Waziri Mkuu wa Tanzania,Mhe Kassim Majaliwa ameongoza maelfu ya
waumini na wakazi wa mkoa wa Dodoma katika mazishi ya Mhashamu Askofu Mstaafu, Mathias Isuja wa Kanisa
Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma.
Amesema kifo hicho ni pigo kwa watu
wote na si kwa kanisa pekee kwa sababu walimtegemea kulisaidia Taifa kiroho na
kimaendeleo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo Jana
(Jumatano, Aprili 20, 2016) wakati akizungumza na waumini na wakazi wa mkoa huo
na mikoa jirani kwenye ibada ya mazishi iliyofanyika kwenye Kanisa la Kiaskofu
la Mtume Paulo wa Msalaba mjini Dodoma.
Askofu Isuja ambaye alizaliwa Agosti
14, 1929 alikuwa Askofu wa kwanza mzalendo katika Jimbo la Kanisa Katoliki la
Dodoma. Alistaafu kazi ya uaskofu mwaka 2004 kwa mujibu wa sheria ya kanisa.
Alifariki Aprili 13, mwaka huu.
Waziri Mkuu amesema Serikali
itaendelea kumuenzi Askofu Isuja kwa kazi nzuri aliyoifanya wakati wa uhai wake
na kuyaendeleza yote aliyoyaanzisha kwenye maeneo aliyowahi kuyatumikia.
“Tumepoteza
mtu makini, sisi ni mashahidi wa mchango mkubwa wa marehemu siyo tu katika
kutoa huduma za kiroho, bali pia huduma za kijamii zilizolenga kuleta maendeleo
kwa wananchi katika jimbo hili la Dodoma na katika taifa kwa ujumla,”
amesema.
Mapema, akitoa mahubiri wakati wa
ibada hiyo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Mhashamu Judathadeus Ruwa’ichi
alisema waumini wa kanisa hilo wa mkoa wa Dodoma na Tanzania nzima wanapaswa
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha marefu aliyomjalia Askofu Isuja.
“Tunapaswa
kumshukuru kwa maisha marefu ambayo Mungu alimzawadia baba yetu Isuja. Katika
Zaburi ya 90 tunasoma kuwa mwanadamu ana miaka ya matazamio ambayo ni 70,
lakini yeye alipewa miaka ya matazamio 70 na akazawadiwa nyongeza ya miaka 10
na kisha miaka mingine sita na nusu,” alisema.
Alisema zawadi nyigine ambayo Mungu
aliwapatia waumini hao ni ya imani ambayo Baba Askofu Isuja aliipokea,
aliifundisha na aliishi na akawataka waendelee kumshukuru Mungu kwa hilo.
“Miaka
56 ya utumishi wake kama padre na askofu ni zawadi kwa Dodoma na Tanzania na
siyo kwake yeye binafsi,” alisema.
Ibada hiyo ya mazishi ilihudhuriwa na
Maaskofu Wakuu na Maaskofu wa kawaida 28 kutoka majimbo ya Dodoma, Mwanza,
Mbeya, Njombe, Mpanda, Iringa, Songea, Tabora, Morogoro na Mahenge.
Mengine ni Musoma, Rulenge, Mbinga,
Moshi, Same, Kahama, Sumbawanga, Shinyanga, Mtwara na Lindi. Majimbo mengine ni
Bukoba, Tanga, Singida, Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha, Kondoa na Kayanga.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980.
DODOMA.
JUMATANO, APRILI 20, 2016.
|
No comments:
Post a Comment