Kikwete Mwenyekiti tena CCM apita kwa asilimia 99.92: Mangula,Dk Shein makamu wake. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Wednesday, November 14, 2012

Kikwete Mwenyekiti tena CCM apita kwa asilimia 99.92: Mangula,Dk Shein makamu wake.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana kilikamilisha safu yake ya uongozi kwa kuwapitisha kwa kishindo viongozi wa ngazi za juu wa Chama hicho katika uchaguzi ambao ulionekana kuwa na nidhamu kutokana na kutokuwa na uharibifu wa kura.




Katika uchaguzi wa safu za juu za Chama hicho, Mwenyekiti, Makamu wa Mwenyekiti Zanzibar na Bara wajumbe wa mkutano huo walitekeleza ombi la Yusuph Makamba la kumchagua kwa kishindo Jakaya Kikwete kuongoza CCM .


Anne Makinda
Akitangaza matokeo hayo Spika wa Bunge la Tanzania ambaye ndiye alikuwa msimamizi,Anne Makinda alisema kwamba Mwenyekiti  alipata ushindi wa kura 2,395 sawa na asilimia 99.92 huku kura mbili zikisema hapana.



Makamu Mwenyekiti Zanzibar Dk Ali Shein alipata kura 2,397 wakati makamu wa Bara Phillip Mangula naye alipata idadi hizo za kura huku kukiwa hakuna kura zilizoharibika wala kusema hapana kwa viongozi hao wawili.



Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akipongezwa na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa na Makamu wenyeviti wawili, Spika wa Bunge Anna Makinda, baada ya kumtangaza kushinda nafasi hiyo ya Uenyekiti, katika uchaguzi uliofanyika hivi punde katika ukumbi wa Kizota, Dodoma, ikiwa ni kuhitimisha shughuli za Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM. Wapili Kulia ni Makamu Mwenyekiti Mpya wa CCM (Zanzibar) Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Rais Dk. Moahamed Gharib Bilal.
  

Mwenyekiti wa CCM, Taifa, Jakaya Kikwete na Makamu wake wawili Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein (Zanzibar) na Philip Mangula (Bara) wakiwa meza kuu baada ya kutangazwa kushika nyandhifa zao.


Wajumbe wakiserebuka baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangazwa kuwa mshindi wa Uenyekiti wa CCM, Taifa.


Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete akiongoza kikao baada ya kushinda tena kiti hicho. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), Dk. Ali Mohamed Sheni na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phili Mangula.

Mohamed Seif Khatib
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuunda sekretarieti mpya baada ya uchaguzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti Bara na Zanzibar utakaofanyika leo.


Kwa upande wa Zanzibar, matokeo hayo yanaonyesha kuwa walioshinda ni pamoja na Mbunge wa Uzini, Mohamed Seif Khatib; Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Ali Mwinyi, Waziri wa Fedha Zanzibar, Omar Yussuf Mzee, Abdulhakim Chasama na  Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Shamsi Vuai Nahodha.


Wengine  ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Khadija Hassan Aboud, Bhaguanji Mansuria, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Khamis Mbeto.


Watu maarufu walioangukia pua katika uchaguzi huo ni Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Abdallah Juma Sadallah, mtoto wa Rais Mstaafu, Abdallah Mwinyi ambaye pia ni Mbunge wa Afrika Mashariki, Mbunge wa Viti Maalumu, Kidawa Salehe na Naibu Waziri wa Fedha wa zamani, Abdisalaam Issa Khatib.



Wajumbe wakipiga kura.
Majina ya wajumbe wa Nec walioshinda bara na kura walizopata katika mabano ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira aliyeongoza kundi hilo kwa kupata kura 2,135, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba (2,093), Mwekahazina wa CCM, Mwigulu Nchemba (1,967), na Katibu wa UVCCM, Martine Shigela (1,824).



Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi (1,805), Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe (1,455), Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mathayo David Mathayo (1,414), Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Jackson Msome (1,207), Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama (1,374) pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana  na Michezo, Fenela Mukangara (984).


Wakati walioshinda Bara na wapambe wao wakitambiana, majina makubwa yaliyoanguka katika uchaguzi huo ni pamoja ni Mbunge wa Afrika Mashariki, Shy-Rose Bhanji, Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama, Richard Hiza Tambwe na Mbunge wa zamani wa Muleba Kaskazini, Ruth Msafiri.



Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Benjamin Mkapa akiongoza Mkutano Mkuu kwa muda baada ya Kikwete kujiuzulu.  (Picha zote na Bashir Nkoromo)


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad