Serikali Kagera Kuumaliza Haraka Mgogoro wa Wananchi wa Rutoro na Wawekezaji. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Thursday, September 06, 2018

Serikali Kagera Kuumaliza Haraka Mgogoro wa Wananchi wa Rutoro na Wawekezaji.

Na: Sylvester Raphael.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Marco E. Gaguti amewaahidi Wananchi wa Kijiji cha Rutoro Wilayani Muleba mkoani humo ambao ni Wakulima kushughulikia haraka migogoro ya ardhi kati yao na Wawekezaji wenye Vitalu katika Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Mkoani Kagera ili Wawekezaji waweze kufuga kwa tija na wakulima waendeshe kilimo chao bila kuingiliana na wawekezaji ambao ni wafugaji.

Mkuu wa Mkoa Kagera, Gaguti alitoa ahadi hiyo Septemba 6, 2018 akitembelea vitalu vya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Kikurula Wilayani Karagwe na Kagoma Wilayani Muleba ambapo alikagua uwekezaji wa NARCO eneo la Kikurula na kukutana na Wananchi wa Rutoro ambao wana mgogoro wa muda mrefu na wawekezaji ambao walipewa vitalu na Serikali kuendesha ufugaji wa kisasa na baadhi ya vitalu hivyo kuvamiwa na wananchi hao.

Wananchi wa Rutoro wakitoa malalamiko yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera walidai kuwa wanashindwa kuendeleza maeneo yao ya kilimo kutokana na Serikali kutomaliza mgogogro kati yao na Wawekezaji ambao ni wafugaji na mgogoro huo umedumu kwa takribani miaka kumi na miwili toka mwaka 2006 hadi sasa.

Baada ya kusikiliza malalamiko hayo kutoka kwa Wananchi na kutembelea Vitalu vya Wawekezaji ambao ni Wafugaji, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Marco Gaguti aliwaeleza Wananchi wa Rutoro pamoja na Wawekezaji kuwa alikwenda maeneo hayo kujifunza, kuona na kusikia mwenyewe juu ya mgogoro huo ili autafutie ufumbuzi wa haraka  ili kila upande uendelee na shughuli zake za kulijenga taifa.

Katika hatua nyingine Meneja wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Mkoani Kagera Bw. Mashaka Mlonge alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa NARCO sasa inafanya tathimini upya kuona wawekezaji ambao hawajawekeza na kuviendeleza vitalu vyao kama walivyokubaliana na Serikali ambapo tayari Vitalu vitano kati ya 54 vilivyopo Mkoani Kagera Wawekezaji wake wamepewa “notice” ya kuachia vitalu hivyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad