
Utawala wa
Rais Dkt.John Magufuli umebainisha mambo 10 yaliyofanyika katika kipindi cha miaka
miwili tangu ulipoingia madarakani.
Rais
Magufuli aliapishwa kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano Novemba 5,2015
akichukua nafasi iliyoachwa na Rais Jakaya Kikwete aliyehudumu kwa miaka 10
kuanzia 2005-2015.
Akitoa
tathimini ya utawala huo Jana Jumapili Novemba 5,2017 jijini Dar es Salaam,
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali,
Dk Hassan Abbasi amesema ndani ya miaka miwili mengi yamefanyika ambayo
ameyagawa katika maeneo 10.
Mosi, Dk Abbasi amesema uwajibikaji wa
watumishi wa umma na wananchi kwa jumla umekuwa mkubwa kwa kuwa kumekuwepo na
ari ya kufanya kazi.
Pili, amesema ni msukumo ambao Serikali
imeweka katika ukusanyaji wa kodi na kinachopatikana kinatumika ipasavyo.
"Zaidi
ya Sh236 bilioni ziliokolewa kutoka kwa walipa kodi zilizokuwa zinawalipa
watumishi hewa, tumeondoa watumishi wenye vyeti feki. Zaidi ya Sh142 bilioni
nazo zimeokolewa kutoka kwa watumishi walioghushi vyeti na zote zimeelekezwa
kutatua kero za wananchi," amesema Dk Abbasi.
Tatu, amesema vita ya ufisadi imekuwa
kubwa na imesaidia kuleta mageuzi na fedha ambazo zimekuwa zikiokolewa kutokana
na vita hiyo zinaelekezwa kwa wananchi kupitia miradi ya maendeleo.
"Kuna
Mahakama ya mafisadi imeanzishwa, kesi zake zinaanzia ngazi ya chini na mpaka
sasa kuna kesi tatu, mbili ziko Dar es Salaam na moja iko Mtwara na zingine 107
ziko ngazi za chini zinashughulikiwa," amesema.
Nne, amesema, "Serikali
inavyopigania rasilimali za Taifa. Vita katika eneo la madini tumefanya kupitia
upya mikataba na kubwa tumejitambua kama Taifa na sasa wawekezaji wanajua
Tanzania ukienda lazima uheshimu sheria."
Tano, Dk Abbasi amesema uamuzi mgumu lakini
makini uliofanywa na Serikali ingawa wapo waliopinga na kueleza haiwezekani,
lakini imewezekana.
"Watumishi
kutokwenda nje ya nchi, kati ya mwaka 2014/15, Sh216 bilioni zilitumika lakini
kwa miaka miwili hii ni Sh25 bilioni pekee ndizo zimetumika. Mimi nimesafiri
mara mbili tu," amesema akizungumzia moja ya uamuzi huo.
Amezungumzia
azma ya Serikali kuhamia Dodoma akisema imefanikiwa kwa sehemu kubwa na tayari
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yupo Dodoma. Amesema mwaka huu Makamu wa Rais,
Samia Suluhu Hassan atahamia na mwakani atakuwa ni Rais Magufuli.
Sita, ametaja ni azma ya nchi kujitegemea
akisema wananchi wanafanya kazi ili kutekeleza hilo. Amesema ukusanyaji mapato
umeongezeka kutoka Sh 9.9 trilioni hadi Sh 14 kwa mwaka.
Saba, amesema miradi mikubwa inatekelezwa
kama vile ujenzi wa reli ya kisasa na uboreshaji wa shirika la ndege, akisema
ununuzi wa ndege umefanyika na hadi Julai,2018 zitakuwa zimewasili
nchini.
Nane, amesema Serikali imeongeza bajeti
katika maeneo muhimu ya sekta za afya, elimu bure na miundombinu ya barabara.
"Kumekuwepo
na upatikanaji wa dawa katika hospitali zetu ukilinganisha na awali, hii
inasaidiwa na mkakati wa Serikali wa kununua dawa moja kwa moja kwa wazalishaji
na bajeti ya Wizara ya Afya imeongezeka kutoka Sh 30 bilioni hadi Sh 261 bilioni,
yote haya ni mafanikio ya miaka miwili," amesema.
Tisa, Dk Abbasi amesema Rais Magufuli
amekuwa akiahidi na kutekeleza.
Kumi, amesema suala la Tanzania ya
viwanda licha ya kueleza ni gumu lakini ni lazima nchi ielekee huko.





No comments:
Post a Comment