Mabingwa wa soka Africa Mashariki na kati ,Timu ya Yanga imelazimisha matokeo ya sare ya kufungana bao 1-1 na
wapinzani wao wa jadi,ambao ni Mabingwa watetezi wa Ligi kuu,Timu ya Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara, uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuanzia saa 1:02
usiku.
Yanga ambao walimaliza mechi hiyo wakiwa pungufu baada ya Simon Msuva
kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 77 kwa kumrudishia rafu Juma Nyosso,
ndio waliohaha kusawazisha bao, baada ya kutanguliwa kwa bao la mapema la
kiungo Amri Kiemba dakika 4 tu ya mchezo baada ya kupokea pande zuri toka kwa
Mwinyi Kazimoto.
![]() |
SIMBA: Juma Kaseja, Nassor Chollo, Paul Ngalema, Juma Nyosso, Shomary
Kapombe, Jonas Mkude/Haruna Moshi, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu,
Edward Christopher/Daniel Akuffo na Mrisho Ngassa.
|
Simba walicheza vizuri kipindi chote cha kwanza wakigongeana pasi za
uhakika na kuwazidi kasi uwanjani wapinzani wao, wakati Yanga pamoja na
kuzinduka baada ya kufungwa bao, lakini makosa yalikuwa mengi.
Pasi zao zilikuwa nyingi hazifiki, walikuwa wanapokonyeka mipira
kirahisi, wanazidiwa nguvu na wapinzani wao katika kugombea mipira na hata
mashambulizi yao hayakuwa ya mpangilio, zaidi ya kuonekana kubahatisha zaidi
huku Mbuyu Twite alifumua shuti zuri dakika ya 38 kutoka wingi ya kulia, ambalo
lilitoka nje sentimita chache.
Kabla hata ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika, kocha
Mholanzi Ernie Brandts alimtoa Hamisi Kiiza na kumuingiza Frank Domayo ili
kuimarisha safu ya kiungo, ambayo ilionekana kuzidiwa na Simba inayofundishwa
na Mserbia, Milovan Cirkovick.
Kipindi cha pili, Yanga walianza na mabadiliko, kocha Ernie Brandts
akimtoa kiungo Nizar Khalfan na kumuingiza mshambuliaji Didier Kavumbangu,
ambaye alikwenda kuongeza nguvu ya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Katika dakika ya 63, beki Paul Ngalema aliunawa mpira katika harakati
za kuokoa na refa Mathew Akrama akaamuru penalti, ambayo ilikwamisha kimiani
kiufundi na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
![]() |
Bahanuzi anafunga
penalti.
|
Aidha kocha wa Simba, Milovan
amesema kwamba ulikuwa mchezo mzuri na Yanga walicheza vizuri, lakini timu yake
ilicheza vizuri na anajivunia.
Amesema Yanga imeimarika tofauti
na ilivyokuwa awali na kwamba hizo ni dalili Ligi Kuu msimu huu itakuwa ngumu.
Kwa upande wake, kocha wa Yanga, mwanzoni hawakucheza vizuri, lakini
baadaye walitulia na kucheza vizuri. “Hii ni mechi ya kweli ya upinzani,
unaweza kuona rafu na kadi nyingi,”alisema Brandts.
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 13, ndani ya mechi tano na
kuendelea kuongoza Ligi Kuu, wakati Yanga imefikisha pointi nane na kubaki
nafasi ya tano, kwani Coastal Union imetoa sare ya 2-2 na JKT Oljoro mjini
Arusha na kufikisha pointi tisa.
No comments:
Post a Comment