Tume ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa na matamshi ya Mhe. Paul
Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam yanayokiuka misingi ya utawala bora
aliyoyatoa tarehe 25 Agosti, 2016 wakati wa kuaga miili ya askari Polisi watatu
waliouawa Mbande, Mkoani Dar es Salaam.
Kwa mujibu
wa Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Bahame Tom Nyanduga, leo (Agosti 26, 2016) Mhe.
Makonda ametumiwa barua ya wito inayomtaka afike makao makuu ya Tume mtaa wa
Luthuli, tarehe 30 Agosti, 2016 ili kujadili kile Tume ilichokiona kuwa ni
kejeli kwa Tume pamoja na jumuiya yote ya watetezi wa haki za binadamu.
Aidha, Tume
imeona kuwa maagizo aliyoyatoa Mkuu huyo wa Mkoa kwa Jeshi la Polisi hayana
msingi wa kisheria na hayako ndani ya mamlaka ya Mkuu wa Mkoa.
Kwa mujibu
wa Kifungu cha 6(1)(f) na (i) pia Kifungu cha 27(1) na (2) (a) vya Sheria ya
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Sura Na. 391 ya Sheria za Tanzania
2002, THBUB ina mamlaka ya kuchunguza mwenendo wa mtu au taasisi yoyote
kuhusiana na utendaji wa kazi zake zinapokiuka mipaka ya madaraka yake, ili
kuchukua hatua za kurekebisha ukiukwaji huo.
Imetolewa
na:
(SIGNED)
Idara ya
Elimu kwa Umma na Mafunzo
TUME YA HAKI
ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Agosti 26,
2016.
|
No comments:
Post a Comment