Picha 8-Barabara aliyopita Rais JPM Kagera, Malori yazidi Kukwama. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Saturday, August 05, 2017

Picha 8-Barabara aliyopita Rais JPM Kagera, Malori yazidi Kukwama.

Eneo la Nyabugombe,wilayani Biharamulo mkoani Kagera Zaidi ya magari 500 yamekwama tangu usiku wa Jana August 4, 2017 katika barabara  kuu ya lami itokayo Nyakanazi –Lusahanga-Rusumo eneo la kijiji cha Nyabugombe kata ya Nyakahura wilayani Biharamulo,mkoani Kagera  kilomita mbili kuingia wilayani Ngara mkoani humo kutokana na barabara hiyo kuharibika tangu ijengwe miaka 32 iliyopita.
Barabara hiyo imeanza kuchimbika na lami kubanduka na kubaki vumbi licha ya kufanyiwa ukarabati wakati wote wa kila mwaka.

Ubovu wake ni kujaa mashimo yanayochangia magari yenye mizigo kushindwa kuendelea na safari, huku mengine yakipinduka baada ya kupanda milima na hata kurudi nyuma.Wakizungumza na Mwandishi wa Mtandao huu  katika eneo hilo, baadhi ya  madereva wamesema eneo hilo ni bovu miaka yote na unapofanyika ukarabati, wakandarasi wanatumia saruji rojorojo bila kuzingatia kuwa magari yanayopita yanakuwa na tani nyingi za mizigo.

Wamesema  magari  hayo yanasafiri kutoka  na kuingia Dar Es Salaam hadi  Rwanda na Burundi na hata Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC,  kwa kuingiza  fedha zinazoweza  kuinua uchumi wa Taifa,  hivyo serikali ya Tanzania  haina budi kujenga upya barabara hiyo, kutoka Nyakanazi wilayani Biharamulo hadi Rusumo   Wilayani ya Ngara mkoani Kagera.


Kukwama kila wakati kwa magari katika eneo hilo la Nyabugombe , safari za magari ya abiria kutoka Ngara kwenda mikoani kupitia eneo la barabara hiyo zimekuwa zikisimama kwa saa kadhaa huku huduma za kijamii kama maji,  mighahawa ya kuuzia chakula , zahanati na mawasiliano ya mitandao ya simu za mkononi vikikosekana na kuleta changamoto kwa wasafiri.

Hata hivyo Mhandisi wa barabara wa mkoa wa Kagera Bw.Chakindo Nasiri, alipotafutwa kwa njia ya simu amesema barabara hiyo inahitaji kujengwa upya, na kinachofanyika hivi sasa ni ukarabati mdogo ili kuwezesha magari kupita kusafirisha bidhaa kuelekea nchi za Rwanda. Burundi na DRC.


Picha Na Shaban Ndyamukama.

Post Bottom Ad