Mariam Khamis |
Mazishi
ya aliyekuwa mwimbaji mahiri wa taarabu hapa nchini Mariam Khamis ‘Paka Mapepe’,
yanatarajiwa kufanyika leo Jumatano, Magomeni Makuti wilayani Kinondoni, jijini
Dar es Salaam.
Mariam
(pichani) ambaye hadi anafariki alikuwa ni mwajiriwa wa TOT Taarab, alimefariki
alfajiri ya kuamkia leo kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kifo chake
kikitokana na matatizo ya uzazi, ingawa mtoto wake yu salama.
Kwa
mujibu wa Baba Mdogo wa marehemu anayetajwa kwa jina moja la Sembuli, alisema
kuwa, wamefikia uamuzi wa kumzika marehemu leo, baada ya kuombwa na Mkurugenzi
wa TOT Kapten Komba kufanya hivyo ili wapate kuhudhuria mazishi ya mfanyakazi
mwenzao.
Mariam
Khamis alitamba sana na wimbo wa Mapaka Mapepe alouimba akiwa na Melody, kiasi
cha kumpa jina hilo la utani, kabla ya kujiunga na Zanzibar Stars, kisha Five
Stars na hatimae TOT.
Wimbo
wake wa kwanza kurekodi na TOT ulikuwa ni ‘Sidhuriki na Lawama’ ambao unatamba
sana hadi sasa anapopchukuliwa na mauti yaliyoelezwa kutokana na Kifafa cha
Uzazi alichokumbana nacho baada ya kujifungua kwa operesheni kubwa.
Alijiunga
na TOT Taarab mwanzoni mwa mwaka jana, akitokea katika kundi la Five Stars
Modern Taarab aliloingia mwishoni mwa mwaka 2009.
Mariam
Khamis aliipa kisogo Five Stars na kuhamia TOT
Taarab muda mfupi kabla ya ajali ya kundi hilo iliyosababisha vifo vya
wasanii 13, akiwemo kijana mahiri Issa Kijoti mnamo mwezi Machi, mwaka jana
katika eneo la Mikumi Morogoro.
Akiwa
Five Stars, alitikisa kwa vibao viwili ikiwemo ‘Ndo Basi Tena’ pamoja na
‘Uzushi Haunitii Doa’ .
Historia
yake kimuziki ilianzia mwaka 2003, mara baada ya kuhitimu elimu ya sekondari,
ambako alipenda sana Taarab, kwa kuvutiwa na magwiji wa mipasho.
Baadhi
ya magwiji hao waliokuwa wakimvutia Mariam Khamis ni pamoja na Zuhura Shaaban,
‘Malkia wa Mipasho’ , Khadija Kopa na marehemu Nasma Khamis ‘Kidogo’.
Kati
ya watu waliogundua mapema kipaji chake cha uimbaji na kukifanyia kazi, ni baba
yake mdogo aitwaye Kessy Abdallah ambaye alimuunganisha kwenye kundi la Segere
No2, jijini Dar es Salaam, ili kujifua zaidi.
Akiwa
Segere, ambalo baadhi ya vinara wake alikuwa Mussa Msuba,
alirekodi
kibao kimoja kinachokwenda kwa jina la ‘Mpenzi’na kabla albamu yake haijatoka,
kundi lilisambaratika.
Mwaka
2007, Mussa Mipango, kati ya wapigaji mahiri wa gitaa zito, Besi hapa nchini,
aliyeko TOT Taarab hivi sasa, alimuunganishia katika kundi la Zanzibar Stars
Modern Taarab ‘Watoto wa Pwani’.
Hakukaa
sana Zanzibar Stars kwani mwaka huohuo, 2007 alihamia East African Melody
Taarab alikorekodi kibao ‘Paka Mapepe’ kilichotokea kutikisa kiasi cha
mashabiki kuamua jina hilo liwe la kwake moja kwa moja.
Mwaka
2008, alirejea Zanzibar Stars alikofikia kurekodi kibao ‘Huliwezi Bifu’, kabla
ya vingine kama vile; ‘Raha ya Mapenzi’, ‘Narindima Mie’ na ‘Shoga Habari Ndo
Hiyo’ .
Mara
baada ya kuingia TOT Taarab, alipewa
kurekodi kibao ‘Sidhuriki na Lawama’, ambacho hata mwenyewe alikuwa
akithibitisha kuwa, kilitokea kumsogeza na mashabiki wengi wa mipasho.
Kati
ya watu ambao mara kwa mara alipenda kuwataja kuwa ni miongoni mwa waliochangia
kumfikisha alipoishia, ni pamoja na baba na mama yake waliompa moyo tangu
alipoanza kujiingiza katika muziki.
Aidha,
alikuwa pia akipenda kuvishukuru vikundi vyote vya muziki wa taarab alivyopitia
ikiwamo Melody na mashabiki pamoja na wapenzi wote kwa ujumla.
Paka
Mapepe alizaliwa mwaka 1986, jijini Dar es Salaam na kupata elimu ya msingi
katika shule ya Amana, Ilala kuanzia mwaka 1994 hadi 2000 na sekondari ya
Jamhuri kati ya mwaka 2001 na 2003.
Aliolewa
na mpiga gita la besi mahiri wa gitaa la Besi, Haji Kijungu, aliyejaliwa kuzaa
naye mtoto mmoja aitwaye Taliq (6) pamoja na mwingine aliyezaliwa na
kusababisha kifo chake.
Wasanii
mbalimbali wa muziki nchini, hususani wa Taarabu, wameelezea kustushwa na kifo
cha Mariam, ambapo Habari Mseto ulishuhudia waimbaji na mashabiki mbalimbali
kwenye Hospitali ya Muhimbili, ulikohifadhiwa mwili wa marehemu.
No comments:
Post a Comment