Na Shaaban
Ndyamukama –Ngara.
Wakulima wa
zao la maharage wameshauriwa kulima na kupanda mbegu ya aina moja shambani kwa
lengo la kupata mavuno bora yanayoweza kuwaingizia kipato kwa biashara badala
ya kutegemea matumizi ya chakula pekee ndani ya familia.
Ushauri huo
umetolewa na diwani wa kata ya Rulenge wilayani Ngara Hamisi Baliyanga
wakati akizungumza na waandishi wa habari za kilimo huku akihamasisha
wakulima wanaojiandaa kulima maharage ya rangi mchanganyiko katika
msimu wa kilimo cha mabondeni.
Bw Baliyanga
amesema maharage ya rangi mchanganyiko yanawapunja wakulima kibiashara
ukilinganisha na wanaovuna rangi moja wakati hatua za utayarishaji wa
shamba hadi kuvuna unafanana kati ya mkulima mmoja na mwingine.
Katika msimu
wa mavuno rangi moja inauzwa Shilingi 1200 hadi shilingi 1500 tofauti na rangi
mchanganyiko yanayouzwa Shilingi 500 mpaka shilingi 600 wakati maandalizi na
hatua za kilimo zinafanana” Amesema Baliyanga
Pia Afisa
ushauri wa kilimo kata ya Rulenge wilaya ya Ngara Bw Esau Nyamuziga
amewataka wakulima wa maharage kuvuna zao hilo mashambani kuepuka upotevu
wa mavuno na kupata hasara katika mapato na matumizi ya mbegu.
Nyamuziga amesema
wakulima hawana budi kutambua gharama za kilimo katika msimu mwingine
na kwamba uvunaji wa maharage kutoka shambani na kuyaandalia
nyumbani wanapata hasara ya kubaki baadhi ya mabegu shambani.
Aidha
ameshauri uvunaji huo ufanyike mapema kabla ya kukauka kwa muda mrefu kwani
maharage hupasukia kwenye maganda na mengine hupotea wakati wa usafirishaji kwa
kutumia kichwa, baiskeli na vyombo vingine vya usafiri.
“Uvunaji
mwingine wa maharage ni kujihadhari na upuraji kwa kutumia fimbo nzito katika sehemu
ngumu kwani yanaweka kupasuka punje zake kwa kutumia nguvu na kusababisha
kukosa soko kibiashara” Amesema Nyamuziga.
Wakizungumza
na Radio kwizera baadhi ya wakulima wamesema sababu ya
kupanda mbegu mchanganyiko ni kutokana na ardhi wanayotumia kutokuwa na
rutuba hivyo kutegemea mavuno ya kubahatisha katika misimu
mbalimbali.
Mmoja wa
wakulima hao ni Mzee Nicolaus Kanuma ambaye amesema baadhi mbegu zinastahimili
mvua na nyingine ukame hivyo wanapochanganya wanapata mavuno kulingana na
mabadiliko ya hali ya hewa.
Afisa kilimo
wilayani Ngara Bw Costantine Mudende amesema wakulima wilayani Ngara wataepuka
kulima mbegu mchanganyiko za maharage watakapoanza kupata mbengu mpya za aina
tano ambazo zimeanza kufanyiwa majaribio.
Hata
hivyo mkuu wa wilaya ya Ngara Luteni kanali Michael Mntenjele ameshauri
wakulima kutumia Radio Kwizera kupata elimu ya kilimo na kwamba radio
hiyo izingatie ratiba ya wakulima itakayonufaisha walengwa wa kipindi
husika.
No comments:
Post a Comment