Ni kweli
siku hazigandi kwamba Rais John Magufuli aliyeingia madarakani baada ya
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana 2015, ametimiza siku 100 leo,February 12,2016.
Tangu
alipotoa hotuba yake siku ya kuapishwa na ile ya uzinduzi wa Bunge la 11, Rais
Magufuli amejitahidi kuishi katika
maneno yake kwa kutenda kile anachokisema.
Miongoni mwa
mambo aliyoahidi ni kupambana na rushwa pamoja janga la dawa za kulevya,
akisema dawa za kulevya zimeathiri vijana wengi, hivyo akaahidi kushughulikia
mtandao huo na wakubwa wanaohusika.
Kwa upande wa rushwa, Rais Magufuli aliahidi
kupambana na ufisadi na rushwa na katika kutekeleza hilo, alisema ataunda
mahakama maalumu ya kushughulikia wezi wakubwa yaani mafisadi.
Pia aliahidi kuwashughulikia wafanyakazi
wazembe ili Serikali yake isiendelee kulea watu wanaolipwa mishahara tu wakati
hawafanyi kazi yoyote.
Katika
kubana matumizi ya serikali, aliahidi kudhibiti warsha ambazo hazina umuhimu
katika Serikali wala kuongeza ufanisi kwa wafanyakazi.
Aliahidi pia
kudhibiti safari za nje, ambazo zimekuwa zikigharimu Serikali fedha nyingi
ambazo zingeweza kutumika katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Rais
Magufuli pia alisema Serikali yake itaongeza wigo katika ukusanyaji wa mapato,
ukizingatia kuwa kodi ni kitu muhimu na ni lazima zikusanywe.
Aliahidi
kufufua viwanda viliyobinafsishwa, ambavyo baadhi alidai vimegeuzwa mazizi ya
mbuzi wakati waliopewa kwa madhumuni ya kuviendeleza.
Aliahidi pia
kushughulika na kero zinazolalamikiwa kutendwa na polisi, hospitali, mizani,
Mahakama, maliasili na vilio vya wachimbaji.
Tayari Rais
Magufuli ametenda yale ambayo aliyaahidi kwa Watanzania. Amebana matumizi ya
serikali kwa kudhibiti safari zisizo na tija, matumizi yasiyo ya lazima,
ameshughulikia watumishi wazembe, ameshughulikia mafisadi ndani ya serikali na
kutoa elimu ya bure.
Alivyoanza kazi.
Mara tu
baada ya kuingia ofisini, alimuapisha Mwanasheria Mkuu, George Masaju
aliyemteua muda mfupi tu baada ya kuapishwa.
Katika siku
zake hizo za mwanzo, alitumia mtindo wa kufanya ziara za kushtukiza katika
taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na kukemea viongozi wazembe na
wanaoendekeza ufisadi na rushwa serikalini.
Mtindo wake
huo, ukatumiwa pia na watendaji wengine wa Serikali wakiwamo mawaziri na wakuu
wa mikoa na wengine.
Katika siku
zake hizo za mwanzo, Rais Magufuli pia alifanya mabadiliko makubwa Ikulu kwa
kufuta baadhi ya vitengo, kikiwamo cha lishe na benchi la wageni na kuagiza
wananchi wote wenye matatizo waanzie ngazi za chini.
Atoa Msimamo
wake.
Novemba 7,
mwaka jana akiwa Ikulu, Dar es Salaam, alikutana na watumishi wa Serikali ikiwa
ni pamoja na manaibu katibu wakuu, manaibu wakuu na watendaji wakuu wa
Serikali.
Katika kikao
hicho, aliwataka kujiandaa kufanya kazi kwa ufanisi katika Serikali ya awamu ya
tano chini yake. huku akiwasisitiza juu ya dhamira yake ya kuendeleza kaulimbiu
yake ya “Hapa kazi tu”.
Kikao hicho
pia kiliudhuriwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu
na aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade
ambapo alitoa mwelekeo wa Serikali anayoitaka.
Afuta Safari
za Nje.
Rais
Magufuli alitumia kikao hicho kutangaza kufuta safari zote za nje ya nchi hadi
hapo atakapolitolea suala hilo uamuzi mwingine, na kueleza shughuli zote
zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wa
Tanzania wanaowakilisha nchi.
Alisema
mtumishi atasafiri nje iwapo kutatokea jambo la dharura, na lazima kibali
kitolewe na yeye, Katibu Mkuu Kiongozi au Makamu wa Rais.
Badala yake
aliwataka watendaji hao kufanya zaidi ziara za kwenda vijijini ili kuzijua na
kutatua kero za wananchi.
Hadi sasa,
Rais Magufuli bado hajakwenda safari yoyote ya nje ya nchi zaidi ya kuwatuma
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenda
kumwakilisha kwenye shughuli mbili tofauti.
Safari
zake ndani ya nchi.
Novemba 20,
mwaka jana,2015, Rais Magufuli alisafiri kwa mara ya kwanza nje ya Dar es Salaam
alipokwenda mkoani Dodoma ambako alifungua Bunge la 11.
Katika
mkutano wake, Rais Magufuli alijikuta akisusiwa hotuba yake na wabunge wa
upinzani waliokuwa wakipinga uteuzi wake na kutomtambua Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kama rais halali,
baada ya kufutwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Januari 12,
mwaka huu,2016, Rais Magufuli alisafiri kwa ndege ya kukodi kwenda Zanzibar ambako
alihudhuria maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Januari 21,
mwaka huu alifanya ziara ya kwanza mkoani Arusha, ambako alikwenda pia katika
Chuo cha Maofisa wa Kijeshi (TMA) Monduli kutunuku vyeo askari wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya kuhitimu mafunzo, huku naye akiwa amevalia
sare za jeshi hilo.
Februari 5,
mwaka huu pia Rais Magufuli alisafiri kwa gari kutoka Dar es Salaam kwenda
mkoani Singida kuhudhuria maadhimisho ya miaka 39 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akataa
sherehe ya kifahari Bungeni.
Rais
alionekana tofauti na viongozi wengine waliomtangulia baada ya kuifanya sherehe
ya kuzindua Bunge kutokuwa ya kifahari na hivyo akaokoa Sh milioni 251, ambazo
aliagiza zikanunue vitanda Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Jumla ya
vitanda 300, magodoro 300, viti maalumu vya wagonjwa 30, vitanda vya kubeba
wagonjwa 30 na mashuka 1,695.
Afuta
gwaride la Uhuru.
Novemba 9,
mwaka jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue, alitangaza kuwa Rais Magufuli
aliamua kufuta shamrashamra za Sikukuu ya Uhuru na kwamba fedha zitakazookolewa
atazipeleka sehemu nyingine.
Fedha Sh
bilioni nne zilizopaswa kutumika kugharimia shamrashamra za Siku ya Uhuru,
ambazo zingefanyika tarehe 9 Desemba 2015, Rais aliamuru zitumike kufanya
upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam yenye urefu wa
kilometa 4.3.
Baraza la
Mawaziri.
Desemba 10,
mwaka jana 2015, Rais Magufuli alitangaza baraza lake la mawaziri ambalo alianza kwa
kuteua mawaziri 19, ingawa wizara ni 18. Mawaziri sita kati ya hao ni wanawake.
Katika
uteuzi wake, aliacha wazi nafasi nne za uwaziri kwa madai alikuwa akitafuta
watu watakaofaa kuteuliwa kuongoza wizara husika.
Wizara
ambazo hakuteua mawaziri katika baraza lake la awali alilolitangaza ni Wizara
ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Desemba 23,
mwaka jana,2015 ikiwa ni siku 13 tangu alipotangaza Baraza la Mawaziri, Rais
Magufuli alikamilisha baraza lake kwa kuwataja mawaziri wanne waliokuwa
wamebakia.
Uteuzi wa
Rais Magufuli umekuwa wa tofauti ambapo viongozi wengi aliowateua kushika
nafasi mbalimbali ni wasomi wa ngazi ya uprofesa na udaktari.
Mabalozi
Wapigishwa Kiapo cha Utii.
Katika
mwendelezo wa kuhakikisha kuwa wale anaowateua wanakubaliana na kasi yake, Rais
Magufuli aliwapa kiapo cha utii makatibu wakuu wa wizara na manaibu wao.
Akiwaapisha
kiapo hicho aliwaeleza wazi kwamba yule atakayeshindwa kufanya kazi ni bora
ajiondoe mwenyewe na kupisha wengine watumikie wananchi.
Majipu
152 Yatumbuliwa.
Ndani ya
siku hizi 100 za uongozi
wa Rais Magufuli, watumishi wa umma 152 wamefukuzwa
kazi kutokana na kasoro
mbalimbali za kiutendaji.
Hao ni
watumishi waliotimuliwa kwa majina au vyeo vyao, lakini ukijumlisha na wengine
waliosimamishwa au kufukuzwa kwa matamko bila kutajwa majina, idadi ni kubwa
zaidi.
Watumishi
hao wamesimamishwa na baadhi wamefukuzwa kazi kutokana na tuhuma mbalimbali za
kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma, Rais kutoridhishwa na utendaji wao, wizi
kwenye taasisi zao, ukwepaji kodi, tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma na
utovu wa nidhamu.
1.Muhimbili.
Hatua za
kusimamisha na kutimua zilianza siku nne tu baada ya Rais kuapishwa, ambapo
Novemba 9, 2015 Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),
Hussein Kidanto, alihamishwa na bodi iliyokuwa na wajumbe 11 ilivunjwa.
2.TRA.
Rais
Magufuli alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Rished
Bade Novemba 27.
3.Bodi ya
TPA.
Desemba 7,
mwaka jana, Magufuli alivunja bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) pamoja
na kutengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka,
Mwenyekiti wa Bodi ya Bandari, Profesa Joseph Msambichaka na Mkurugenzi Mkuu wa
Bandari, Awadh Massawe.
Pia,
aliwasimamisha kazi wasimamizi wanane wa Bandari Kavu (ICD). Jumla ya
waliotimuliwa TPA na TRA ni watu 47.
4.Takukuru.
Akiendelea
na kasi yake, Desemba 16, 2015 Rais alitengua uteuzi wa nafasi nyeti ya
Mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah. Rais alisema alichukua hatua hiyo
baada ya kutoridhishwa na utendaji wa Takukuru chini ya mkurugenzi huyo.
Maofisa
wengine wa taasisi hiyo walisimamishwa kazi kwa kukiuka maagizo yaliyohusu
safari za nje.
Waliosimamishwa
kazi ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas, wakiwa
watumishi waandamizi wa taasisi hiyo.
5.Rahco.
Rais JPM
alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli
Tanzania (Rahco), Benhadard Tito, Desemba 23, 2015 kwa kile kilichoelezwa ni
“ukiukwaji mkubwa wa taratibu za ununuzi” katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya
ujenzi wa reli ya kati.
Pia alivunja
bodi ya Rahco yenye wajumbe wanane na bodi ya TRL yenye wajumbe wanane pia.
6. Katibu
Tawala Mwanza.
Akiendelea
na kasi hiyo, Januari 15, alitengua uteuzi na kumfukuza kazi Katibu Tawala wa
Mkoa wa Mwanza, Faisal Issa kutokana na “utovu mkubwa wa nidhamu” aliounyesha
katika kikao cha cha kamati ya ulinzi kilichofanyika mjini Mwanza.
7.Idara ya
Uhamiaji.
Rais
Magufuli alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile na
Kamishna wa Uhamiaji anayeshughulikia utawala na fedha, Piniel Mgonja Januari
21 ili kupisha uchunguzi baada ya kubaini dosari kadhaa kwenye ofisi hiyo.
8.NIDA.
Januari 25, Dk
Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa (Nida), Dickson Maimu kutokana na matumizi yasiyoridhisha ya Sh179
bilioni.
Wengine
waliosimamishwa Nida ni Joseph Makani ambaye ni mkurugenzi wa Tehama, Rahel
Mapande (ofisa ugavi mkuu), Sabrina Nyoni (mkurugenzi wa sheria) na George
Ntalima, ofisa usafirishaji.
Pia,
aliwarudisha nyumbani mabalozi wawili, Dk Batilda Buriani aliyekuwa Japan, Dk
James Msekela (Roma, Italia). Pia, Peter Kallaghe (Uingereza) na kurejeshwa Wizara
ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano, Kikanda na Kimataifa.
Dunia nzima Yamkubali.
Kutokana na
kasi yake ya mabadiliko ya kweli ya uongozi wake, hasa kudhibiti matumizi na
kuelekeza fedha katika huduma za kijamii, Rais Magufuli amekuwa gumzo kwenye
anga za kimataifa.
Uongozi wake
umeelezwa kuwa wa mfano, kwani miongoni mwa mambo anayoyafanya, yanagusa
ulimwengu na anatekeleza yote bila kufanya safari yoyote ya nje ya nchi kama
wanavyofanya viongozi wengine.
Tangu aingie
madakarani, amedhibiti mabilioni ya fedha na kuzielekeza katika kuboresha
huduma za afya, ikiwamo kuongeza upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya
Ukimwi (ARV’s), ruzuku ya shule na miundombinu ya barabara.
Changamoto: Sakata la
Zanzibar.
Pamoja na
yote, suala la kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar limekuwa likiitesa
Serikali ya Rais Magufuli.
Wakati Chama
Cha Mapinduzi kikitaka uchaguzi huo urudiwe, Chama cha Wananchi (CUF)
kimeendelea kushikilia msimamo wake kuwa hakitakubali marudio ya uchaguzi huo
na hakitashiriki.
CUF
wanaamini Rais Magufuli pekee ndiye anayeweza kumaliza mzozo huo ulioibuka
visiwani humo, lakini kiongozi huyo hajazungumza lolote hadi hivi sasa tangu
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alipotangaza
kufutwa na kurudiwa kwa uchaguzi huo.
Kuendelea
kuwako kwa mgogoro huo, ni wazi kwamba kunaitia doa Serikali ya Dk. Magufuli
nje ya nchi.
Pata Picha, Habari za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa kujiunga na Mimi Hapa...FACEBOOK .. TWITTER .. INSTAGRAM … Pia Usisite kututumia tukio la Picha/Habari kwa WhatsApp +255789925630 Or +255756830214.
|
No comments:
Post a Comment