Polisi Mwingine Auawa katika Mapambano Makali na Majambazi –Mkuranga. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Saturday, August 27, 2016

Polisi Mwingine Auawa katika Mapambano Makali na Majambazi –Mkuranga.

Ilikuwa ni kama filamu ya askari na maadui wakati askari wa Jeshi la Polisi walipopambana na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi kwenye nyumba iliyo eneo la Vikindu wilayani Mkuranga.

Taarifa ambazo zimepatikana kutoka kwa watu waliokuwa karibu na operesheni hiyo na ambazo hazijathibitishwa na mamlaka rasmi, zinasema kamishna wa Kitengo cha Kuzuia Ujambazi, ASP Thomas Njuki aliuawa kwa kupigwa risasi kichwani.

Taarifa hizo zilisema kuwa jambazi mmoja aliuawa ingawa idadi ya waliokamatwa haikufahamika mara moja kutokana na mashuhuda kutoa takwimu tofauti.

Kamanda wa Polisi wa Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema ataongea na waandishi wa habari leo saa 4:00 asubuhi kuzungumzia tukio hilo.

Tukio hilo limetokea siku chache baada ya askari wanne wa Jeshi la Polisi kuuawa wakati wakibadilishana lindo kwenye tawi la benki ya CRDB lililoko Mbande jijini Dar es Salaam.

Nyumba waliokuwa Wanaishi hao Majambazi.

Watu hao, waliofika wakiwa wamepanda pikipiki, walipora silaha na kutoweka nazo. Katika tukio la jana, askari wa Jeshi la Polisi walikuwa na nia ya kuwakamata watu waliowashuku kuwa ni majambazi.

Kwa mujibu wa watu wanaoishi karibu na nyumba hiyo, mpambano kati ya polisi na majambazi hao ulianza saa 7:30 usiku baada ya polisi kuvamia nyumba walimopanga majambazi hayo.

Tukio lilivyotokea.

Chanzo kimoja cha habari kimeeleza kuwa baada ya polisi kufuatilia nyendo za wakazi wa nyumba hiyo walianza upelelezi na kubaini kuwa huenda wanahusika na matukio kadhaa ya uhalifu, likiwamo la uvamizi wa kituo cha polisi cha Stakishari na lile la tawi la CRDB Mbande mkoani Pwani.

Mpashaji huyo alisema kuwa jana saa saba usiku, polisi walifika kwenye nyumba hiyo iliyo Mtaa wa Vikindu Mashariki ambayo ina maduka upande wa mbele, ikipakana na nyumbani nyingine mbili pembeni na nyuma zikiwa umbali usiozidi hatua nne.

Habari hizo zinasema askari hao kwanza walimtuma mwenyekiti wa serikali ya mtaa kwenda kuwasihi wafungue mlango na walipokataa ndipo walipoenda kugonga, wakiwaamrisha watu hao wafungue mlango.

Baada ya kuona hawatii amri ya kufungua mlango, polisi waliamua kuvunja vitasa kwa kutumia bastola, ndipo risasi zikaanza kurushwa,” alisema mpashaji habari huyo.

 Kwa kuwa mkuu alikuwa mbele, wahalifu walimpiga risasi kichwani na alikufa palepale.”
Mtu huyo alisema kuwa baada ya Kamishna Njuki kufariki, askari wengine walirudi nyuma kujihami zaidi.

Baada ya hapo polisi waliendelea kupiga risasi kuelekea maeneo mbalimbali ya nyumba hiyo na wahalifu hao kujibu mashambulizi.

Kila chumba ambacho polisi walikuwa wakijaribu kurusha risasi, zilijibiwa. Inaelekea kila chumba kilikuwa na mtu mwenye silaha,” alisema shuhuda mwingine wa tukio hilo.

Habari kutoka kwa majirani zinasema hadi saa 2:45 asubuhi, milio ya risasi iliendelea kurindima katika eneo hilo.

Baadaye polisi waliomba kuongezewa nguvu na Jeshi la Wananchi (JWTZ) ambao walifika na kuendeleza mapambano hayo.

 Mtoto ataja alipojificha baba.

Wakati mapambano yakiendelea, sauti za watoto waliokuwa wakilia zilisikika na ndipo askari wa JWTZ waliamuru watu hao wawatoe nje.

Watoto walipotoka nje, polisi waliwauliza baba yupo wapi, mtoto mmoja akajibu yupo darini,” alisema

Baada ya polisi kusikia hivyo, walielekeza mashambulizi yao darini na kufanikiwa kumjeruhi mtu aliyejificha darini ambaye alishuka.

Wakati polisi wakishinikiza atoke ndani ili kujisalimisha, mtu huyo alijipiga risasi mara baada ya kutoka na kufariki dunia.
Wakazi Vikindu wahaha!

Kutokana na tukio hilo, taharuki ilitanda kwa wakazi wa Vikindu na biashara zote zilifungwa eneo hilo huku wananchi wakiwa na chupa za maji kutokana na mabomu ya machozi yaliyokuwa yakipigwa kila mara.

Wakazi wa eneo ambalo lipo karibu na maegesho ya magari ya Farid Seif, hawakuruhusiwa kutoka ndani na waliofanikiwa kutoka usiku hawakuingia hadi jana saa 7.00 mchana wakati hali ilipotulia.

Kutokana na majibizano ya risasi, watu wanaofanya kazi jijini Dar es Salaam ambao wanaishi vijiji vya Melela, Vianzi, Pemba Mnazi na Mfuru hawakwenda kazini kutokana na barabara inayotoka Vikindu kufungwa hadi saa 7.00 mchana.

Tukio hilo lilisababisha umati wa watu kukusanyika kushuhudia mapambano hayo, lakini hakuna raia aliyeruhusiwa kuvuka mita 150 kwenda eneo la tukio.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad