|
HOTUBA YA
MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KWENYE MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI – PARK HYATT
ZANZIBAR, TAREHE 10 APRILI, 2016.
Ndugu zangu
Waandishi wa Habari,
Ndugu
Waalikwa,
Naanza kwa
kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na uzima tukaweza
kukutana hapa leo.
Namshukuru
Mwenyezi Mungu pia kwa kuijaalia nchi yetu kwa kiasi kikubwa kubaki katika hali
ya amani na utulivu licha ya jitihada kubwa zilizofanywa na zinazoendelea
kufanywa na baadhi ya watu za kuivuruga amani yetu.
Naendelea
kumuomba Mola wetu aendelee kuibariki nchi yetu na watu wake, aijaalie kuwa
nchi ya amani na atujaalie hekima na busara katika kuendesha mambo yetu.
Nichukue
fursa hii pia kukushukuruni nyinyi waandishi wa habari kwa kuitikia wito wetu
na kuja kutusikiliza. Shukrani maalum zije kwenu wale ambao mmesafiri kutoka
Dar es Salaam na kuja Zanzibar makhsusi kwa ajili ya mkutano huu.
Tunathamini
sana mashirikiano yenu nyote tukitambua nafasi na mchango mkubwa wa vyombo vya
habari katika maendeleo ya nchi yoyote ile.
Mtakumbuka
kwamba siku saba zilizopita tulizungumza nanyi ambapo tuliwasilisha kwenu
maazimio 13 ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama Cha Wananchi (CUF)
kuhusiana na msimamo wa Chama chetu dhidi ya ubakaji wa demokrasia Zanzibar
uliofanyika tarehe 20 Machi, 2016 na ambao ulipewa jina la uchaguzi wa marudio.
Leo hii
tumekuiteni ili kutimiza agizo nililopewa na Baraza Kuu lililonitaka nizungumze
na wananchi wa Zanzibar ili kuwaeleza kwa kina mwelekeo wa hali ya kisiasa ya
Zanzibar na hatua zinazochukuliwa na CUF kuhakikisha maamuzi halali ya
kidemokrasia ya Wazanzibari waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015 yanaheshimiwa.
UCHAFUZI WA TAREHE 20 MACHI, 2016
Nilieleza
kwa urefu katika mkutano wangu na waandishi wa habari wa tarehe 11 Januari,
2016 nilioufanya Dar es Salaam juu ya nini kilitokea baina ya tarehe 25 Oktoba
2015 hadi tarehe 28 Oktoba, 2015, siku ambayo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar, Jecha Salim Jecha, alitoa tangazo batili na haramu la kufuta uchaguzi
huru na wa haki uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015.
Nilieleza pia hoja za
kikatiba na kisheria za kwa nini tangazo lile ni haramu na batili na hoja zile
hadi leo watawala wameshindwa kuzijibu.
Kwa hoja
hizo hizo, nikaeleza kwamba hakuna vifungu vya Katiba wala Sheria ya Uchaguzi
ya Zanzibar Nam. 11 ya 1984 vinavyozungumzia kitu kinachoitwa uchaguzi wa
marudio ukiondoa pale inapotokea wagombea wanapopata idadi sawa ya kura.
Sikusudii
kurudia yale ambayo nilishayaeleza siku ile maana hayo sasa yanaeleweka na kila
mtu ndani na nje ya nchi.
Leo hii
nataka niwapongeze kwa mara nyengine tena wananchi jasiri na shupavu wa
Zanzibar kwa kuitumia tarehe 20 Machi, 2016 kukifedhehesha Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kwa mara ya pili ndani ya miezi sita mbele ya macho ya Watanzania na
mbele ya macho ya jumuiya ya kimataifa.
Wananchi
wazalendo wa Zanzibar wanaoipenda nchi yao waliwakataa watawala waovu wa CCM na
sera zao mbovu zinazoidhalilisha Zanzibar yao kupitia sanduku la kura tarehe 25
Oktoba, 2015.
Watawala
waovu wa CCM wakaamua kutumia mabavu na uvunjwaji wa katiba na sheria
kuyapindua maamuzi ya Wazanzibari, kwa sababu tu maamuzi hayo yalikuwa ni ya
kuwakataa watawala hao.
Kwa miezi
mitano kuanzia Oktoba 2015 hadi Machi 2016, watawala waovu wa CCM wakawaingiza
wananchi watulivu na wanaopenda amani wa Zanzibar katika idhilali na hilaki
kubwa kwa kuwazuilia haki zao za msingi za binadamu ili wasiweze kuonesha hisia
zao dhidi ya watawala.
Kwa namna ya
pekee na ya ustaraabu wa hali ya juu na wa kupigiwa mfano, wananchi wa Zanzibar
wakaisubiri tarehe 20 Machi, 2016 na wakapeleka ujumbe wao kwa watawala hao na
kwa dunia nzima kwa njia za amani za kuususia uchafuzi ulioitishwa siku hiyo.
Hali halisi
iliyoonekana na kila aliyetaka kuona ni kwamba zaidi ya asilimia 80 ya
Wazanzibari hawakwenda kupiga kura siku hiyo ili kuonesha hisia zao na
kuthibitisha tena maamuzi yao ya tarehe 25 Oktoba, 2015.
Kituo cha
televisheni cha ITV kilichokuwa kikirusha matangazo ya moja kwa moja kutoka
katika mikoa mitano ya Unguja na Pemba kilionesha vile vilivyoitwa vituo vya
kupigia kura vikiwa havina watu kabisa au vikiwa na watu wachache sana.
Walipowahoji
wale walioitwa maofisa uchaguzi na walioitwa mawakala kila mmoja alikuwa akija
na majibu yake na takwimu zake zinazopingana na za mwenzake.
Vituo vya
televisheni vya kimataifa hasa kile cha Al-Jazeera na CCTV ya China vilionesha
na kuripoti vituo vikiwa vitupu.
Hata televisheni ya watawala ya ZBC ilikuwa
ikipata kigugumizi kuonesha hali ilivyokuwa katika vile vilivyoitwa vituo vya
kupigia kura hadi kuamua kukatisha matangazo ya moja kwa moja.
Magazeti ya
Tanzania na ya nje ya nchi yaliripoti na kuchapisha picha zilizoonesha kususiwa
kwa uchafuzi huo ulioitishwa na watawala wakidhani wanajihalalishia haramu yao.
Mitandao ya
kijamii nayo ilijaa maelezo na vielelezo kutoka watu na taasisi za kimataifa
zinazoheshimika vikionesha hali halisi ilivyokuwa na ujasiri wa Wazanzibari wa
kuususia uchafuzi huo.
Na hatimaye
nchi 16 zikatoa taarifa yao tarehe 21 Machi, 2016 wakieleza kwamba uchaguzi huo
haukuwa wa kuheshimika kwa sababu haukuwa shirikishi na wala haukuwakilisha
matakwa ya wapiga kura wa Zanzibar.
Nitumie
fursa hii kwa mara nyengine tena kuwapongeza wananchi wote wa Zanzibar kwa
ujasiri, uzalendo na ari kubwa walioionesha kwa kuitikia kwa kiasi kikubwa wito
wa chama chao cha CUF wa kuwataka wasishiriki katika uhuni na ubakaji wa
demokrasia uliopewa jina la uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi, 2016, na
hivyo kuudhihirishia ulimwengu kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakina ridhaa
ya wananchi wa Zanzibar.
Naungana na
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF kuwapongeza waliokuwa wagombea wenzangu
wa CUF kwa nafasi za Uwakilishi na Udiwani kwa kusimama na wananchi wa Zanzibar
na kutoshiriki katika uchaguzi huo haramu na batili wa marudio, jambo ambalo
limethibitisha kwamba hawapo kwa ajili ya kutaka nafasi na vyeo binafsi bali
wanachotaka ni kuleta mabadiliko ya kweli kwa maslahi ya watu wote wa Zanzibar.
Pongezi
zangu za dhati kabisa zinakwenda kwa wagombea Urais, Uwakilishi na Udiwani wa
vyama vyengine vya upinzani ambavyo ni NRA, DEMOKRASIA MAKINI, SAU, UMD, JAHAZI
ASILIA, CHAUMMA, UPDP, DP, na ACT-WAZALENDO, na vile vinavyoshirikiana kupitia
UKAWA ambavyo ni CHADEMA, NCCR na NLD kwa kuungana pamoja na Wazanzibari kutetea
demokrasia yao.
CCM WANAPENDA NAMBA LAKINI HAWAJUI
HESABU
Jambo moja
ambalo CCM wamejifedhehesha wenyewe ni lile la kutangaza kile walichokiita
matokeo ya uchafuzi wao bila ya kuzingatia kwamba takwimu zina sifa moja, huwa
hazisemi uongo.
Vijana wana
msemo wao siku hizi; wanasema CCM wanapenda namba lakini hawajui hesabu.
Matokeo ya tarehe 20 Machi, 2016 waliyoyatangaza ni kwamba eti jumla ya watu
waliopiga kura walikuwa 341,865 na kwamba Dk. Ali Mohamed Shein eti alipata
kura 299,982 sawa na asilimia 91.4.
Takwimu za
uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 zilionesha kwamba jumla ya wananchi
waliojitokeza kupiga kura walikuwa ni 402,354 na Dk. Ali Mohamed Shein alipata
kura 182,011 sawa na asilimia 46.28.
Wakati huo
huo kwa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia, wapiga kura kwa
upande wa Zanzibar walikuwa 417,882 ambapo mgombea wa CCM, Dk. John Pombe
Magufuli alipata kura 194,317 sawa na asilimia 46.5.
Kwa hivyo,
kwa kutumia takwimu hizi, mtu anapochukua takwimu hizi na kulinganisha wapiga
kura 402,354 waliojitokeza tarehe 25 Oktoba, 2015 na wale wanaodai eti
walijitokeza tarehe 20 Machi kwamba ni 341,865 watawala wa CCM walichotaka
kutuaminisha ni kwamba tofauti ya waliokuwa hawakujitokeza kupiga kura ilikuwa
ni 60,489 tu.
Suala la kujiuliza ni kwamba iwapo hilo ni kweli kwa nini vituo
vionekane vitupu kabisa tarehe 20 Machi, 2016?
Lakini kwa
upande mwengine, mtu anapokosa hata tahayuri na kudai Dk. Ali Mohamed Shein
amepata kura 299,982 anachotaka kutwambia ni kwamba ndani ya miezi mitano ya
idhilali na mateso aliyowapatisha Wazanzibari ameweza kuongeza kura 117,971.
Kufedheheka
kwa CCM kunakuja zaidi kwamba walisahau kwamba waliyakubali matokeo ya uchaguzi
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa tarehe 25 Oktoba 2015 kwa upande wa Zanzibar
ambapo kama tulivyokwisha onesha waliopiga kura walikuwa wengi zaidi wakiwa ni
417,882 (na hilo ungetegemea lingeinufaisha CCM) na bado mgombea wa CCM akapata
kura 194,317 sawa na asilimia 46.5.
Kwa kutumia idadi waliyotangaza ya kura
299,982 walizompa Dk. Shein wanataka kutwambia kwamba yeye amepata kura 105,665
zaidi kuliko Dr. Magufuli kwa Zanzibar.
Kama takwimu
zao zingekuwa sahihi ina maana pia wapiga kura waliomuunga mkono mgombea wa CUF
ambao hawakwenda kupiga kura ni 60,489 tu (sawa na asilimia 15 tu).
Hivi nani
utamdanganya kwamba Maalim Seif Sharif Hamad anaungwa mkono na asilimia 15 tu
ya wapiga kura wa Zanzibar? Nani utamdanganya kwamba ndani ya miezi mitano, CCM
imeongeza kura 105,665 zaidi ya alizopata mgombea wake Dk. Magufuli kwa upande
wa Zanzibar?
Kutokana na
ubabe na kiburi cha utawala walicho nacho CCM, wameishia kujifedhehesha kwa
takwimu zao za kupika wenyewe. Ndiyo vijana wakasema, CCM wanapenda namba
lakini hawajui hesabu.
NINI MWELEKEO WA CUF NA WAZANZIBARI
BAADA YA UBAKAJI HUU WA DEMOKRASIA?
Wazanzibari
walio wengi wamekuwa wakituuliza nini mwelekeo wa CUF baada ya ubakaji huu wa
demokrasia? Wanatuuliza viongozi wao na hasa mimi tunatokaje katika hali hii
ambayo imedumu miaka nenda miaka rudi kila pale Zanzibar inapofanya uchaguzi?
Kabla
sijalieleza hilo, nataka niweke wazi leo kwamba tulipofanya uamuzi wa kuususia
uchaguzi haramu na batili wa tarehe 20 Machi, 2016 tuliamua kusimama juu ya
uamuzi unaoheshimu misingi ya kikatiba ambayo watu wa Zanzibar tumeamua ndiyo
inapaswa iongoze na iendeshe nchi yetu.
Tulijua kwamba uamuzi huo utakuwa na
athari kwa CUF na kwa Zanzibar lakini tulijua na tuliamini pia kwamba athari
hiyo haiwezi kuwa kubwa zaidi kuliko gharama ya kuikanyaga Katiba na Sheria za
nchi yetu na gharama za kupiga teke demokrasia, haki za binadamu na utawala wa
sheria.
Tulipima na
tukatafakari kwa kina na kuona ni kheri kumeza machungu ya athari binafsi kwetu
lakini tusimame kidete na kifua mbele katika kutetea maamuzi ya watu wa
Zanzibar waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015, na pia kulinda misingi ya Katiba
na Sheria za nchi yetu na misingi ya demokrasia na haki za watu. Tuliona hayo
ni kheri kwa huko twendako badala ya kushiriki katika haramu ya ubakaji wa
demokrasia na matumizi ya nguvu za kijeshi kulazimisha watawala wasio na ridhaa
ya watu.
Tulifanya
maamuzi yale pia kwa lengo la kuepusha shari katika nchi yetu. Leo Wazanzibari
na dunia nzima ni mashahidi kwamba uamuzi ule ulikuwa sahihi na wa busara.
Maana mateso na vitisho walivyokumbana navyo Wazanzibari wakati tumewaachia
uchaguzi ule watawala waovu peke yao vilikuwa vya kiasi kile kilichoshuhudiwa.
Je,
tungeliamua kushiriki na kusimama kulinda na kutetea ushindi wetu hali
ingekuwaje? Bila shaka nchi ingetumbukia katika machafuko ambayo watawala waovu
walikuwa tayari yatokee kuliko kuridhia maamuzi halali ya wananchi wa Zanzibar.
Maamuzi yale
yamethibitika pia kwamba ni sahihi kwa jinsi watu wa Zanzibar walivyoudharau na
kuupuuza uchaguzi haramu na batili wa tarehe 20 Machi, 2016. Watawala waovu wa
CCM waliwadharau watu wa Zanzibar na watu wa Zanzibar wakaamua kuwadharau wao
tarehe 20 Machi 2016.
Kwa upande
mwengine, uamuzi tuliouchukua na kuusimamia pia ni uamuzi uliosimama juu ya
misingi ya heshima na misingi ya utu wa watu, ambayo yalikuwa ndiyo malengo
sahihi ya Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Hayati Mzee Abeid
Amani Karume, malengo sahihi ya Chama cha Afro Shirazi na malengo sahihi ya
Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Kwa hakika,
uamuzi wa kuupuuza na kuudharau uchafuzi wa tarehe 20 Machi, 2016 ni ushindi
mwengine wa Zanzibar katika historia yake ya kisiasa.
Nimalizie
sasa kwa kujibu hoja ya ni upi mwelekeo wa CUF na wa Wazanzibari baada ya
ubakaji huu wa wazi wa demokrasia na haki za watu wa Zanzibar?
Kwanza,
nirudie na kusisitiza msimamo wetu kwamba hatukubaliani na ubakaji wa
demokrasia na haki za watu wa Zanzibar uliofanywa na watawala waovu wakisaidiwa
na vyombo vya dola. Kwa msingi huo, Wazanzibari wataendelea kuipinga serikali
isiyo na ridhaa ya watu kwa kutumia njia za amani, za kidemokrsia na
zinazoendana na misingi ya Katiba na Sheria za nchi yetu.
Jana
kumetangazwa kile kilichoitwa ni Baraza la Mawaziri. Msimamo wetu uko pale
pale. Kama tusivyomtambua aliyelitangaza Baraza hilo, vivyo hivyo hatulitambui
Baraza lake la Mawaziri.
Kwa hakika,
kwa sababu msingi wa watawala waliojinyakulia madaraka ni kupitia uvunjwaji wa
Katiba, kila kinachofuata kimekuwa kikiendeleza uvunjwaji wa Katiba. Katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984 kupitia Marekebisho ya 10 ya mwaka 2010, Ibara ya 9 (1)
inalazimisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na muundo wa Serikali ya
Umoja wa Kitaifa.
Ibara za 39,
39A na 42 za Katiba zimeeleza namna Serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa
itakavyoundwa.
Masharti yote hayo yanaendelea kuvunjwa na mtawala aliyeamua
kuyapiga teke maamuzi ya Wazanzibari na kujiweka madarakani kwa nguvu. Kwa
hivyo, Serikali yake haiwezi kuwa Serikali inayokwenda na Katiba. Kwa ufupi, si
Serikali halali kwa mujibu wa Katiba.
Baraza Kuu
la Uongozi la Taifa la CUF katika kikao chake cha tarehe 2 – 3 Aprili, 2016
lilipitisha maazimio yafuatayo miongoni mwa maazimio yake:
“Azimio Nam. 9:
Haliyatambui
matokeo ya uchaguzi huo haramu na batili, na kwa msingi huo halimtambui Dk. Ali
Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar, haliwatambui waliotangazwa kuwa
Wawakilishi na wala haliwatambui waliotangazwa kuwa Madiwani.
Baraza Kuu
linaungana na wananchi wa Zanzibar waliokataa kuwapa uhalali watu hao na kwa
hivyo halitoitambua Serikali, Manispaa na Halmashauri za Wilaya zitakazoundwa
na watu hao.
CUF
haitoshirikiana na Serikali itakayoundwa kwa sababu ni kinyume na Katiba ya
Zanzibar, kinyume na Sheria ya Uchaguzi na haikutokana na ridhaa ya watu.
Kwa
vyovyote vile, Serikali itakayoundwa haitakidhi matakwa ya Katiba ya Zanzibar
na hivyo CUF haitoshiriki kwenye uvunjaji wa Katiba ambayo inaeleza kwa uwazi
kabisa namna ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
“Azimio Nam. 10:
Linawataka
wananchi wote wa Zanzibar kutumia njia za amani, za kikatiba na kisheria ambazo
zimewahi kutumika katika nchi nyingine duniani kuwakataa watawala waovu na
wasio na ridhaa ya watu waliojiweka madarakani kwa kutumia nguvu na ubakaji wa
demokrasia kwa kutoipa ushirikiano Serikali itakayoundwa na watawala hao.”
Baada ya
maazimio hayo ya Baraza Kuu, kinachofuata sasa ni utekelezaji wake. Hivi sasa
tunapanga mikakati madhubuti ya utekelezaji wa maazimio hayo kwa kutumia njia
za amani, za kidemokrasia na za kikatiba ili kutufikisha kwenye malengo yetu ya
kuona maamuzi ya watu wa Zanzibar yanaheshimiwa.
Nina hakika
kabisa kuwa mikakati tunayoipanga itazaa hatua ambazo zitaibana Serikali haramu
na hatimaye itasalimu amri kwa wananchi wa Zanzibar ambayo kwa mujibu wa Katiba
ya Zanzibar ndiyo wenye mamlaka ya kuiweka madarakani Serikali wanayoitaka.
Katika dunia ya leo, hatuwezi kuongozwa na watawala ambao hawakupewa mamlaka na
watu wenyewe.
Pili,
naipongeza na kuishukuru jumuiya ya kimataifa na washirika wa maendeleo kwa
msimamo waliochukua wa kukataa kubariki ubakaji huo wa demokrasia na haki za
watu wa Zanzibar na kukataa kushiriki katika uapishwaji wa mtu asiye na ridhaa
ya wapiga kura wa Zanzibar.
Napongeza hatua ambazo wameanza kuzichukua dhidi ya
Serikali za CCM ambazo ndizo zilizosimamia ubakaji huo wa demokrasia na haki za
watu.
Natoa wito kwao kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya watawala hawa waovu
zikiwemo kuwawekea vikwazo vya kusafiri, kufuatilia akaunti zao za fedha nje ya
nchi na hatua za kuchunguza matendo yao ya uhalifu dhidi ya binadamu.
Wananchi
waliodhulumiwa haki zao wanaziunga mkono hatua hizo wakiamini kwamba CCM ni
lazima iwajibishwe kwa matendo yake maovu dhidi yao.
Nitumie
fursa hii kwa mara nyengine tena kuwataka wananchi wa Zanzibar kudumisha amani
ya nchi yetu na umoja wa watu wetu. Nikiwa kiongozi wao ninayewapenda na ambaye
nimejitolea kuwatumikia katika umri wangu wote siwezi kuwaongoza kuelekea
kwenye fujo na ghasia au vitendo vitakavyopelekea kuiharibu nchi yetu na
kuathiri watu wetu. Nina imani kabisa kwamba njia tunayoifuata ni njia ya haki;
na haki siku zote itashinda.
Mwaka 2009,
mimi na mwenzangu, Dk. Amani Abeid Karume, tuliwaongoza Wazanzibari katika
Maridhiano yaliyoashiria mwanzo wa ujenzi wa mahusiano mapya baina ya watu wema
wa Zanzibar kwa kuzika siasa za ubaguzi, utengano, chuki, hasama na fujo na
badala yake kusimamisha siasa za maelewano, umoja, upendo, mshikamano na udugu
katika jamii yetu.
Tulitegemea
kuanzia pale tungeendelea mbele kwa kuchukua hatua za kuyaimarisha maridhiano
yetu na kuyazamisha zaidi kwenye nyoyo za Wazanzibari. Binafsi nasikitishwa na
kuhuzunishwa sana kuona watawala waovu wasiowatakia mema watu wa nchi hii
wameturudisha tulikotoka kwa maslahi yao binafsi.
Natoa wito
kwa Wazanzibari wenzangu kuwa tukatae kurudishwa kwenye siasa zile za ubaguzi,
utengano, chuki, hasama na fujo na kila mmoja afanye lile liliomo katika uwezo
wake kuendeleza maelewano, umoja, upendo, mshikamano na udugu katika jamii
yetu.
Wazanzibari
tumeamua kuisimamisha tena Zanzibar yetu na Zanzibar itasimama tena Inshallah.
Hilo sina wasiwasi nalo kama kiongozi wa Wazanzibari waliyenipa ridhaa yao.
HATIMAYE
TUTASHINDA.
WANANCHI
JASIRI NA SHUPAVU WA ZANZIBAR WATASHINDA.
Ahsanteni
sana.
|
No comments:
Post a Comment