|
Mhe. Dkt.
John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa pamoja na Mhe. Salva Kiir Mayardit, Rais wa
Jamhuri ya Sudan Kusini wamesaini Mkataba wa kuiwezesha Jamhuri ya Sudan Kusini
kuwa Mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Tukio hilo la
kihistoria limefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 15 Aprili, 2016.
Akizungumza
wakati wa haflya hiyo, Mhe. Dkt. Magufuli aliipongeza nchi hiyo na kusema kuwa
anajivunia tukio hili la kihistoria kutokea wakati Tanzania ikiwa ni Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba ukurasa mpya wa ushirikiano na
mahusiano na nchi hiyo umefunguliwa.
Aliongeza
kuwa kihistoria Sudan Kusini, imekuwa na mahusiano ya karibu na nchi za Afrika
Mashariki katika nyanja mbalimbali ikiwemo mwingiliano wa tamaduni, ushirikiano
wa kibiashara na uchumi na ukaribu wa kijografia. Aidha, alieleza kuwa kujiunga
kwa Sudan Kusini kwenye EAC kunaifanya Jumuiya hii kuwa na soko kubwa lenye
takriban watu milioni 160.
Vile vile
Mhe. Rais Magufuli alisema kuwa ili Jumuiya ya Afrika Mashariki iweze kuwa na
maendeleo endelevu suala la kudumisha amani ni la msingi, hivyo aliwahimiza
Sudan Kusini kuendeleza juhudi kwenye mazungumzo ya amani.
‘’Dhana ya
Mtangamano ni kukuza biashara, uwekezaji na miundombinu ili kujiletea maendeleo
endelevu katika Jumuiya yetu, hivyo nahimiza umuhimu wa nchi wanachama
kudumisha amani ili kufikia malengo tuliyojiwekea ‘’ alisema Rais Magufuli.
Wakati
huohuo, Rais Magufuli alimpongeza Rais Kiir kwa jitihada zake katika
kuhakikisha nchi yake inajiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki haraka ambapo
miezi minne baada ya nchi hiyo kupata uhuru iliwasilisha maombi ya kujiunga na
Jumuiya ya Afrika Mashariki na miaka mitano imeweza kuwa mwanachama kamili wa
Jumuiya hiyo.
Kwa upande
wake, Rais Kiir alieleza kufurahishwa kwake na hatua iliyofikiwa na nchi yake
ya kuwa mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, alimshukuru
Rais Magufuli na Marais wa Nchi zote wanachama kwa kuiunga mkono nchi yake kwa
kauli moja.
Mhe. Kiir
aliongeza kuwa uamuzi wa nchi yake wa kujiunga na Jumuiya ni wa dhati na kwamba
una nia ya kuimarisha ushirikiano kwa manufaa ya wananchi wa Afrika Mashariki
kwa ujumla, ambapo nchi yake imeshaanza kufanyia mabadiliko mifumo mbalimbali
kwenye Serikali yake ili kuweza kushiriki kikamilifu katika hatua mbalimbali za
mtangamano ikiwemo kuunda Wizara inayoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.
‘’Hatimaye
Sudan Kusini imerudi nyumbani. Jumuiya ya Afrika Mashariki ni sehemu sahihi kwa
nchi yangu kwani Jumuiya ya Afrika Mashariki ni mtangamano unaoheshimika Afrika
na Duniani kwa ujumla’’ alisisitiza Rais Kiir.
Pia, Rais
Kiir alitangaza kufunguliwa rasmi kwa Ubalozi wa nchi yake hapa nchini na
tayari amemteua Balozi Mariano Deng Ngor kuwa Balozi wa Sudan Kusini nchini
Tanzania.
Awali
akizungumza kabla ya kusainiwa kwa Mkataba huo, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga alisema kuwa Jumuiya ya
Afrika Mashariki itashirikiana kwa karibu na Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha
wananchi wa Sudan Kusini waliothirika na migogoro na kuikimbia nchi yao
wanarejea kwa ajili ya kuendeleza nchi yao.
Jamhuri ya
Sudan Kusini ilipata uhuru wake tarehe 09 Julai, 2011 na iliwasilisha maombi
rasmi ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki tarehe 10 Novemba, 2011.
Aidha,
Tangazo la kukubaliwa kuwa Mwanachama wa EAC lilitangazwa na Mwenyekiti wa
Jumuiya hiyo, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania wakati wa Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi wa EAC uliofanyika jijini
Arusha mwezi Machi 2016.
|
No comments:
Post a Comment