![]() |
Mwanasheria wa ACACIA, Bi. Diana
Wamuza (wa kwanza kulia) akishughudiana makabidhiano ya nyaraka za kurudishwa
kwa Kiwanja cha ndege cha Kahama uliofanywa jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Meneja wa migodi ya dhahabu ya
Buzwagi na Bulyahulu, Bw. Benedict Busuzu.
|
![]() |
Naibu Waziri
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa
akizungumza mara baada ya makabidhiano ya kurudishwa serikalini Kiwanja cha Ndege
cha Kahama kutoka kwa Kampuni ya Migodi ya ACACIA, uliofanyika jana mkoani
Shinyanga.
Mwenye ushungi ni Mkuu wa
Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack na wa kwanza kulia ni Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela.
|

![]() |
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainabu Telack akihutubia
wananchi waliofika kushughudia makabidhiano ya Kiwanja cha Ndege cha Kahama
yaliyofanyika jana baina ya Kampuni ya Madini ya ACACIA na Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege Tanzania (TAA).
Na Mwandishi Wetu, Kahama.
KAMPUNI ya madini ya ACACIA yenye kumiliki migodi ya dhahabu
ya Buzwagi na Bulyahulu imekirudisha serikalini Kiwanja cha Ndege cha Kahama
kwa ajili ya kuchochea maendeleo kwa ujumla.
Awali mwaka 2005 kiwanja hicho kilikabidhiwa kwa makabidhiano
maalum kati ya serikali na iliyokuwa kampuni ya madini ya Barrick walioomba ili
kurahisisha shughuli zao za migodini ikiwemo ya kutumia ndege kusafirisha
wafanyakazi wao na vifaa.
Katika makabidhiano hayo yaliyofanyika jana mbele ya Mkuu wa
Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela aliiomba
serikali kusaidia kurefusha barabara ya kutua na kuruka kwa ndege kutoka Km.
1.5 hadi kufikia Km 2, ili kufanikisha utuaji wa ndege kubwa ikiwemo ya Shirika
la ndege la Tanzania (ATCL) aina ya Bombardier Q400.
“Tunashukuru wenzetu wa ACACIA kwa kurudisha tena serikalini
kiwanja hiki, lakini bado tunaimani tutaendeleza ushirikiano baina yetu, lakini
ombi langu kwa serikali ni kuongeza urefu wa barabara ya kutua na kuruka kwa
ndege ili ndege kubwa zaidi ziweze kutua ninaimani zitachochea shughuli za
kilimo, biashara na madini na uchumi wananchi utaimarika zaidi,” alisema Bw.
Mayongela.
Pia alisema kutua kwa ndege nyingi kutatoa fursa za ajira kwa
wakazi wa mkoa wa Shinyanga na mikoa jirani, ambapo pia TAA itaweza kusogeza
huduma zaidi ikiwemo ya maduka, hoteli na mafuta ya ndege, ambapo sasa ndege hazitalazimika
tena kujaza mafuta Tabora au Mwanza, kwa safari zake mbalimbali.
Naye Naibu Waziri, Mhe. Kwandikwa alisema serikali
itahakikisha inasaidiana na wadau mbalimbali ili waweze kurefusha barabara ya
kutua na kuruka kwa ndege, ili kufanikisha utuaji wa ndege kubwa za abiria na
mizigo, ambazo zitachochea maendeleo ya Wilaya ya Kahama na Mkoa wa Shinyanga
kwa ujumla.
Hatahivyo, Mhe. Kwandikwa aliwataka ACACIA kuweka katika
mipango yao ya kusaidia ujenzi wa upanuzi na urefushaji wa Kiwanja cha ndege
cha Kahama, ili kiweze kutumika kwa lengo la kutua kwa ndege kubwa, ambapo
itachochea sera ya kukuza viwanda.
“Tunamaeneo mengi sana hapa Shinyanga, tunawaita wawekezaji
waje kuwekeza kwa wingi katika ujenzi wa viwanda, kilimo, madini na biashara
nyingine, sasa usafiri wa uhakika upo ukizingatia tunaviwanja viwili vya ndege
kikiwemo hiki cha Kahama na kile cha Shinyanga, na malighafi, umeme na maji
vipo vya kutosha hivyo waje tu kuwekeza,” alisisitiza Mhe. Kwandikwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa, Bi. Telack alisema sasa mkoa
wake utainuka kwa kuwa umepata fursa ya kuongezewa kiwanja cha pili cha ndege
cha Kahama, ambapo sasa wananchi wataweza kusafirisha mazao ya kilimo na
kufanya biashara na mikoa mingine kutokana na usafiri wa ndege ni wa haraka na
uhakika.
“Ninakuomba Naibu Waziri najua hili lipo kwenye wizara yako,
utusaidie kuharakisha kumalizika kwa kiwanja cha ndege cha Shinyanga, maana
hiki hapa tayari kipo ili na sisi tuweze kupata wawekezaji katika viwanda mfano
Wachina wasiende kuwekeza mkoani Pwani pekee bali waje na huku, tunaimani
tutachochea maendeleo sio ya mkoa wetu tu ila kwa Taifa kwa ujumla,” alisema
Bi. Telack.
Kwa upande wa Meneja wa migodi ya dhahabu ya Buzwagi na
Bulyahulu, Bw. Benedict Busuzu alisema wanajivunia tukio la kurudisha kiwanja
cha ndege cha Kahama kwa serikali, ili sasa kiweze kutumika na Watanzania wote katika
kuchochea ukuaji wa viwanda.
Hata hivyo, Bw. Busuzu ameahidi wataendelea kutoa huduma
mbalimbali kwenye kiwanja hicho kama ilivyokuwa awali, na wataendeleza
ushirikiano mzuri ulipo kati yao na TAA.
|
No comments:
Post a Comment