![]() |
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwansha Mwenge wa Uhuru kuzindua mbio zake kwenye uwanja wa Magogo mjini Geita, Aprili 2, 2018 Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama. |
![]() |
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Kiongozi wa wa Mbio za
Mwenge wa Uhuru, Charles Kabeho wakati alipozindua mbio za Mwenge
wa Uhuru kwenye uwanja wa Magogo mjini Geita Aprili 2, 2018.
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 zinaongozwa na Bw. Charles Kabeho
kutoka mkoa wa Dar es Salaam akishirikiana na Bw. Issa Abasi Mohamed (Kusini
Pemba), Bi. Agusta Safari (Geita), Bw. Ipyana Mlilo (Tanga), Bw. Dominick
Njunwa (Kigoma) na Bi. Riziki Hassan Ali (Kusini Unguja).
|
![]() |
Watoto
wakionyesha halaiki katika sherehe za kuzindua mbio za Mwenge wa Uhuru
zilizoongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye uwanja wa Magogo mjini
Geita, Aprili 2, 2018.
Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu.
Waziri mkuu,
Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa mikoa ya Tabora, Geita, Mtwara na Shinyanga
ambayo inaongoza kwa utoro wa wanafunzi kwa shule za sekondari wahamasishe
umuhimu wa elimu na mahudhurio endelevu shuleni.
“Kwa ujumla utoro wa wanafunzi wa Sekondari
ni mkubwa zaidi kwa mikoa husika kuliko shule za msingi. Nitumie nafasi hii
kuikumbusha mikoa niliyoitaja kuhamasisha wananchi wakiwemo wazazi, walezi na
wanafunzi wenyewe kuhusu umuhimu wa elimu na mahudhurio shuleni.”
Waziri mkuu
ametoa agizo hilo Jana,Jumatatu April 2, 2018, wakati akizindua mbio za Mwenge
wa Uhuru kwa mwaka 2018 katika Uwanja wa Magogo mkoani Geita. Kaulimbiu ya mbio
za mwenge kwa mwaka huu ni ‘Elimu ni
ufunguo wa maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu.’
Waziri mkuu
amesema dhamira ya Serikali kupitia kaulimbiu hiyo ni kuwashirikisha wananchi
na wadau mbalimbali wa maendeleo kuwekeza katika elimu na kuzalisha rasilimali
watu yenye ujuzi na stadi zitakazowezesha kuchochea mapinduzi ya viwanda ili
nchi iwe ya uchumi wa kati ifikapo 2025.
Akizungumzia
kuhusu utoro kwa shule za sekondari nchini, waziri mkuu amesema Mkoa wa Tabora
ndiyo unaoongoza kwa utoro kwa kuwa na silimia 9.7,
Geita
asilimia 8.1, Mtwara asilimia 6.4 na Shinyanga asilimia 6.3.
Kuhusu utoro
wa wanafunzi wa shule za msingi nchini, Waziri Mkuu amesema mkoa unaoongoza ni
wa Rukwa kwa asilimia 3.2, Geita asilimia 3.1, Tabora asilimia 2.9, Simiyu
asilimia 2.0 na Singida asilimia1.9.
Amesema
mikoa yenye kiwango kikubwa cha utoro wa wanafunzi na kuacha shule ihakikishe
mahudhurio yanadhibitiwa shuleni ili wanafunzi wote wanaoandikishwa
wahakikishwe wanahudhuria, wanasoma na kuhitimu.
“Ukitaka kuleta maendeleo ya uchumi
ulio imara, ukitaka kujenga jamii inayo heshimu na kufuata misingi ya
uwajibikaji na ubunifu, ukitaka kujenga Taifa lenye amani na utulivu, lazima
uwekeze zaidi katika elimu”.
Waziri Mkuu
amesema ili kuhakikisha Taifa linafikia viwango bora vya elimu, Serikali
imedhamiria kuboresha elimu katika ngazi zote nchini, kuanzia Elimu ya Awali
hadi Elimu ya Juu.
Awali,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu Bibi Jenista Mhagama alisema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa umbali wa
takribani kilomita 103,440.7 kwa siku 195 katika mikoa yote 31 nchini na
halmashauri za wilaya 195.
|
No comments:
Post a Comment