Halmashauri
ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera inakabiliwa na upungufu
wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi na
kusababisha mipango ya kuboresha taaluma kushindwa kutekelezwa kwa
malengo kusudiwa.
Afisa elimu
taaluma idara ya msingi wilayani Biharamulo Amosi Nyamtera amebainisha hayo
jana Juni 12 wakati wa kuadhimisha wiki ya elimu na kwamba
changamoto ni madawati ambapo yaliyopo ni 16,934 katika vyumba 617 kati
ya 1.586 vyenye wavulana 43,927 na wasichana 43136 katika idara hiyo.
Nyamtera
amesema pia wilaya hiyo inahitaji matundu ya vyoo 1,998 kati ya matundu 3,019
yanayohitajika na yaliyopo ni 1021 ambapo nyumba za walimu zinahitajika 1,139
lakini zilizopo ni nyumba 214 na kupungua 925.
Amesema pia
upungufu mwingine ni madawati 6,775 kati ya 23,710 yanayohitajika kwa ajili ya
kukaliwa na wanafunzi 87,063 kuanzia elimu ya awali mpaka darasa la saba
kukidhi kiwango cha taaluma na kwamba walimu wanaohitaji nyumba
ni 1,139 waliopo kati ya 2,086 wanaohitajika.
Amesema vyumba
vya madarasa vinahitajika 1,586 lakini yaliyopo ni 617 na kupungua vyumba
969 kutosheleza uwiano wa wanafunzi 45 katika chumba kimoja ambapo wilaya hiyo
inamiliki shule 85 za serikali zikiwemo nne za binafsi.
Amesema
licha ya mapungufu hayo wilaya ya biharamulo imekuwa na ufaulu wa miaka mitatu
kitaaluma mkoani kagera kuanzia mwaka 2015-2017 kwa wastani wa aslimia 85 mpaka
asilimia 92 kwa darasa la saba na asilimia 99.5 darasa la nne.
“Ufaulu
mzuri umechangiwa na juhudi za wadau wa elimu, wataalamu,wazazi
mashirika na taasisi mbalimbali wakiwemo viongozi wa kisiasa ambao huamasisha
jamii kutambua umuhimu wa elimu kwa mtoto” Alisema Nyamtera.
Hata hivyo
ametoa wito kwa jamii kuwasomesha watoto wa kike na walio na mahitaji maalum
kwa kuwapatia haki ya elimu katika shule zilizobainishwa ambazo ni kabindi na
Biharamulo mjini ambapo watapatiwa mahitaji husika.
Mwenyekiti
wa halmashauri ya wilaya hiyo Afsa Galiatano aliwataka wananchi wa wilaya hiyo
pia wadau mbalimbali kuchangia miundombinu katika shule za msingi na sekondari
kuboresha kiwango cha taaluma na kutimiza ndoto za watoto wao.
Aidha
amesisitiza viongozi kila kijiji kuhamasisha wazazi kutowatumikisha
wanafunzi na kusababisha utoro wa reja reja unaosababisha wazidi
kurudi nyuma katika masomo yao lakini kuwashauri watoto wa kike
kujihadhari na mapenzi ya kingono na kupata ujauzito katika umri
mdogo.
Ameongeza
kuwa baadhi ya changamoto zijadiliwe kuanzia ngazi ya vitongoji mikutano ya
kila baada ya miezi mitatu na kwenye vikao vya kamati ya maendeleo ya kata huku
vikwazo vingine vikifikishwa kwenye baraza la madiwani ili serikali ifanye
utekelezaji kwa kuunga nguvu kazi za wananchi.
Maadhimisho
ya wiki ya elimu wilayani Biharamulo yamefanyika katika kata ya Nyantakara
baada ya kufanya vizuri kitaaluma katika matokeo ya mtihani wa darasa la nne
miaka miwili mfululizo 2016 na 2017 kati ya kata 17 wilayani humo.
Na-Shaaban
Ndyamukama.
No comments:
Post a Comment