Rais John Magufuli juzi,March 13,2016 alitangaza mabadiliko makubwa kwenye nafasi za
ukuu wa miko akiwaacha makada 12, ambao wachambuzi wameeleza kuwa wametemwa
kutokana na sababu kuu nne.
Hata hivyo,
wengine wamesema sababu za kutemwa au kuteuliwa bado zinabaki kuwa hisia kwa
kuwa uteuzi wa wanasiasa hauna vigezo maalumu.
Kwa mujibu
wa wachambuzi hao waliohojiwa na Mwananchi kuhusu uteuzi huo, sababu hizo ni
utendaji, uzoefu, rika na umakini, ambazo hazitofautiana na vigezo ambavyo Rais
Magufuli alivitaja kuwa angevitumia kuteua makada hao wakati alipoongea na
wazee wa Dar es Salaam hivi karibuni.
Viashiria
hivyo ni jinsi viongozi hao walivyokabiliana na ugonjwa wa kipindupindu,
upungufu wa chakula, migogoro ya ardhi na upungufu wa madawati shuleni.
Katika
uteuzi wake juzi, Rais Magufuli aliteua wakuu wa mikoa wapya 13 na kuwaondoa 12
waliokuwa kwenye mikoa ya Tabora, Geita, Kigoma, Tanga, Singida, Mbeya,
Morogoro, Katavi, Mara, Simiyu na Shinyanga.
Akizungumzia
uteuzi huo, Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema anaamini
vigezo alivyobainisha Rais Magufuli ndiyo vimetumika kuwachambua.
“Kwa mfano,
migogoro ile ya Morogoro bila shaka itakuwa imewaathiria baadhi ya wakuu wa
mikoa ukiwamo Morogoro,” alisema.
Kwa upande
wake, Profesa Gaudence Mpangalla wa Chuo Kikuu cha Ruaha alisema kabla ya
kuondolewa kwa wakuu hao wa mikoa, Rais Magufuli alitumia muda mrefu
kuwachunguza ili kujiridhisha kabla ya kupata watu wanaoweza kwenda na kasi
yake.
“Nadhani kwa
sasa ameona nani anamfaa na nani ambaye hawezi kuendelea naye. Ingawa kutambua
sababu za kuwaondoa inakuwa vigumu, hata aliowateua lazima waendane naye,
majukumu yanajulikana ila zaidi ni kuwa wabunifu na wachapakazi,” alisema.
Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika Idara ya Sayansi ya Siasa na utawala
bora, Richard Mbunda alifafanua sababu hizo nne alizosema zilichagiza kiongozi
huyo kuwaondoa 12.
Mbunda
alitaja kigezo cha kwanza kuwa ni rekodi ya utendaji wa kiongozi mmoja huku
akimtolea mfano Paul Makonda aliyepandishwa kutoka ukuu wa wilaya kuwa mkuu wa
mkoa baada ya muda mfupi kuwa amebebwa na kigezo cha ubunifu.
Pili, Mbunda
alitaja kigezo kingine kuwa ni uzoefu wa mtendaji uliosaidia kuchochea
maendeleo katika maeneo yao.
“Kwa mfano,
kuna viongozi kama Joel Bendera na Saidi Meck Sadiki ni wazee wenye uzoefu,”
alisema Mbunda.
Tatu, Mbunda
alitaja kigezo cha kuchanganya rika kwa viongozi hao huku akiwatolea mfano
Makonda (Dar es Salaam) na Martin Shigela (Tanga).
Hata hivyo,
mhadhiri huyo alisema: “Kilichoonekana katika uteuzi huo, Rais hakuzingatia
suala la uwiano wa kijinsia, lakini si hoja kama ameangalia watu wa kumsaidia
zaidi katika kasi yake.”
Mbunda
alitaja sababu nyingine aliyozingatia kuwa ni umakini, akisema mazingira hayo
yameonekana katika uteuzi wa wakuu wa mikoa wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) katika mikoa ya mipakani.
“Kwa
kuangalia asili ya maeneo hayo, ilistahili kabisa kupeleka watu kama hao, kwa
sababu changamoto za maeneo hayo zinahusu masuala ya kiusalama zaidi,” alisema
mhadhiri huyo.
Vigezo vya
Magufuli.
Akizungumza
na wazee wa Dar es Salaam takribani wiki tatu zilizopita, Rais Magufuli alitaja
vigezo ambavyo wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi watendaji wa halmashauri
wanatakiwa kuvitumia kujipima.
Vigezo hivyo
ni kuimarisha mapambano dhidi ya kipindupindu, kuondoa kero ya madawati,
migogoro ya ardhi, upungufu wa chakula na matumizi sahihi ya fedha za umma.
Hata hivyo,
Dk Bashiru Ali wa Idara ya Sayansi ya Jamii ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) alisema hakuna vigezo vinavyotambuliwa rasmi kutumika kwenye uteuzi wa
viongozi kisiasa au kuwaondoa wa zamani.
Alisema
kuondolewa kwa mkuu wa mkoa wa Morogoro hakuwezi kuwa ushahidi wa moja kwa moja
kuwa kunatokana na migogoro ya wakulima na wafugaji.
“Migogoro
iko. Hata Manyara ipo, si Morogoro pekee. Kwa hivyo huwezi kutumia kigezo hicho
kama sababu iliyomtoa moja kwa moja mtu,” alisema.
Migogoro ya
wakulima na wafugaji pia iko mkoani Dodoma.
“Kuhusu
uteuzi wa Rais, tunaweza kuona viashiria kadhaa vya ukada, uwezo wa mtu, uzoefu
au fadhila lakini itabakia kuwa hisia tu, kwa mfano labda mpakani wamepelekwa
wanajeshi wastaafu kwa sababu kumekuwa na changamoto ya biashara za magendo,
dawa za kulevya. Lakini ulinzi ni tatizo maeneo mengi, kwa hivyo inabakia kuwa
hisia tu,” alisema.
:- By Kelvin
Matandiko, Mwananchi.
|
No comments:
Post a Comment