|
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo
November 15 2017, amerejea jijini Dar es salaam akitokea kijijini kwake
wilayani Chato, mkoani Geita.
Baada ya kutoka Uwanja wa Ndege,
Rais Magufuli akiwa ameongozana na Makamu wa Rais Bi Samia Suluhu Hassan pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar
es salaam,amekagua Ujenzi wa Daraja la juu Tazara ( Tazara Fly-Over) na Ujenzi
wa Daraja la ghorofa tatu la Ubungo (Ubungo Interchange).
Akikagua maendeleo ya ujenzi wa
Daraja la Ubungo, Rais Magufuli amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara nchini
TANROADS Mkoa wa Dar es salaam Mhandisi Ndyamukama Julius kuvunja sehemu ya
jengo la TANESCO na jengo la Wizara ya Maji yaliyopo katika eneo la hifadhi ya
barabara ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya daraja hilo.
Sheria ya hifadhi ya barabara katika
eneo hilo ni mita tisini kila upande kutoka katikati ya barabara hivyo ni
lazima sheria hiyo iheshimiwe ili kuharakisha ujenzi wa Daraja la ghorofa tatu
katika eneo hilo la Ubungo uanafanyika bila vikwazo kwani sheria ni msumeno
haina budi kuzingatiwa hata na Serikali yenyewe amesema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli ameiagiza
TANROADS kutangaza tenda ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita kumi na
sita (16) kutoka eneo linapoishia Daraja la ghorofa tatu katika eneo la Ubungo
kuelekea Chalinze ili itanuliwe kwa lengo la kurahisha usafiri katika jiji la
Dar es salaam.
Rais Magufuli amewataka Makandarasi
wanaojenga Daraja la Tazara na Ubungo kuharakisha ujenzi wa madaraja hayo usiku
na mchana ili yaweze kumalizika kwa wakati ama kabla ya muda huo katika
kurahisisha maendeleo ya kibiashara katika jiji la Dar es salaam.
“Dar es salaam ni jiji la kibiashara
hivyo hakuna budi miundombinu yake ya usafiri iweze kurahisha usafirishaji wa
bidhaa mbalimbali kutoka ndani ya jiji na nje ya jiji la Dar es salaam’-Rais
Magufuli.
Mhandisi wa Masuala ya Usalama wa
Ujenzi Mhandisi Richard Baruani amemueleza Rais Magufuli kuwa Ujenzi wa Daraja
la Tazara umefikia asilimia 64 ambapo Daraja hilo linatarajiwa kukamilika mwezi
Oktoba 2018.
Kwa upande wa Daraja la ghorofa tatu
la Ubungo, Mhandisi Mshauri Reginald Kayanga amesema ujenzi wake unatarajiwa
kuanza rasmi Desemba 2017.
|
No comments:
Post a Comment