|
Maazimio Ya
Kamati Kuu Ya ACT-Wazalendo Kufuatia Kikao Chake Kilichofanyika Jumamosi 13
Februari 2016 Katika Hoteli Ya Kagame Jijini Dar Es Salaam.
Kamati Kuu
ya Chama cha Wazalendo (ACT-Wazalendo) ilifanya kikao chake cha kawaida siku ya
Jumamosi tarehe 13 Februari 2016 katika Ukumbi wa Hoteli ya Kagame Jijini Dar
es Salaam.
Pamoja na
mambo mengine, Kamati Kuu ilijadili, kutolea maoni na kuazimia mambo yafuatayo
yanayohusu chama na Taifa kwa ujumla.
1. Kamati
Kuu ilijadili na kuzingatia hali ya kisiasa nchini na kutolea maoni mambo
yafuatayo:-
A. Kamati
Kuu iliwapongeza wananchi na Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC) kwa kufanikisha
uchaguzi mkuu kwa amani kwa upande wa Jamhuri Muungano wa Tanzania. Hata hivyo,
Kamati Kuu inalaani kitendo cha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar za
kuvuruga zoezi la kukamilisha kujumlisha matokeo ya kura zilizopigwa katika
uchaguzi huo.
B. Kamati
Kuu ilipokea na kujadili utendaji wa serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais John Pombe Joseph Magufuli na
kuzingatia yafuatayo:-
i. Kamati
Kuu imetambua jitihada za serikali ya Dk Magufuli katika kupambana na rushwa na
ufisadi nchini kupitia dhana ya kile anachokiita ‘kutumbua majipu’.
Hata hivyo,
Kamati Kuu imezingatia kuwa bado hali ya maisha ya wananchi imeendelea kuwa
ngumu kama inavyothibitishwa na kuendelea kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu kwa
maisha ya binadamu kama vile sukari, mchele, na mafuta ya kula.
Aidha, pamoja
na bei ya mafuta kuendelea kushuka kwa kasi katika soko la mafuta duniani, bei
ya mafuta hapa nchini imeshuka kwa kiwango kidogo kisicholingana na kiwango cha
kushuka katika soko la dunia.
ii. Pamoja
na kwamba chama chetu kinaunga mkono juhudi za kuwachukukia hatua za kinidhamu
watumishi wa umma wenye tuhuma za rushwa na ubadhirifu wa mali za umma,
tunasisitiza kwamba juhudi hizo lazima zifanywe kwa kuzingatia misingi ya
utawala wa sheria, utawala bora na utu.
Aidha,
serikali ya Rais Magufuli haijajikita katika kuleta mabadiliko ya kimfumo,
ikiwemo:- kubadili mikataba ya kinyonyaji ya raslimali kama vile madini na
mafuta; kufuta posho za makalio katika mfumo wa utumishi wa umma ikiwemo Bunge;
kuachana na matumizi ya magari ya anasa (mashangingi); tunaendelea kuagizi
sukari nje; hakuna mpango wa kuifanyia mabadiliko TAKUKURU; na serikali
haielekei kama itashughulikia suala la Katiba Mpya ambayo ndiyo ajenda kubwa
kwa miaka mingi sasa.
2. Kamati
Kuu imepokea na kujadili hali ya kisiasa katika visiwa vya Zanzibar na
kuzingatia na kuazimia yafuatayo:-
A. Kamati
Kuu imeendelea kusisitiza kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Ndugu
Jecha Salumu Jecha, hakuwa na uhalali wa kisiasa, kikatiba na kisheria kufuta
zoezi lililokuwa linaendelea la kuhesabu kura mnamo tarehe 28 Oktoba 2015.
Dalili zote
za kisiasa zinaonyesha kwamba Ndugu Jecha alichukua hatua alizochukua kwa
shinikizo na/au mapenzi ya kisiasa kwa lengo la kuzuia ushindi wa chama
kimojawapo ulioelekea kuwa dhahiri.
Kamati Kuu
imezingatia pia kuwa, mbali na Chama cha Mapinduzi, waangalizi wote wa uchaguzi
wa ndani na nje, pamoja na Jumuiya ya Kimataifa, ikiwemo Jumuiya ya Afrika
Mashariki, wametamka bayana kwamba uchaguzi wa Zanzibar ulifanyika katika
mazingira ya haki, huru na demokrasia na matokeo ya uchaguzi huo yalizingatia
utashi na matakwa ya wapiga kura wa Zanzibar.
Kwa
kuzingatia haya, Kamati Kuu imeazimia yafuatayo:-
i. Kupinga
marudio ya uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi 2016 na kwamba Chama
chetu cha ACT-Wazalendo hakitashiriki katika uchaguzi huo
ii. Kutoa
wito maalumu kwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kuchukua hatua stahiki
kwa mamlaka aliyepewa kikatiba kuhakikisha kwamba Umoja na Amani ya Taifa
inaendelea kuimarika nchini kwa kuzingatia misingi ya demokrasia, utawala wa
sheria na utawala bora.
iii. Kamati
kuu ya ACT-Wazalendo,inataka madiwani na wawakilishi walioshinda na kutangazwa
rasmi na ZEC katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25/2015 watambuliwe na waanze
kuwatumikia wananchi.
Kwa sababu
wawakilishi na madiwani waliotangazwa na ZEC ni halali kwa mujibu wa katiba,
sheria na kanuni za Uchaguzi wa Zanzibar
iv. Kamati
Kuu inaamini kwamba suluhu ya mkwamo wa kisiasa Zanzibar ni kufanya mazungumzo
yatakayojumuisha wadau wote muhimu katika mchakato wa uchaguzi wa Zanzibar.
Hatuamini kwamba mkwamo huu utatuliwa kwa vitisho vya kidola.
3. Kamati
Kuu imepokea, kujadili na kupitisha taarifa ya uchaguzi wa chama na kuzingatia
yafuatayo:-
A. Kamati
Kuu imewapongeza na kuwashukuru wananchi waliojitokeza kupiga kura na kukiunga
mkono chama na hata kufanikiwa kumpata mbunge mmoja, madiwani 41 katika mikoa
mbalimbali, na kuongoza Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji
B. Kamati
Kuu imepitisha taarifa ya mapato na matumizi katika uchaguzi mkuu ambapo chama
kilipokea na kutumia shilingi 656,625,000/=.Taarifa hii inawekwa wazi kwa umma
kama tulivyoahidi kwa kuzingatia tunu yetu ya uwazi
C. Kamati
Kuu imevipongeza vyombo vya habari kwa kazi kubwa waliofanya katika
kuwaelimisha wananchi kuhusu uchaguzi mkuu na kwa kufanya kazi kwa weledi na
bila ubaguzi
4. Kamati
Kuu imejadili na kupitisha Mkakati wa Chama kwa kipindi cha miaka mitano
2016-2020.
Mkakati huu
unalenga kukiimarisha chama katika maeneo matano yafuatayo:-
i)
Kuimarisha safu ya uongozi na watendaji katika ngazi zote
ii)
Kuimarisha mfumo wa mawasiliano ya ndani na kwa umma
iii) Kuibua
na kushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi kwa
kuwashirikishi wananchi
iv)
Kuimarisha mahusiano na vyombo vya habari
v) Kujiandaa
kikamilifu na kimkakati kwa chaguzi za serikali za mitaa wa mwaka 2019 na
uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, na chaguzi ndogo zitakazojitokeza.
5. Ili
kutekeleza kikamilifu Mkakati wa Chama, pamoja na hatua zingine, Kamati Kuu
imeziunda upya Kamati za chama makao makuu kama ifuatavyo:-
i) Kamati ya
Fedha na Miradi ya Kujetegemea
ii) Kamati
ya Utafiti, Sera na Mipango
iii) Kamati
ya Uadilifu, Ulinzi na Usalama wa Chama
iv) Kamati
ya Katiba, Sheria na Mambo ya Nje
v) Kamati ya
Itikadi, Mawasiliano na Uenezi
vi) Kamati
ya Maendeleo ya Jamii
vii) Kamati
ya Mafunzo na Chaguzi
viii) Kamati
ya Wabunge na Uendeshaji wa Serikali za Mitaa
Kamati kuu
imeiagiza sekretariet ya chama kuanza utekelezaji wa mpango mkakati, ili
kukiandaa chama kwa Uchaguzi ujao na uchaguzi mbali mbali
Pia kamati
kuu inawahimiza wanachama waendelee na juhudi za ujenzi wa Chama na kutunza
amani ya nchi.
Zitto Ruyagwa
Kabwe
Kiongozi wa
Chama
14/02/2016.
Pata Picha, Habari za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa kujiunga na Mimi Hapa...FACEBOOK .. TWITTER .. INSTAGRAM … Pia Usisite kututumia tukio la Picha/Habari kwa WhatsApp +255789925630 Or +255756830214.
|
No comments:
Post a Comment