BARAZA la
Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeanza kung’ata kwa
kutumia kanuni ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwa kelele na mitetemo.
Kwa sasa mtu
akitaka kufanya sherehe mtaani, kupiga muziki kwa kelele, kuendesha ngoma za
kukesha za nusu uchi (vigodoro) au ‘bai koko’ au kufanya ibada kwa kelele
mitaani, atapaswa kulipa Sh milioni 10.
Pia, baa na
kumbi za starehe za usiku zitakazopiga kelele, zitapaswa kulipa kiasi hicho.
Aidha, NEMC
imesema pia kuwa wale watakaohusika na kelele za migodini za kutumia baruti,
kupasua miamba zilizo zaidi ya matakwa ya sheria ya mazingira ya kelele na
mitetemo, watapaswa kulipa Sh milioni tano ili kupata kibali.
NEMC imetaka
watu kuheshimu kanuni za viwango vya kelele na mitetemo katika maeneo
mbalimbali nchini. Imeonya kuwa watakaokiuka, hatua kali zitachukuliwa dhidi
yao. Kanuni hizo zimeanza kutumika mwaka jana (2015).
Mkurugenzi
Mtendaji wa NEMC, Bonaventure Baya alisema hayo Dar es Salaam jana.
Alisisitiza
kuwa uchafuzi wa mazingira, unaosababishwa na kelele na mitetemo, umekuwa
ukifanyika bila kujali sheria za nchi na sasa watashughulikia suala hilo
ipasavyo.
Alisema hivi
sasa kanuni za kudhibiti suala hilo, zimekamilika na zimeanza kutumika
kikamilifu. Mtu yeyote atakayekwenda kinyume cha kanuni na sheria, atachukuliwa
hatua kali. Baya alitoa ufafanuzi kuwa yapo maeneo yenye kelele zaidi ya
viwango vinavyoruhusiwa kisheria, ikiwamo maeneo ya migodini.
Alieleza
kwamba kanuni zimeweka vigezo na tozo maalumu la kuanzia Sh milioni tano hadi
Sh milioni 10, kulingana na eneo na aina ya kelele na mtetemo. Alisema mambo
mengine ambayo kanuni zimeweka ni faini kwa kila kanuni itakayovunjwa na
kusisitiza kuwa hatua hizo zitachukuliwa ipasavyo.
Kulingana na
hatua hiyo ya NEMC, sasa mtu mwenye kutaka kufanya sherehe mtaani,
itakayohuisha kelele zitakazosumbua jamii pamoja na majirani zake, ikiwamo
muziki maarufu wa ‘kigodoro’, ibada za makanisani zinazozidi matakwa ya
kisheria ya uanzishwaji wa makanisa hayo katika jamii, atapaswa kulipa Sh
milioni 10 ndipo aruhusiwe kuendelea na shughuli yake.
Kwa mujibu
wa NEMC, ruhusa hiyo inayo lipiwa, pia ina muda na viwango vyake, ambapo kila
muda husika unapoisha, kelele zinapaswa kupunguzwa ama kuzimwa. Hii inahusisha
pia baa na kumbi za starehe za usiku.
Baya
aliitaka jamii kuepuka uchafuzi huo wa mazingira wa kelele na mitetemo, ambao
watu wengi wamekuwa wakidhani si tatizo. Alitaka watu kuheshimu matakwa ya
sheria na kanuni kwa nyakati za mchana na usiku.
“Tumekuwa
tukipokea malalamiko kutoka kwa watu wengi, wakilalamikia usumbufu wa kelele na
mitetemo kutoka kwa watu wanaoendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi na
kijamii katika jamii,” alifafanua Baya.
Alitoa angalizo
kwa wanaotumia vyombo vya muziki na sauti katika maeneo ya makazi, ambavyo
vimeleta madhara kwa afya za watu. Alisema matumizi ya vipaza sauti na vyombo
vya sauti kubwa, wanapaswa kuwa na kibali maalumu.
Alieleza
kuwa kanuni za kelele na mitetemo, zimeweka vigezo na viwango vya sauti kwa
ajili ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya hospitali, makazi,
migodini, kumbi za kijamii, kumbi za usiku za starehe, matangazo, baa na maeneo
mengine.
Baya alisema
baraza limepata changamoto kadhaa, ikiwamo uelewa mdogo wa jamii kuhusu kiwango
cha sauti kinachotakiwa na kisichoruhusiwa na baadhi ya watu kwa makusudi
huvunja sheria.
Kuhusu
faini, alisema sheria ya mazingira imeweka wazi faini kwa wanaokiuka na
kuchafua mazingira kwa kelele na mitetemo. Faini hiyo haiingiliani na tozo la
Sh milioni tano hadi Sh milioni 10 lililoelezwa, ambapo mtu anapaswa kulipa si
chini ya Sh milioni 50 na si zaidi ya Sh milioni 50 ama kifungo jela.
Kaimu
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sheria za Mazingira wa NEMC, Ruth Lugwisha alisema
tatizo la kelele na mitetemo, limekuwapo kwa muda mrefu. Alisema tangu
kupitishwa kwa kanuni, tayari watu kadhaa wamewajibishwa.
Alisema
miongoni mwa waliowajibishwa ni makanisa, kumbi za starehe na baa. Hata hivyo,
hakuwa tayari kuwataja wahusika wala maeneo. Alisema uwajibishwaji huo
ulihusisha faini, kufungiwa na onyo.
Papo kwa Papo >>>> Pata Picha, Habari za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa kujiunga na mimi hapa…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp .
|
No comments:
Post a Comment