BINGWA MICHUANO YA BANCABC SUPER 8 KUPATA MIL 40/-
Bingwa wa
michuano ya BancABC Super 8 inayoanza keshokutwa (Agosti 5 mwaka huu) katika
miji ya Dar es Salaam, Zanzibar, Mwanza na Arusha atapata sh. milioni 40 wakati
makamu bingwa sh. milioni 20. Pia timu mbili zitakazoishia hatua ya nusu
fainali kila moja itapata sh. milioni 15 wakati zilizobaki kila moja itapata
sh. milioni 5.
Timu
zimepangwa katika makundi mawili ya A na B. Kundi A lina timu za Simba
(mabingwa wa Tanzania Bara), Jamhuri, Zimamoto na Mtende zote za Zanzibar.
Kundi ni Super Falcon (mabingwa wa Zanzibar), Azam, Mtibwa Sugar na Polisi
Morogoro zote za Tanzania Bara.
Mechi za
ufunguzi keshokutwa (Agosti 5 mwaka huu) ni Simba vs Jamhuri (Dar es Salaam),
Zimamoto vs Mtende (Mwanza), Mtibwa Sugar vs Polisi Morogoro (Arusha) na Super
Falcon vs Azam (Zanzibar). Awali mashindano yalikuwa yaanze Agosti 4 mwaka huu
lakini yamesogezwa mbele kwa siku moja.
Hatua ya
makundi itamalizika Agosti 12 mwaka huu. Mechi za nusu fainali na fainali zote
zitachezwa Dar es Salaam. Nimeambatanisha ratiba.
Mdhamini
bancABC atagharamia usafiri wa ndege kwa timu zote kutoka kituo kimoja hadi
kingine, malazi na jezi. Yanga imejitokea kwenye mashindano hayo na nafasi yake
imechukuliwa na Mtibwa Sugar ambayo ilishika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu ya
Vodacom.
LIGI DARAJA LA KWANZA SASA TIMU 24.
Ligi Daraja
la Kwanza (FDL) kuanzia msimu huu wa 2012/2013 itakuwa na timu 24 kutokana na
mabadiliko ya mfumo wa mashindano yaliyofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF).
Kamati ya
Utendaji ya TFF ilikutana Julai 29 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine
ilifanya mabadiliko ya mfumo wa mashindano ikiwemo FDL kuchezwa kwa mtindo wa
nyumbani na ugenini badala ya ule wa awali wa vituo.
Kutokana na
mabadiliko hayo, timu za FDL zitagawanywa katika makundi mawili ya timu 12 kila
moja kutokana na ukaribu wa kanda na kucheza kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Timu ya
kwanza kutoka kila kundi itapanda kucheza Ligi Kuu msimu unaofuata wakati ya
tatu itakayoungana na hizo mbili itapatikana kwa mechi za nyumbani na ugenini
kwa timu zilizoshika nafasi ya pili katika kila kundi.
Ili
kufikisha idadi ya timu 24 kwenye FDL, Kamati ya Utendaji ya TFF kwa kuzingatia
mapendekezo ya Kamati ya Mashindano imeamua timu tatu za juu kwenye Ligi ya
Taifa kutoka vituo vyote vitatu vya ligi hiyo zimepanda daraja.
Sasa timu 24
za FDL ni Ashanti United (Dar es Salaam), Burkina Moro (Morogoro), Green
Warriors (Dar es Salaam), Kanembwa JKT (Kigoma), Kurugenzi Mafinga (Iringa),
Majimaji (Ruvuma), Mbeya City (Mbeya), Mkamba Rangers (Morogoro), Mlale JKT
(Ruvuma) na Morani (Manyara).
Nyingine ni
Moro United (Dar es Salaam), Mwadui (Shinyanga), Ndanda (Mtwara), Pamba
(Mwanza), Polisi (Arusha), Polisi (Dodoma), Polisi (Iringa), Polisi (Mara),
Polisi (Tabora), Rhino Rangers (Tabora), Small Kids (Rukwa), Tessema (Dar es
Salaam), Transit Camp (Dar es Salaam), Villa Squad (Dar es Salaam).
Timu nne
zitashuka daraja kurudi Ligi ya Mkoa. Timu hizo ni mbili zilizoshika nafasi za
mwisho kwa kila kundi. Timu nne zitakazopanda kucheza FDL zitapatikana kwa
mchujo utakaohusisha mabingwa wa mikoa.
Kwa mfumo
huo mpya wa mashindano, ligi za mikoa zitakazosimamiwa na kuendeshwa na vyama
vya mpira wa miguu vya mikoa zinatakiwa kuwa na timu zisizopungua 16 na
zisizozidi 20. Ligi za mikoa pia zitachezwa mwaka mzima kwa mikondo miwili
(nyumbani na ugenini).
Ligi ya mkoa
itashusha timu mbili na kupandisha nyingine mbili kutoka ligi ya wilaya. Ligi
za wilaya zitakazosimamiwa na kuendeshwa na vyama vya mpira wa miguu vya wilaya
zinatakiwa kuwa na timu zisizopungua 10 na zisizozidi 20.
Kwa wilaya
zenye timu zaidi ya 20, chama husika cha mpira wa miguu kitapanga utaratibu wa
kuzichuja kwa mashindano ili kupata zile bora 20 zitakazocheza ligi rasmi ya
wilaya.
Mabingwa wa
wilaya katika mkoa husika watacheza mechi za kuchujana (play offs) ili kupata
timu mbili zitakazopanda daraja kucheza ligi ya mkoa husika.
Kutokana na
mabadiliko hayo ya mfumo wa mashindano, sasa madaraja rasmi ya ligi ni Ligi
Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi ya Mkoa (Ligi Daraja la Tatu) na Ligi ya
Wilaya (Ligi Daraja la Nne).
TFF
inasisitiza kuwa kwa mujibu wa kalenda yake ya matukio, kipindi cha usajili wa
wachezaji kwa madaraja yote ni kimoja, na ligi zitachezwa kwa wakati mmoja.
Usajili wa
hatua ya kwanza ni kuanzia Juni 15 hadi Agosti 10 mwaka huu wakati kipindi cha
pili cha usajili ni Agosti 21 hadi Septemba 4 mwaka huu. Usajili wa dirisha
dogo ni Novemba 15 hadi Desemba 15 mwaka huu.
Ligi kwa
madaraja yote zitaanza Septemba. Ligi Kuu itaanza Septemba Mosi mwaka huu, Ligi
Daraja la Kwanza ni Septemba 15 mwaka huu, Ligi ya Mkoa na ile ya Wilaya
zenyewe zitaanza Septemba 8 mwaka huu.
Mechi za
kufungua msimu kwa madaraja yote (Ngao ya Jamii) ambazo kwa sasa zinakutanisha
bingwa na makamu bingwa zitachezwa Agosti 25 mwaka huu wakati michuano ya Kombe
la FA itaanzia wilayani Septemba 24 mwaka huu.
KOZI YA UONGOZI YA FIFA KUANZA AGOSTI 6.
Kozi ya
Uongozi na Utawala ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)
itafanyika Msimbazi Center jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 6-11 mwaka huu
ikiwa na washiriki 30.
Washiriki wa
kozi hiyo itakayonedeshwa na wakufunzi kutoka FIFA ni viongozi kutoka TFF,
Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), vyama vya mpira wa miguu vya mikoa,
klabu za Ligi Kuu na viongozi wa mpira wa miguu wa wanawake.
Walioteuliwa
kushiriki ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani, Rais wa ZFA
Amani Makungu, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF; Ahmed Mgoyi, Blassy
Kiondo, Stanley Lugenge, Khalid Abdallah, Hussein Mwamba na Eliud Mvella.
Wengine ni
Katibu Mkuu wa ZFA, Kassim Salum, Katibu Msaidizi wa ZFA, Masoud Attai,
wenyeviti wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Kagera (Jamal Malinzi),
Dodoma (Nassoro Kipenzi) na Pascal Kihanga (Morogoro).
Makatibu wa
vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Mara (Mugisha Galibona), Mtwara (Vincent
Majiri), Morogoro (Hamisi Semka), Kagera (Salum Chama), Tanga (Beatrice Mgaya)
na Dodoma (Stuart Masima). Pia yumo Mwenyekiti wa Coastal Union, Ahmed Hilal na
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga.
Washiriki
wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, Mkurugenzi wa Ufundi, Sunday
Kayuni, Ofisa Habari, Boniface Wambura, Mkurugenzi wa Masoko na Matukio, Jimmy
Kabwe, Mkurugenzi wa Mashindano, Saad Kawemba, Ofisa Sheria wa TFF, Neema
Lucumay, Ofisa wa Mpira wa Miguu wa Wanawake, Grace Buretha, Amina Karuma
(Mpira wa miguu wa wanawake) na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Shadrack
Nsajigwa.
STARS KUIKABILI BOTSWANA AGOSTI 15.
Timu ya
Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Agosti 15 mwaka huu itapambana na Botswana
(Zebras) katika mchezo maalumu wa Kalenda ya FIFA utakaofanyika jijini
Gaborone.
Tayari Kocha
Kim Poulsen alishatangaza kikosi cha wachezaji 21 kitakachoingia kambini Agosti
8 mwaka huu tayari kwa mechi hiyo ya kirafiki ya kujipima nguvu.
Boniface
Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment