Tafiti za kisayansi zimebaini kuwa nguo za ndani hasa zinazobana kwa wanaume na zile za aina ya nailoni (nylon) zinaathiri uwezo wa mbegu za kiume, hivyo kushindwa kutunga mimba.
Utafiti huo
uliofanyika katika nchi za Ufaransa na Uingereza na kuchapishwa katika Gazeti
la Daily Mail la Uingereza unabainisha kuwa, wanaume wanaovaa nguo za ndani
zinazobana na zile zilizotengezwa kwa malighafi ya nailoni, mbegu zao za kiume
(manii) huwa nyepesi na kupoteza uwezo wa kutunga mimba.
Vazi la
ndani la wanaume linalojulikana kama boksa na nguo nyingine za ndani za kubana
zenye asili ya nailoni, zinakuwa na athari kubwa zaidi hasa zinapovaliwa katika
sehemu zenye joto, kama Dar es Salaam.
Kutokana na
matokeo hayo, wanasayansi wameonya kuwa wanaume wanapaswa kuchukua tahadhari,
hasa kutokana na tafiti nyingi za karibuni kuthibitisha kuongezeka kwa matatizo
ya mbegu za kukosa uwezo wa kutunga ujauzito katika nyumba ya uzazi ya
mwanamke.
Akizungumzia
utafiti huo jana, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi katika
Hosipitali ya Taifa Muhimbili, Dk Cyril Massawe, alisema una ukweli kutokana na
mbegu za kiume kuwa nje ya mwili wa mwanamume tofauti na mwanamke ambaye kizazi
chake kipo ndani.
“Kwa kawaida
mwanamume anayeishi maeneo ya joto anapaswa kuwa makini sana, ili kuhifadhi
vizuri manii yake anatakiwa kutumia mavazi yenye kupitisha hewa,” alisema Dk
Massawe.
Ufaransa na
Uingereza.
Utafiti
uliofanywa Ufaransa umebaini kuwa, upungufu wa nguvu za kiume kwa wanaume wengi
ulianza kutokea tangu mwanzoni mwa 1990.
Awali,
ilikuwa ikiaminika kuwa kupungua kwa uwezo wa mbegu za kiume kulitokana na
sababu kama vile mtindo wa maisha, ulaji na matumizi ya dawa kupindukia na
matumizi ya vyakula vyenye kemikali nyingi, lakini safari hii utafiti umebaini
kuwa matumizi ya nguo za ndani yamekuwa yakiwaathiri wanaume wengi.
Mtafiti wa
Uingereza, Profesa Richard Sharpe anasema tatizo hilo linaweza kuepukwa ikiwa
mhusika atajitahidi kuvaa nguo zinazokubalika na mahala alipo. Hata hivyo,
anapendekeza uchunguzi zaidi ufanywe ili kulinda kizazi cha sasa na kijacho.
Mtafiti huyo
kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh anasema: “Uingereza suala hili halijawahi
kuonekana wala kutiliwa mkazo na kuwa kipaumbele katika afya, labda kwa sababu
ya wasiwasi kwamba sehemu za mwanamume zinatakiwa kubanwa. Hivi sasa hakuna
shaka kwamba suala hilo ambalo liliongelewa hapo awali lina ukweli ndani yake,
hivyo ni wakati kwa watu wote kuchukua hatua.”
“Kutokuchukua
hatua kutasababisha familia nyingi kukosa watoto na hivyo idadi ya watu
itapungua, lakini katika hali ya kawaida, ni vyema watu wakaelimishwa namna ya
uvaaji. Sehemu za joto mtu anatakiwa kuvaa pamba na si nailoni ili kulinda
mbegu zake.”
Profesa
Sharpe anasema bado wanasayansi wana kazi kubwa kwani mpaka sasa karibu kila
eneo ambalo wanasayanasi wamelichunguza limebainisha kuchangia tatizo hilo,
lakini mpaka sasa wanafikiri kuwa vyakula vyenye mafuta na vile vyenye kemikali
nyingi vina mchango mkubwa zaidi katika tatizo hilo.
Watafiti
ambao walitumia takwimu kutoka katika vituo vya afya 126, waligundua kuwa tangu
mwaka 1989 mpaka 2005, kulikuwa upungufu wa uwezo wa manii kwa mwanamume
kufanya kazi kwa asilimia 32.2, kiwango ambacho ni karibu asilimia mbili kwa
mwaka.
Watafiti
walisema: “Kwa ufahamu wetu, ni utafiti wa kwanza kufanyika na umehusisha mbegu
za kiume hai na uwezo wa manii katika nchi nzima kwa kipindi kirefu.”
“Huu ni
utafiti mkubwa na unatoa onyo kali kiafya kwa jamii. Lakini huwezi kumlazimisha
mtu kuhusu matumizi ya nguo za ndani,” wanasema.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment