Hadi
mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao na kipindi cha pili, Simba SC
inayofundishwa na Mserbia Milovan
Cirkovick ilipata bao la kuongoza dakika ya 53, mfungaji mshambuliaji kutoka
Ghana, Daniel Akuffo aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa
na Amir Maftah.
Mathare
walisawazisha bao hilo dakika ya 68, mfungaji Daniel Mwaura aliyeipasua ngome
ya Simba SC, iliyokuwa ikiogozwa na Paschal Ochieng na Juma Nyosso.
Beki
wa Mathare alimuangusha kwenye eneo la hatari, Uhuru Suleiman dakika ya 80 na
ushei na refa akaamuru ipigwe penalty iliyopachikwa kimiani kiufundi kwa
guu la kushoto la Kiggi Makassy.
Simba
ilicheza vizuri mechi hiyo leo hii Haruna Moshi ‘Boban’ akirudishwa katika
nafasi ya kiungo baada ya kupatikana kwa washambuliaji halisi na kucheza
kwa utulivu, akigawa vizuri mipira na hata kuwapokonya mipira viungo wa
timu pinzani.
Dakika
za mwishoni ilishuhudiwa Boban akipitia mpira kwa nguvu miguuni mwa
mshambuliaji wa Mathare baada ya
Maftah kupitwa, kuashiria kwamba kijana amebadilika si Yule wa kukaba kwa
macho.
Feliz
Sunzu na Akuffo walikuwa wanapishana vizuri pale mbele na waliitia misukosuko
ngome ya Mathare- zaidi ni kwamba wawili hawa wanahitaji muda zaidi wa
kucheza pamoja ili kutengeneza safu kali ya ushambuliaji ya Simba SC.
Juma
Kaseja na Mrisho Ngassa hawakushiriki kabisa mechi ya leo kwa sababu walikuwa
wagonjwa na Keita alimpisha Nyosso baada ya kuumia.
Simba
itamenyana na Azam katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa
pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Septemba 8, mwaka huu, Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Kihistoria
hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili
kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na
Yanga.
Mtibwa
ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na
kutwaa Ngao wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado
inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari
Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika
mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga
iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana,
Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga
mabao 2-0.
Katika
mchezo huo, kikosi cha Simba kilikuwa; Wilbert Mweta/Hassan Waziri, Nassor
Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah/Paul
Ngalema, Paschal Ochieng, Komabil Keita/Juma Nyosso, Salum Kinje/Ramadhan
Chombo ‘Redondo’, Mwinyi
Kazimoto/Haruna Shamte, Haruna Moshi, Felix Sunzu, Abdallah Juma/Amri Kiemba na
Daniel Akuffo/Uhuru Suleiman.





No comments:
Post a Comment