![]() |
|
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia), akijadiliana
jambo na Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Bibi. Siriel Mchembe, kabla ya kuzungumza na
wananchi wa kata ya Leshata, wilayani Gairo, Mkoani Morogoro.
|
![]() |
|
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto), akimsikiliza
Mtendaji mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), Mhandisi Peter Ulanga (kulia)
alipokagua minara ya simu wilayani Gairo, Mkoani Morogoro.
|
![]() |
|
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto), akitoa
maelekezo kwa Wafanyakazi wa Kampuni ya Vodacom Tanzania mara baada ya kufungua
mnara wao katika kijiji cha Chakwale wilayani Gairo, Mkoani Morogoro.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameyataka makampuni ya
simu nchini kuhakikisha mawasiliano ya simu yanapatikana wakati wote katika
ubora unaotakiwa ili kuwawezesha wananchi kupata huduma inayowiana na thamani
ya fedha wanayolipa.
Akikagua na
kuzindua minara ya simu ya kampuni za TTCL, VODACOM, HALOTEL, na TIGO katika Wilaya
ya Gairo mkoani Morogoro, Profesa Mbarawa amesema Serikali itaendelea kushirikiana
na kampuni za simu kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote UCSAF ili katika
kipindi cha miaka mitatu ijayo sehemu zote za Tanzania ziwe zimefikiwa na
huduma ya mawasiliano ya simu ya uhakika.
"Tumieni
mawasiliano ya simu kufanya biashara, kuboresha huduma za jamii kama elimu na
habari ili kukuza ustawi wa maisha yenu", amesema Profesa Mbarawa.
Waziri Prof.
Mbarawa amewaonya wananchi kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ya simu
kwani ipo sheria kali inayodhibiti matumizi mabaya ya simu.
Amezungumzia
umuhimu wa kampuni za simu kujenga minara katika maeneo mapya na kukarabati
minara ya zamani ili kuwezesha mawasiliano kuwa katika ubora maeneo yote ya
nchi.
Amewataka
wakazi wa vijiji vya Letugunya, Leshata na Chakwale kutumia fursa ya
upatikanaji wa mawasiliano kuongeza uzalishaji wa mazao na kuyauza kwa bei
nzuri na hivyo kukuza uchumi wao.
Kwa upande
wake Mtendaji mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote Mhandisi Peter Ulanga
amemhakikishia Waziri Profesa Mbarawa kuwa mfuko huo umejipanga kukamilisha miradi yote
kwa wakati na kufanya uhakiki wa takwimu za mawasiliano nchi nzima ili kubaini
maeneo ambayo yana changamoto kubwa ya mawasiliano na kuyatatua.
Mkuu wa
Wilaya ya Gairo Siriel Mchembe
amemshukuru Waziri Mbarawa kwa kuboresha huduma za mawasiliano katika Wilaya
hiyo na kumhakikishia wananchi watailinda miundombinu hiyo ili idumu kwa muda
mrefu.
IMETOLEWA NA KITENGO
CHA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI,UCHUKUZI NA MAWASILIANO.
|









No comments:
Post a Comment