Watu watatu wafariki katika matukio mawili tofauti katika wilaya ya Muleba na Ngara mkoani Kagera, likiwemo la ajali ya gari. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Sunday, September 11, 2016

Watu watatu wafariki katika matukio mawili tofauti katika wilaya ya Muleba na Ngara mkoani Kagera, likiwemo la ajali ya gari.

Watu watatu wamefariki katika matukio mawili tofauti katika wilaya ya Muleba na Ngara mkoani Kagera, likiwemo la ajali ya gari na kusababisha majeruhi tisa ambao wamelazwa katika hospitali ya Nyamiaga wilayani Ngara. 

Katika tukio la kwanza huko wilayani Muleba watu wawili wamefariki kwa kuzama ndani ya ziwa viktoria katika kijiji cha Katembe kata ya Nyakabango ambapo Mwenyekiti wa kijiji hicho Edson Timotheo amemtaja mtu mmoja aliyetambulika kuwa ni Rastus Audax (34) mkazi wa kijiji hicho.

Timotheo amesema  marehemu    mwingine hakufahamika jina lake na amezikwa baada ya kukosa jamaa zake na kwamba walionusurika ni Sebastian Simon (17) na Daniel Onesmo (17) ingawa hawakutaja makwao na kwamba walikuwa wakivua kwa kutumia kokolo

“Watu hao watatu hawakufahamika wanakotokea na walimshawishi mkazi wa kijiji hiki kuwasindikiza ziwani na ndipo wakakutwa na mauti na walijificha kwani walikuwa wakivua kwa njia haramu”
Katika tukio lingine limetokea wilayani Ngara, ambapo mtu mmoja amefariki dunia na wengine tisa  kujeruhiwa baada ya kupata ajali ya gari kijiji cha  Kumuyange wakielekea kusomba matofali na mawe ya ujenzi wilayani humo.

Mkuu wa Jeshi la Polisi wilayani humo, Abel Maige amemtaja aliyepoteza maisha kuwa ni  Issa Rushenza (35) mkazi wa kijiji cha Buhororo na kwamba ajali hiyo ilitokea septemba 10,2016 saa 9:15 mchana na chanzo cha ajali hiyo ni kupoteza mfumo wa breki kisha gari hilo kupinduka.

Majeruhi hao ni Machumi Marco (27) Paschal Marco (40), Elias Rushenza (25), Paschal Marcel (29), Malianus Marchardes (28) wakazi wa kijiji cha Buhororo, wengine ni  Zaburi Cosmas (23) wa kumuyange, Alifa Mussa (40) wa Mubinyange pamoja na Aloys Hilali (32) wa Nyamiaga wote wakazi wa wilayani Ngara.

Amesema gari lililosababisha ajali hiyo ni aina ya Isuzu lenye namba za usajili  T851 DDQ mali ya Nikolaus Kidenke wa  Ngara na kwamba uchunguzi wa Jeshi la Polisi unaendelea, ambapo amewataka wamiliki na madereva kuhakikisha wanaanza safari wakiwa wamejiridhisha na usalama wa vyombo vyao vya usafiri.

BY SHAABAN NDYAMUKAMA

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad