Kufuatia maamuzi ya kikao cha Kamati ya Katiba na Sheria ya TFF
kilichokaa Jumatatu iliyopita kujadili hatma ya wachezaji Kelvin Yondani na
Mbuyu Twite, Kamati ya Utendaji ya Simba SC ilikutana kwa siku mbili mfululizo
(Septemba 11 na 12) kujadili kuhusu maamuzi hayo.
Kabla ya kutangaza maamuzi ya Kamati ya Utendaji, nitumie nafasi hii
kuwashukuru wanachama waandamizi wa klabu; Mzee Samuel Sitta, Profesa Philemon
Sarungi, Mzee Yusuf Makamba na Profesa Juma Kapuya kwa mchango wao mkubwa wa
kimawazo kwa kamati ya utendaji ambao ulikuwa na ushawishi mkubwa kwenye
kufikia maamuzi ambayo tumeyafikia.
Kamati ya Utendaji ya Simba imefikia maamuzi yafuatayo.
1.
Simba haitajitoa kushiriki katika
michuano yote inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Ingawa uongozi ulipata shinikizo kubwa kutoka kwa wapenzi na wanachama wake la
kutaka timu ijitoe kwa kutoridhishwa na maamuzi ya kamati ya sheria, uongozi
umeona ni vema timu ikashiriki ligi. Uamuzi huu umezingatia ukweli kwamba
kujiondoa kwenye ligi usingekuwa uamuzi wa kimichezo. Hivyo Simba itashiriki
katika Ligi Kuu ya Vodacom msimu unaoanza wikiendi hii.
2.
Kwamba wanachama au wapenzi wote
waliokuwa na nia ya kutaka kupeleka suala hili mahakamani wasitishe dhamira yao
hiyo. Iwapo suala hili litapelekwa mahakamani, klabu inaweza kuathirika kwa
namna nyingi ikiwamo kuzuiwa kushiriki mashindano yoyote yanayotambuliwa na
TFF, CAF na FIFA.
3.
Kwamba uongozi wa Simba unaendelea na
jitihada nyingine za kutafuta haki kwenye maamuzi hayo ya kamati.
4.
Uongozi unalipeleka kwenye vyombo vya
dola suala la mchezaji Kelvin Yondani. Kwavile mchezaji mwenyewe amekataa kuwa
hakusaini Simba, namna pekee ya kumaliza utata kwenye hili ni kulipeleka kwenye
vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vina vifaa na watu wenye uwezo wa
kung’amua alama za vidole za watu.
5.
Uongozi wa Simba utakuwa ukitoa
taarifa za mara kwa mara kila zinapokuja kuhusiana na masuala haya na unawataka
wanachama na wapenzi wake kutulia wakati uongozi ukiendelea
kuyashughulikia .
Gazeti la NIPASHE.
KATIKA gazeti la NIPASHE toleo la leo Septemba 13, 2012, ukurasa wa
mwisho kuna habari yenye kichwa cha habari; “Rage Bingwa wa Kudanganya.”
Habari hiyo ndiyo ilikuwa habari kiongozi (lead story) ya gazeti hilo
kubwa na la kuheshimika hapa nchini.
Ndani ya habari hiyo, Mwenyekiti wa Simba, Mhe; Ismail Aden Rage,
ameelezwa kuwa ni mtu mwongo na anayependa kudanganya watu kila wakati.
Habari hizi zimemsikitisha Rage binafsi na kumfedheesha kila mwenye
kuitakia mema Simba.
Kinyume kabisa cha misingi ya taaluma ya uandishi, habari hiyo ya NIPASHE
imeandikwa pasipo kumhoji Rage mwenyewe au kiongozi yeyote wa Simba. Simba
ingeelewa kama mwandishi angeandika taarifa ile kama wazo binafsi au makala.
Lakini kuiandika kama habari, kwa kunukuu taarifa za upande mmoja na
zenye lengo la kutaka kumdhalilisha Mwenyekiti na klabu ya Simba, gazeti la
NIPASHE limekwenda mbali sana.
Kwa mfano, gazeti hilo limeeleza “uongo” mmojawapo wa Rage kuwa ni hatua
yake ya kutangaza kuitisha Mkutano Mkuu wa wanachama baada ya maamuzi ya Kamati
ya Mgongolwa.
Gazeti hilo limedai kwamba huo ni uongo kwa vile ili kuitisha mkutano,
Mwenyekiti anahitaji idhini ya zaidi ya theluthi mbili ya wanachama. ! Hata
hivyo, Katiba ya Simba inampa Mwenyekiti ridhaa ya kuitisha Mkutano Mkuu wa
dharura wakati wowote atakapoona inafaa.
Suala la theluthi mbili linakuja wakati wanachama wanapotaka kuitisha
mkutano huo wakati uongozi ukiwa hautaki. Lakini huu umeelezwa pia kama “uongo”
wa Rage.
Ikumbukwe pia kwamba Mheshimiwa Rage ni mbunge, mwenyekiti wa Simba na ni
mtu ambaye amewahi kushikilia nyadhifa mbalimbali katika sehemu nyeti.
Kusema kwamba mtu wa namna hii ni bingwa wa kudanganya ni matusi kwa watu
wanaomchagua kushika nafasi za heshima na wale waliowahi kumteua kushika nafasi
hizo kwa kuzingatia uchapakazi wake, ushawishi wake na mvuto alionao kwa
wananchi.
Simba haina nia, sababu wala haja ya kugombana na chombo chochote cha
habari achilia mbali NIPASHE. Hata hivyo, kwa sababu taarifa hii imegusa hadhi
ya mtu binafsi na taasisi anayoiongoza au watu wanaomwamini, klabu ingeomba
yafuatayo kutoka gazeti la NIPASHE.
Kwanza, gazeti hilo liombe radhi katika kipindi cha siku saba kutoka leo
kuhusiana na habari hizo ambazo zimemsononesha sana.
Pili, radhi hiyo iombwe kwa ukubwa uleule ambao habari ya leo iliandikwa.
Kinyume cha hayo, Rage na Simba haitasita kutafuta njia nyingine ya
kusafisha jina na hadhi yake binafsi na hadhi ya wale ambao wanamheshimu.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC.





No comments:
Post a Comment