Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Dkt John Pombe Magufuli akiongoza mkutano wakati wa Mkutano wa 17 wa
Dharura wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ukumbi wa mikutano wa
Ikulu jijini Dar es salaam ,Septemba 8, 2016.
Anafuatiwa
na Rais Paul Kagame wa Rwanda, Mwakilishi maalum wa Rais wa Sudan ya Kusini Mhe
Aggrey Tisa Sabuni, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt
Ali Mohamed Shein na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Liberat
Mfumukeko.
Wakuu wa
nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana kutumia kipindi cha miezi 3
hadi Januari mwakani ili kuupitia upya mkataba wa mahusiano ya kiuchumi na
kibiashara kati ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ulaya (EPA) kabla ya
kukubaliana na baadhi ya vipengele vya mkataba huo.
Akizungumza katika mkutano wa dharura wa 17 wa
Jumuiya hiyo Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alisema hatua hiyo
imetokana na mjadala na majadiliano ya kina kutoka kwa Wakuu wa Jumuiya hiyo.
Rais Magufuli alisema kwa mujibu wa mkataba
huo, Umoja wa Ulaya ulitaka mkataba huo usainiwe mwaka huu, ambapo hata hivyo
kwa kuzingatia maslahi na ustawi wa jumuiya hiyo, viongozi wa nchi wanachama
wamehitaji muda zaidi wa kufanya maamuzi juu ya mkataba huo.
Dkt. Magufuli alisema kufuatia uamuzi huo,
Viongozi hao wameitaka Sekretarieti ya Jumuiya hiyo kuandaa utaratibu wa
kusimamia masuala ya mahusiano kuhusu mkataba huo kwa kufanya mawasiliano na
Umoja wa Ulaya.
“Tumewaomba wenzetu wa Umoja wa Ulaya
wasiiadhibu nchi ya Kenya kwa kuwashinikiza kusaini mkataba wa EPA ifikapo
oktoba mosi mwaka huu, ni vyema nchi zote wanachama tujiridhishe na vipengele
vya mkataba huo kabla ya kuweka saini ya makubaliano” alisema Rais Magufuli.
Akitolea mfano baadhi ya sababu zinazoifanya
nchi za Jumuiya hiyo kuhitaji muda zaidi wa majadiliano kuhusu mkataba huo ni
pamoja na uhakika wa kulinda viwanda vya ndani vya nchi wanachama, njia bora za
kulinda maslahi ya wakulima, namna bora ya makusanyo ya kodi za bidhaa kutoka
nchi za Ulaya.
|
No comments:
Post a Comment