Wanakiji wa
kijiji cha Mkulula kilichopo Kata ya Malenga Makali mkoani Iringa wakimsikiliza
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo
pichani) kuhusu jitihada za Serikali za kuwapatia wananchi mawasiliano wakati
wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu kwenye kijiji hicho ya ukagua
upatikanaji wa mawasiliano.
Naibu Waziri
wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto)
akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Amina Masenza (wa kwanza kulia) ramani
ya maeneo yanayopata mawasiliano mkoani humo wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge
ya Miundombinu ya kukagua upatikanaji wa mawasiliano kwenye mkoa huo.
Anayeshuhudia katikati ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Hawa Mchafu.
Naibu Waziri
wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto)
akiteremka kwenye kilima kilichojengwa mnara wa mawasiliano wakati wa ziara ya
Kamati ya Bunge ya Miundombinu ya kukagua upatikanaji wa mawasiliano kwenye
kijiji cha Mkulula kilichopo Kata ya Malenga Makali mkoani Iringa. Wa pili
kulia ni mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Bhagwanji Meisuria.
Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeyataka makampuni ya simu nchini kutoa huduma
za data kwa wananchi waishio vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara
ambapo makampuni hayo yamejenga minara kwa ajlii ya kuwapatia wananchi
mawasiliano.
Hayo
yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Ndiye wakati wa ziara ya
Kamati ya Bunge ya Miundombinu ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano
kwa wananchi waishio viijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara wakati
akizungumza na wanakijiji wa kijiji cha Mkulula kilichopo Kata ya Malenga
Makali mkoani Iringa.
Nditiye amefafanua kuwa kampuni za simu
zinatoa huduma ya sauti tu yaani 2G kwenye minara ya mawasiliano waliyojenga
badala ya kutoa huduma ya data kwenye maeneo hayo ili wananchi wapate huduma ya
intaneti. Amesema kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)
inatoa ruzuku kwa makampuni hizo ili wajenge minara.
“Tunataka wananchi wapate mawasiliano kwa kuwa wanalipia na ni
haki yao ya msingi kuwasiliana na hii
ndio Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya kuhudumia wananchi wa hali zote,” amesema Nditiye.
Ameongeza
kuwa hadi sasa UCSAF imetoa ruzuku kwa makampuni ya simu ambapo jumla ya kata
530 zimepatiwa huduma ya mawasiliano kwenye maeneo mbali mbali nchini na ujenzi
wa mnara mmoja una gharimu kati ya kiasi cha shilingi milioni mia mbili hadi
milioni mia tatu.
Akiwa katika
ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Mchafu amesema kuwa makampuni ya simu yanapowekeza
yasiwekeze kwa mahitaji ya kipindi kifupi bali miundombinu ya mawasiliano
wanayojenga izingatie mahitaji ya muda mrefu kwa kuwa wananchi wanaongezeka
kwenye maeneo hayo na wanakuwa wengi mathalani kwenye eneo la kata hiyo
wananchi wananchi wanafanya shughuli za uchimbaji wa madini, kilimo na ufugaji
wa samaki.
Ameongeza
kuwa watoa huduma waweke mawasiliano ya data yaani 4G ili wananchi wapate
huduma. “Haiwezekani fedha imetolewa na Serikali ya kujenga mnara kiasi cha
shilingi milioni 260 halafu wananchi hawawasiliani,” Mhe. Mchafu amesema.
Amefafanua kwa wanakijiji hao kwa kusema kuwa, “mnara
mnauona umejengwa na TIGO kwa kupatiwa ruzuku na Serikali kupitia UCSAF kiasi
cha shilingi milioni 260, nawaomba muiamini Serikali kuwa itatua kero zenu”
Mhe. Mchafu amesema.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment