|
Wakatai Rais John Magufuli akisisitiza kuwa utumbuaji
majipu utaendelea kufanyika hadharani bila kificho, pigo jingine kwa
waliotumbuliwa na wanaosubiri kutumbuliwa, limetangazwa.
Akisoma Mwelekeo wa Kazi za Serikali Bungeni
Jana April 22, 2016, Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa, mbali na kusisitiza kuendelea kushughulikia watendaji Wazembe, Wabadhirifu na Wavivu, alitangaza kuwa Divisheni ya
Mahakama ya Rushwa na Ufisadi imeanzishwa katika Mahakama Kuu na itaanza kazi
zake Julai mwaka huu,2016.
Hatua hiyo ni pigo kwa watuhumiwa wa
ufisadi ambao tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, wamekuwa
wakichukuliwa hatua hadharani ya kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi dhidi ya
tuhuma zao, kiasi cha baadhi ya wanasiasa kushindwa kuvumilia na kujitokeza
kulalamika.
Miongoni mwa wanasiasa waliojitokeza
kulalamikia hatua ya watuhumiwa hao kuchukuliwa hatua ni Mwenyekiti wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman
Mbowe na aliyekuwa mgombea Urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu
uliopita, Edward Lowassa.
Mahakama ya Rushwa.
Mahakama hiyo ni moja ya ahadi
zilizonadiwa na Dk Magufuli katika
Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015-2020 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka
jana, akisema katika Hotuba ya Ufunguzi wa Bunge na kuirejea wakati wa uzinduzi
wa Mwaka wa Mahakama na Siku ya Sheria Duniani.
Katika maandalizi ya uundwaji wake,
Jaji Kiongozi, Shaban Lila, aliwahi kusema kwamba mahakama iliitisha wadau
mbalimbali wa haki jinai, kuangalia namna ya kuanzisha mahakama hiyo, ambapo
mjadala ulikuwa ni kuanzisha mahakama huru au kitengo maalumu ndani ya Mahakama
Kuu, kitakachopewa kipaumbele cha kushughulikia mafisadi.
Akitangaza kukamilika kwa mchakato
huo jana, Waziri Mkuu Majaliwa alisema: “Napenda kuliarifu Bunge kwamba Serikali imeanzisha
Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi katika Mahakama Kuu itakayoanza
kufanya kazi Julai, 2016.”
Uharaka wa Kesi.
Mbali na kuanza kufanya kazi kwa
mahakama hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa pia alisema kuwa Serikali itaimarisha Ofisi
ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
ili ziharakishe utoaji wa haki.
Uimarishwaji wa ofisi hizo pia
unatokana na agizo la Rais Magufuli
alilotoa siku hiyo ya uzinduzi wa Mwaka wa Mahakama na Siku ya Sheria Duniani,
alipotaka kesi za uhujumu uchumi na ufisadi ziendeshwe kwa kasi, ili jitihada
za Serikali za kupambana na matatizo hayo, zizae matunda.
Katika hotuba hiyo ya Siku ya Sheria
Duniani, Rais Magufuli alielezea
kushangazwa na kitendo cha ofisi ya DPP, kuchelewa kuwapeleka mahakamani
watuhumiwa waliokamatwa na ushahidi.
Alitoa mfano wa watuhumiwa
waliokamatwa na meno ya tembo, ambapo alitaja Mahakama ya Kisutu kuwa ilikuwa
na kesi 26 za watu walioshikwa wakiwa na nyara za Serikali, lakini kesi hizo
zikachukua zaidi ya miaka mitano bila kufanyiwa uamuzi.
Dk Magufuli alisema maelezo
yaliyokuwa yakitolewa ni kwamba upelelezi bado unaendelea wakati wahusika wa
kufanya upelelezi huo wapo na washitakiwa walishikwa wakiwa na vielelezo.
Alisema inawezekana hakimu akawa
anataka kutoa hukumu, lakini DPP na Polisi wanaofanya uchunguzi, wanasema
upelelezi unaendelea, jambo linaloonesha tatizo lililopo la ucheleweshaji kesi.
Utumbuaji Kuendelea.
Katika hotuba hiyo ya Majaliwa,
iliyokwenda sambamba na makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka
wa fedha 2016/17, alisema Serikali itaendelea kuwawajibisha wale wote ambao hawataendana
na Falsafa na Mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano, lakini akasisitiza kwamba
serikali itachukua hatua kwa kuzingatia na kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu
za Utumishi wa Umma.
“Niwahakikishie Watanzania kwamba hakuna mtumishi au
mwananchi atakayeonewa au kunyanyaswa katika hili. Hivyo wale wote ambao wako
safi waendelee kutimiza wajibu wao bila woga. Kazi zifanyike kwa weledi na kwa
kasi bila urasimu,” alisema.
Majaliwa alisema katika kutekeleza
falsafa ya Hapa Kazi Tu na ili Tanzania ifikie uchumi wa kipato cha kati
ifikapo mwaka 2025 ni sharti kila mtu afanye kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu
wa hali ya juu.
“Ili yawepo mapinduzi ya kweli ya kuelekea kwenye uchumi
wa Kati tunaodhamiria ni lazima tuimarishe uwajibikaji na maadili kwa viongozi,
watendaji na kwa kila Mtanzania. Sote tumeshuhudia hatua
zinazochukuliwa na serikali dhidi ya watumishi wasio waadilifu, wanaotumia
fedha za umma na madaraka yao vibaya.
“Ndio maana tumeanza kwa nguvu kuimarisha nidhamu,
uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha za umma ili zielekezwe kwenye shughuli
zenye manufaa kwa Watanzania walio wengi na si vinginevyo,” alisema
Waziri Mkuu Majaliwa.
Akizungumzia utekelezaji wa Sera ya
Utoaji Elimu Bure kuanzia Darasa la Kwanza hadi Kidato cha Nne, Waziri Mkuu Majaliwa alisema ipo changamoto ya
upungufu mkubwa wa madawati baada ya kuanza kuandikisha watoto shule bila
malipo.
Kutokana na hilo, aliwaagiza
Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini waliokamata mbao kutokana na makosa
mbalimbali kutozipiga mnada mbao hizo na badala yake watumie mbao hizo
kutengeneza madawati kuanzia jana na pia halmashauri kutumia rasilimali zake
kutengeneza madawati kwa kila shule.
|
No comments:
Post a Comment