Serikali ya Tanzania imeijia juu
Malawi kuhusiana na suala la mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa na kueleza kuwa
ina uwezo wa kulipeleka kwenye Mahakama
ya Haki ya Kimataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Bernard Membe amesema serikali inaweza kwenda ICJ
na kushinda kesi na ziwa Nyasa kuendelea kubaki na ramani yake ya awali ya enzi
na enzi.
Hata hivyo, hadi sasa serikali ya
Malawi imesusia vikao viwili ambavyo vilipangwa kufanyika kwa lengo la kutatua
na kupata jawabu ya mgogoro huo ambao umekuna vichwa vya viongozi wa nchi hizo
mbili.
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam leo Mh.
Bernard Membe amesema hatuwezi kukubali mtu mmoja asije na taratibu
zisifuatwe, na kufafanua kuwa tatizo hilo litakiwisha kipindi cha Rais Jakaya
Kikwete na kuwa litamalizika kabla ya kuondoka madarakani mwaka 2015.
Katika maelezo yake Mh. Membe
amesema hadi sasa Serikali ya Tanzania
haijatangaza rasmi kujiunga na ICJ, ingawa Malawi tayari ni Mwanachama, hivyo
endapo nchi ikitangaza kujiunga hata sasa inaweza kukimbilia ICJ na kuibuka
kidedea.
Ingawa Mh. Membe alishindwa
kueleza sababu ya Tanzania kutojiunga hadi sasa, amefafanua kuwa uwezo wa kushinda ni mkubwa
kutokana na baadhi ya migogoro ya aina hiyo kutatuliwa bila ubaguzi kwani
Mahakama hiyo itachora ramani ile ile ambayo ipo tangu zamani.
Alienda mbali zaidi na kueleza
kuwa, Serikali ya Tanzania haijafikiria kukimbilia ICJ kwa kuamini kuwa suala
hilo linaweza kutatulika kwa njia ya amani.
Kwa mujibu wa kauli yake, kama
mazungumzo hayo yatakwama Serikali
itaweza kulipeleka suala hilo kwenye Umoja wa Afrika kwa ajili ya kutatuliwa
kwa amani zaidi.
Hivyo, Serikali haipendi kuona
mgogoro huo ukiendeshwa kishabiki hasa kwa Serikali ya Malawi kutokana na
kukaidi baadhi ya makubaliano waliyofikiwa awali.
Ametumia fursa hiyo kutoa
ufafanuzi kwamba, kama mazungumzo baina yao yatakwama Serikali inaweza kulipeleka suala hilo kwa
wazee wenye busara Marais wastaafu wa Afrika.
Aidha Mh. Membe ametumia nafasi
hiyo kuwatoa wasiwasi raia wa Tanzania wanaoishi karibu na eneo hilo kuwa
hakuna vita yeyote itakayoweza kutokea hivyo waendelee na shughuli zao za kila
siku za uzalishaji kama kawaida.





No comments:
Post a Comment