Mbunge wa jimbo la Kasulu Vijijini Agripina Buyogera amelaani kitendo cha polisi kuwapiga na kuwaua wananchi wilayani Kasulu Mkoani Kigoma na kumtaka Waziri wa mambo ya ndani kuchukua hatua kukomesha vitendo hivyo. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Saturday, December 29, 2012

Mbunge wa jimbo la Kasulu Vijijini Agripina Buyogera amelaani kitendo cha polisi kuwapiga na kuwaua wananchi wilayani Kasulu Mkoani Kigoma na kumtaka Waziri wa mambo ya ndani kuchukua hatua kukomesha vitendo hivyo.


Kamanda wa Polisi,

Mkoa wa Kigoma

RPC. Fraiser Kashai
Mbunge wa jimbo la Kasulu Vijijini Agripina Buyogera amelaani kitendo cha polisi wilayani humo kuwapiga na kuwaua wananchi wilayani Kasulu mkoani Kigoma ambapo amemtaka Waziri wa mambo ya ndani kuchukua hatua kukomesha vitendo hivyo.


Buyogera amesema hayo wilayani Kasulu wakati wa mazishi ya Gasper Mussa Mkazi wa kijiji cha Heru Shingi tarafa ya Makere wilayani Kasulu Mkoani Kigoma , aliyefariki dunia wakati wa sikukuu ya Christmass kutokana na kipigo kutoka kwa askari polisi wilayani humo.



Mbunge huyo wa jimbo la Kasulu Vijijini amesema kuwa vitendo vya askari polisi wilayani humo kuchukua hatua ya kuwapiga na kuua raia vimekuwa vikitokea mara kwa mara na wameshatoa taarifa kwa jeshi la polisi lakini hakuna hatua zozote ambazo zimeshachukuliwa hadi sasa.



Ili kuweka mambo sawa mbunge huyo amelitaka jeshi la polisi kuwahamisha askari polisi ambao wameakaa wilayani humo kwa muda mrefu kwani kukaa kwao kwa muda mrefu kunawafanya wajione kama tayari wanamiliki uhai wa watu na kufanya chochote wanchoweza.



Naye Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Herushingo, Babona Kihenge alisema kuwa amesikitishwa na kitendo cha askari polisi kumpiga na kumuua mtuhumiwa jambo ambalo linaondoa imani ya wananchi kwa jeshi hilo.



Babona alisema kuwa vitendo vya polisi kuwapiga na kuwasababisha wananchi ulemavu wa kudumu na wakati mwingine kusababisha vifo vimekuwa vikitokea mara nyingi na kwa sasa wameiomba serikali kuchukua hatua kukomesha mauaji hayo yanayofanywa na polisi.



Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya Kasulu, Jonathan Bujiji amethibitisha kwamba marehemu Gasper alifikishwa hospitalini hapo akiwa amekufa jambo ambalo linathibitisha kwamba marehemu alifia kituo cha polisi kabla ya kufikishwa hospitalini hapo.



Aidha baadhi ya wananchi wamelaumu kitendo hicho cha polisi hao kumpiga na kumuua mtuhumiwa huyo ambaye chanzo cha ugomvi kinaelezwa kuwa ni kunywa pombe na kukataa kulipa katika kilabu cha pombe ambacho kinamilikiwa na askari aliyeongoza mauaji hayo aliyejulikana kwa jina la Peter.



Inaelezwa kuwa sababu ya marehemu kukataa kulipa pombe aliyokunywa kilisababishwa na askari huyo kukaidi kumlipa pesa zake kama ujira wa kazi ya kukarabati baadhi ya maeneo ya kilabu hicho cha pombe kabla sikukuu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad