya Mashindano, Farouk Karim, Makamu  wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika  ufunguzi huo unaotarajiwa kufanyika usiku na kufuatiwa na mechi kati ya Simba ya Tanzania bara na Jamhuri ya Pemba.



Aidha  mchezo mwingine siku hiyo  utakuwa kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya Miembeni, ambao utafanyika kwenye uwanja wa Mao Tsetung kuanzia saa 10 alasiri na kwamba, maandalizi yote yamekamilika, ambapo timu zote shiriki zimeshaanza kuwasili visiwani humo.


Karim alisema kuwa, Januari 4 kutakuwa na mechi mbili, ambapo Jamhuri na Bandari zitacheza saa 10 alasiri na saa 2 usiku, Tusker ya Kenya itakuwa dimbani dhidi ya Simba huku Januari 5, Mtibwa Sugar itapepetana na Coastal Union saa 10 alasiri, wakati Miembeni na Azam shughuli itakuwa saa 2 usiku.



Alisema, mechi nyingine zitakuwa kati ya Tusker na Jamhuri saa 10 alasiri na mechi ya mwisho ya kundi hilo itakuwa kati ya Simba na Bandari wakati kundi B zitakuwa kati ya Miembeni na Coastal Union saa 10 alasiri na mechi ya mwisho katika mzunguko huo wa kwanza ni kati ya Azam na Mtibwa Sugar.



Karim aliongeza kuwa, hatua ya nusu fainali itaanza Januari 9 kwa mchezo mmoja huku wa pili ukiwa ni Januari 10, ambapo mechi zote zitapigwa saa 2 usiku.



Aliongeza kuwa, fainali za michuano hiyo zitarindima Januari 12 saa 2 usiku, ikiwa ni kilele cha michuano hiyo ambayo hufanyika kila mwaka.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad