Waziri Mkuu wa Tanzania, Bw.
Kassim Majaliwa amepiga marufuku tabia ya baadhi ya viongozi katika
maeneo mbalimbali nchini kuwakamata na kuwaweka ndani watumishi wakiwemo
wauguzi bila ya kufuata taratibu.
Pia
amewataka wauguzi nchini kufanya kazi kwa weledi, uaminifu pamoja na kufuata
maadili ya taaluma yao kwa kuwa maisha ya wagonjwa yako chini yao.
Waziri Mkuu
ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Oktoba 04, 2017) wakati akifungua Mkutano Mkuu
wa Mwaka wa 45 wa Chama cha Wauguzi Tanzania, mkoani Lindi.
“Naagiza
viongozi wote kufuata na kuzingatia sheria. Kama kuna makosa ya kitaaluma,
Mabaraza husika yashughulikie jambo hilo na ni marufuku kuwaweka ndani
watumishi kwa tuhuma za kitaaluma.”
Amesema
kwamba katika sekta ya afya bila wauguzi ambao ni kundi kubwa kati ya
Wanataaluma wa Afya, Serikali haitaweza kutekeleza ipasavyo mikakati mbalimbali
iliyopangwa kwa ajili ya kuboresha sekta hiyo.
Katia hatua
nyingine Waziri Mkuu amewaasa wauguzi wote nchini kuhakikisha wanazingatia
kiapo cha maadili ya kazi yao na kwamba Serikali haitamvumilia yeyote atakae
bainika kwenda kinyume.
“Nanyi
Wauguzi mnao wajibu wa kutoa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia kiapo na miiko
ya taaluma yenu. Tunazo taarifa kuhusu baadhi ya Wauguzi kutoa lugha chafu kwa
wagonjwa, kuomba rushwa na wengine kujihusisha na vitendo vya wizi wa dawa.”
Amesema
lengo la Serikali ni kuhakikisha afya za Watanzania wote zinaimarika ili
kuendana na kasi ya utendaji kazi wa Serikali ya kuinua uchumi na kufikia wa
kiwango cha kati, hivyo ni lazima watoe huduma bora kwa wananchi.
Pia
amewaomba waunge mkono kwa nguvu zote jitihada za Serikali katika kuhakikisha
miundombinu na vifaa vyote havihujumiwi na watu wachache ili viwe msaada mkubwa
hususani kwa akina mama wajawazito ili wajifungue salama.
Akizungumzia
kuhusu upungufu wa wauguzi nchini, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea
kuajiri watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo Wauguzi na Wakunga na kuwapanga
katika maeneo yenye upungufu zaidi.
Awali, Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Khamis
Kigwangalla alisema baadhi ya viongozi katika maeneo mbalimbali wamekuwa
wakiwakamata na kuwachukulia hatua watumishi wa Sekta ya Afya bila ya kufuata
taratibu, jambo ambalo si sahihi.
Mkutano huo
umehudhuriwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Dkt. Kigwangalla, Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania Bw. Paul Magesa,
Mbunge wa Lindi Mjini Bw. Hassan Kaunje, Mbunge wa Kuteuliwa Mama Salma
Kikwete(MB) Viti maalum.
Wengine ni
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Gustav Moyo, Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na
Ukunga Tanzania Bw. Stewart Mbelwa.
Wengine ni
Mbunge wa Viti Maalumu, Hamida Abdallah, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya
Uuguzi Bw. Ndementria Vermund, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania Dkt. Obadia
Nyongole na wawakilishi wa wauguzi kutoka mikoa yote nchini.
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
JUMATANO,
OKTOBA 04, 2017.
|
No comments:
Post a Comment