|
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameviagiza vyombo vya
dola kuchunguza na kuchukua hatua za kurejesha mali za Chama Kikuu cha Ushirika
cha Nyanza ambazo zilinunuliwa na
kutwaliwa na watu binafsi kwa njia za ujanja ujanja.
Rais
Magufuli ametoa agizo hilo tarehe 11 Agosti, 2016 alipokuwa akiwahutubia
wananchi wa Mwanza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa
Furahisha Jijini Mwanza.
Dkt.
Magufuli alisema Serikali yake haipo tayari kuwafumbia macho watu wachache
waliovifilisi vyama vya ushirika vya wakulima kwa kujimilikisha mali za
ushirika yakiwemo majengo, viwanda na mashamba na ametaka mali hizo zirudishwe
mikononi mwa wananchi.
"Hata
kama walichukua miaka 20 iliyopita, vyombo vya dola vichukue hatua na mali hizo
zirudishwe kwa umma" Alisema Rais Magufuli.
Katika
Mkutano huo Rais Magufuli pia alisema Serikali itafanya oparesheni kubwa ya
kuteketeza Makokoro katika ziwa Victoria ikiwa ni juhudi za kukabiliana na
tatizo la uvuvi haramu uliosababisha kupungua kwa samaki na kuathiri shughuli
za uvuvi na usindikaji wa minofu ya samaki katika viwanda.
Alibainisha
kuwa lengo la kuchukua hatua hiyo ni kuwezesha samaki wengi kuzaliana ili lengo
la Serikali la kujenga viwanda vya kusindika mazao ikiwemo viwanda vya
kusindika minofu ya samaki lifanikiwe.
Kabla ya
kuhutubia mkutano huo Rais Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja
la waenda kwa miguu la Furahisha linalokatiza barabara ya Uwanja wa Ndege
kwenda katikati ya Jiji la Mwanza.
Daraja hilo
litakuwa na urefu wa meta 46, upana wa meta 3.6 na kimo cha meta 5.5 na ujenzi
wake unatarajiwa kukamilika Mwezi Desemba Mwaka huu kwa gharama ya Shilingi
Bilioni 6.455
Akizungumzia
ujenzi huo Rais Magufuli alimtaka Mkandarasi anayejenga Daraja la Furahisha
kukamilisha kazi hiyo Mwezi Desemba Mwaka huu kwa mujibu wa mkataba, na pia
ameagiza Mkandarasi aliyekuwa akifanya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza
kuendelea na kazi hiyo ndani ya wiki moja kwa kuwa Serikali imejipanga kumlipa
fedha za kazi hiyo.
Pia Dkt.
Magufuli ameahidi kuongeza fedha katika ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka
Katikati ya Jiji la Mwanza hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza ili barabara hiyo
ifike hadi uwanjani badala ya kuishia eneo la Pasiansi.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Mwanza
11 Agosti,
2016.
|
No comments:
Post a Comment