Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema hakuna kiongozi yeyote
wa kisissa nchini anayemuogopa.
Aidha, Dk.
Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar ameahidi kumchukulia hatua yeyote
atakayevunja sheria za nchi.
Amesema kuna baadhi ya wananchi, hasa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif
Hamad, ambaye amekuwa akivunja sheria za nchi kwa makusudi huku akijisifu na
kuona kama serikali inamuogopa jambo ambalo sio sahihi.
Makamu Mwenyekiti huyo alitoa msimamo huo wakati akizungumza na mamia ya
viongozi wa CCM, wakiwemo Mabalozi, Wenyeviti na Makatibu wa Matawi na Maskani
za Wilaya ya Mfenesini Kichama.
Mkutano huo ulifanyika katika Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere, Bububu
nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Dk. Shein alisema Zanzibar ina Rais mmoja ambaye ni yeye na kama kuna watu
wanatamani nafasi hiyo ni lazima wachaguliwe kihalali.
Alikemea tabia za Maalim Seif ya kujaribu kila mara kuingiza nchi katika
machafuko na aliahidi kuwa vyombo vya dola havitavumilia.
Alisema tayari dola inaendelea na taratibu za kisheria na endapo akitiwa
hatiani atahukumiwa kisheria.
Maalim Seif alihojiwa na Polisi kwa saa tatu katikati ya wiki kabla ya kuachiwa
kwa dhamana ya wadhamini wawili.
“Mimi simuogopi Maalim Seif kwani ni kiongozi wa kisiasa kama mimi, ila
tofauti yetu ni kwamba mimi ni Rais wa Zanzibar na yeye ni kiongozi wa
chama," alisema na kueleza "hivyo haniwezi kwa
lolote."
"Kwa mambo anayofanya, endapo akishitakiwa na kutiwa hatiani ajue
kwamba kisheria kosa lolote la jinai halifi na wakati wowote anaweza kukamatwa
na kushitakiwa endapo mahakama ikiona kuna haja ya kufanya hivyo."
Dk. Shein alisema Maalim Seif hawezi kuogopwa kwani hana vifaru, roketi
renja za kivita vya kuwatisha watu wamuogope.
Alisema sheria ndio kinga dhidi ya migogoro ya Zanzibar na kiongozi yeyote
atakayejifanya mbabe, hata akiwa rais wa nchi, sheria zitamshughulikia.
Aliwaambia wananchi wa Zanzibar wanaoona Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984
inavunjwa ama inataka kuvunjwa, wana haki ya kufungua mashtaka Mahakamani kwa
mujibu wa kifungu cha 25 1(a).
Aidha aliahidi kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka
2015/2020 hadi ifikie asilimia 90 ili wananchi waendelee kupata maendeleo kwa
wakati.
Dk. Shein alisema ahadi hiyo itatekelezwa kwa wakati endapo wananchi
wataendelea kushirikiana vizuri na serikali katika shughuli na harakati mbali
mbali za maendeleo ya nchi.
Rais shein alifafanua kwamba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, CCM
Zanzibar imetekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010/2015 kwa asilimia 80.
Alisema kwamba mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri baina ya wananchi
na viongozi mbali mbali wa Chama na serikali kwenye kuharakisha maendeleo ya
nchi.
Aidha aliwapongeza wafuasi wa CCM katika Wilaya hiyo kwa kuichagua kwa kura
nyingi CCM, katika Uchaguzi wa Marudio wa Machi 20 na kupata ushindi wa zaidi
ya asilimia 90.
Alisema kwamba ushindi huo ni taswira ya mafanikio ya Chama na serikali katika
kuwatumikia wananchi kwa uadilifu mkubwa huku ikijipanga kuimarisha uchumi wa
nchi kufikia uchumi wa kati.
“Uchaguzi Mkuu umekwisha hivyo kwa sasa tufanye kazi kwa pamoja kuendeleza
maendeleo ya Zanzibar kwani kila jambo lenye tija na manufaa linahitaji umoja
na ushirikiano kutoka kwa wananchi,” alisema Dk. Shein na kuongeza:
“Pia nakuombeni wafuasi wa CCM muendelee kuwa wavumilivu licha ya kuwepo kwa
changamoto mbalimbali za kisiasa kutoka kwa wapinzani.
"Jambo hilo linatafutiwa ufumbuzi na vyombo vya kisheria."
Dk. Shein alisema ataendelea kusimamia Sheria na Katiba ya Zanzibar kwa misingi
ya uadilifu, lakini hatawavumilia watu wanaovunja sheria kwa makusudi.
|
No comments:
Post a Comment