![]() |
|
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 19 Aprili,
2016 amefungua rasmi Daraja la Kigamboni linalounganisha usafiri wa barabara
kati Kigamboni na Kurasini Jiji la Dar es salaam na amependekeza Daraja hilo
liitwe Daraja la Nyerere (Nyerere Bridge).
Sherehe za
ufunguzi wa daraja hilo kubwa na la kipekee kwa Afrika Mashariki na Kati
zimefanyika kando ya daraja hilo upande wa Kigamboni na kuhudhuriwa na viongozi
na wageni mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Balozi wa China
nchini Tanzania Dkt. Lu Youqing, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na
Uchukuzi Mhandisi Edwin Ngonyani, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) Mheshimiwa Antony Mavunde, Wabunge na Mameya wa Jiji na
Dar es salaam.
|

![]() |
|
Ujenzi wa
daraja hilo umehusisha nguzo mbili za pembezoni na mihimili miwili inayoshikilia
nyaya 36, na daraja zima lina urefu wa meta 680, upana wa mita 32, njia sita za
magari, njia mbili za watembea kwa miguu na barabara unganishi zenye urefu wa
kilometa 2.5.
Daraja hilo
limejengwa kwa fedha za ndani na kugharimu jumla ya shilingi Bilioni 254.12
ambapo kati ya fedha hizo asilimia 60 zimetolewa na Shirika la Hifadhi ya Jamii
(NSSF), na asilimia 40 zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
|

![]() |
|
Kujengwa kwa
Daraja hili kutaondoa kero ya msongamano wa magari na usafiri kwa wakazi wa
Kigamboni na wakazi wa katikati ya Jiji la Dar es salaam ambao walilazimika
kutumia kivuko (Ferry) ili kukatiza eneo la mkondo wa bahari ya Hindi ama
kutumia barabara ya kuzunguka kupitia Kongowe lenye urefu wa kilometa 52.
Daraja hilo
limefanyiwa majaribio kwa kutumia Malori 44 yenye uzito wa tani 30 na
limethibitika kuwa na uwezo wa kubeba jumla ya tani 1,320 na hivyo linatarajiwa
kusaidia usafirishaji wa mizigo ya kutoka na kuingia katika bandari ya Dar es
salaam.
Akizungumza katika
sherehe hizo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
ameagiza vyombo husika vianze mchakato wa daraja hilo kupewa jina la
"Daraja la Nyerere" (Nyerere Bridge) ikiwa ni kuuenzi mchango mkubwa
wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefanya kazi kubwa
ya kuijenga Tanzania.
|
![]() |
Aidha,Rais
Magufuli amewapongeza wadau wote waliohusika kufanikisha ujenzi wa Daraja hilo
likiwemo Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na
Uchukuzi na wakandalasi kutoka China, na ametaka watanzania wajivunie daraja
hilo kubwa na lililojenga heshima kubwa kwa nchi.
Pia Dkt.
John Pombe Magufuli ametoa wito kwa Vyombo vya Habari vya Tanzania kuitangaza
vyema Tanzania na kuwa na uzalendo wa kweli kwa nchi yao badala ya kubeza kazi
nzuri zinazofanywa ndani ya nchi kwa manufaa ya watanzania.
|









No comments:
Post a Comment