Serikali inatarajia kumwaga ajira kwa askari katika mwaka ujao wa fedha.Taarifa juu ya
ajira hizo, zilitolewa jana,May 16,2016, Bungeni
na Waziri mwenye dhamana.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato ya
Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2016/2017 kuhusu ajira za askari, Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga alisema wataajiriwa askari wapya 3,700
katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Waziri Kitwanga alisema mbali ya
kuajiri askari hao, pia watawapandisha vyeo askari 7,140, wakaguzi 1,325 na
maofisa 991.
Alisema katika mwaka 2015/2016, jumla
ya askari polisi wapya 3,882 waliajiriwa, na askari wakaguzi na maofisa 4,065
wa vyeo mbalimbali walipandishwa vyeo kwa kufuata utaratibu wa ajira.
“Aidha, serikali imeendelea kuhuisha
viwango vya mishahara na posho mbalimbali, ikiwemo posho ya chakula ambayo
iliongezwa kutoka Sh 180,000 hadi kufikia Sh 300,000 kwa mwezi,” alieleza
Waziri Kitwanga.
Alisema katika mwaka ujao wa fedha,
Jeshi la Polisi litaongeza umakini katika kusimamia nidhamu kwa askari wake kwa
kufanya uchambuzi wa kina (vetting) kwa kuchukua vijana waliomaliza mafunzo ya
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wanaoomba kujiunga na Jeshi la Polisi ili kuwa na
askari wenye nidhamu na moyo wa dhati wa kulitumikia Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wa Jeshi la Magereza,
alisema linatarajia kutoa mafunzo kwa maofisa na askari 4,975 katika ngazi
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na yale ya Taaluma ya Urekebishaji.
Alisema ili kukabiliana na changamoto
ya uchache wa miundombinu ya makazi kwa askari Polisi, serikali kupitia mkopo
kutoka Serikali ya China inakusudia kujenga nyumba 4,136 chini ya usimamizi wa
Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi.
Akizungumzia Jeshi la Zimamoto na
Uokoaji, alisema jeshi hilo linahitaji vituo 152 Tanzania Bara, lakini kwa sasa
lina vituo 57 na kati ya hivyo, 38 vipo katika miji na 19 katika viwanja vya
ndege.
Alisema huo ni upungufu wa vituo 95
hali inayosababisha maeneo mengi kukosa huduma za zimamoto na uokoaji.
Inategemea kujenga kituo kimoja cha
zimamoto na uokoaji katika eneo la Kigamboni katika Jiji la Dar es Salaam na
kuendelea na ujenzi wa Jengo la Makao Makuu Tazara - Mchicha, Dar es Salaam.
Aidha, alisema Jeshi la Polisi
litaendelea kupambana na makosa yanayovuka mipaka hususani ugaidi, uharamia,
biashara ya dawa za kulevya, biashara haramu ya kusafirisha binadamu, wizi wa
vyombo vya moto hususani magari, wizi wa kutumia mitandao ya Tehama, bidhaa
bandia, na biashara haramu ya silaha na uchafuzi wa mazingira.
|
No comments:
Post a Comment