|
Vyama tisa
vya siasa kati ya 22 vyenye usajili wa kudumu vipo hatarini kufutwa kutokana na
kushindwa kukidhi vigezo na matakwa ya kisheria yaliyoviwezesha kupata usajili
wa kudumu.
Hatua ya
kufutwa vyama hivyo, vikiwamo baadhi visivyo na ofisi za kudumu (vyama vya
mfukoni) itafikiwa ikiwa vitashindwa kujieleza kutokana na makosa ambayo Ofisi
ya Msajili wa Vyama vya Siasa imebaini katika ukaguzi uliofanyika hivi karibuni
Bara na Visiwani.
Jukumu kubwa
la Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni kusimamia, kuboresha, kuendeleza na
kudumisha demokrasia ya vyama vingi hapa nchini majukumu ambayo yanatokana na
Sheria ya Vyama vya Siasa Na. 5 ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi
Na. 7 ya mwaka 2010.
Majukumu
mengine ya ofisi ya msajili ni kusajili vyama vya siasa na kuvifuta vyama
ambavyo havikidhi matakwa ya sheria hiyo na kusimamia ugawaji wa ruzuku ya
Serikali kwa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza ofisini kwake jana, Msajili wa
Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alisema uhakiki uliofanywa na
ofisi yake katika vyama hivyo upande wa Bara na Visiwani umebaini kasoro nyingi
zikiwamo za ukiukaji wa masharti ya usajili.
“Katika uhakiki uliofanywa na ofisi yangu
tumebaini kasoro mbalimbali ambazo kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa ni
miongoni mwa vigezo muhimu vinavyoangaliwa ili chama kiwe na sifa ya
kusajiliwa,” alisema.
“Kasoro
tulizozibaini ni nyingi na baadhi ya vyama kutokana na mapungufu waliyo nayo
huhitaji kutoa nafasi tena….unaweza kuvifuta hapohapo.”
Msajili
hakutaka kutaja majina ya vyama hivyo ambavyo tayari vimeandikiwa barua lakini
alitaja makosa kuwa baadhi havina ofisi za kudumu Tanzania Bara na Visiwani au
upande mmoja na vingine havina anuani ya posta.
“Unakuta
chama fulani kina ofisi labda Zanzibar lakini hakina ofisi Bara,” alisema Jaji
Mutungi. Alisema vyama vingine havina viongozi wa kitafa kutoka pande mbili za
Muungano na pia havina bodi ya wadhamini iliyosajiliwa kwa Wakala wa Usajili
Ufilisi na Udhamini (RITA) kama sheria inavyohitaji.
Katika
ukaguzi huo, Msajili alibaini pia kasoro nyingine kuwa ni kukosekana kwa orodha
ya wanachama wa chama husika jambo alilosema nalo ni muhimu kila chama kuwa na
orodha ya idadi ya wanachama wake.
Vilevile,
baadhi ya vyama hivyo vimeshindwa kuonyesha akaunti ya fedha ya chama hali
inayotia shaka namna vinavyojiendesha.
|
No comments:
Post a Comment