AFISA MIFUGO
wa kata ya Kakunyu, wilayani Misenyi mkoani Kagera, Bw.Eric Kagoro amenusurika
kutumbuliwa jipu kwenye mkutano wa hadhara kuhusiana na sakata la kuruhusu
ng’ombe 291 waje kulishwa kwenye ranchi ya mifugo ya Misenyi.
Tukio hilo
limetokea Jana mchana (Jumatatu, Machi 14, 2016) wakati Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa akizungumza na mamia ya wananchi waishio jirani na ranchi hiyo katika
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye makao makuu ya ranchi hiyo.
Waziri Mkuu
alimuibua Bw. Kagoro katikati ya mkutano kwa kumtaja jina na tuhuma zinazomhusu
kuhusu mifugo iliyokamatwa. “Afisa Mifugo wa kata yupo hapa?."
Aliuliza Waziri Mkuu. "Wewe ndiyo Eric?” Alipojibu ndiyo
akaulizwa tena:”Nimekujuaje?”
“Nimeambiwa
wale ng’ombe waliokamatwa ni wa rafiki yako na wewe ndiye ulitoa kibali waje
kulishwa kwenye ranchi hii. Siyo kazi yako kuruhusu mifugo ya nje ije kulishwa
hapa kwenye ranchi. Kuanzia sasa ni marufuku kwa mtu yeyote kuingiza mifugo
kwenye ranchi ili ipate malisho “
“Leo
Nimekusamehe .Kazi yako ni kuhakikisha mifugo ya kwenye kata hii iko salama.
Kazi yako ni kuwasaidia wafugaji wa kata hii wafuge vizuri na uhakikishe mifugo
yao inakuwa na tija.” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.
Kwa upande
mwingine, Waziri Mkuu alitumia fursa
hiyo kuwaasa watendaji wa kata na vijiji kutotumia nafasi zao kuleta migogoro
baina ya watu wa nje na wananchi wanaowaongoza. “Mwenyekiti wa kijiji huna
ruhusa ya kugawa kitalu cha ranchi au kuruhusu mtu yeyote akalime ndani ya ranchi”,
alisema.
Aliwataka
pia maafisa uhamiaji wawe makini na vyeti vya kuandikisha uraia wanavyovitoa
kwa wananchi wanaoishi mipakani kwani imekuwa ni mianya ya kuleta migogoro ya
ardhi. “Watu wa uhamiaji kuweni makini na CN mnazotoa (CN=Certificate of Naturalisation).
Wote wanaoomba CN wanataka blocks tu”
Alitoa agizo
kuwa watafutwe watu wote walioingia nchini kwa mgongo wa CN, wakamatwe na
kurejeshwa makwao. “Kuna watu wamekuja hapa nchini wakaomba CN lakini wakikaa
wanaleta wenzao waje kununua ardhi kwa kutumia mgongo wa CN zao.”
Alisema kuna
watu wametoka wilaya ya Karagwe ambako pia kuna tatizo kama la Misenyi na
kuwataka wahusika wajiandae kuchujwa na kuchukuliwa ardhi zao kama watakuwa
hawajaziendeleza ili wapewe Watanzania wenye uhitaji wa kulima na kufuga.
|
No comments:
Post a Comment