Serikali ya Tanzania yapiga Marufuku Usafirisha Chakula nje ya Nchi. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Tuesday, June 27, 2017

Serikali ya Tanzania yapiga Marufuku Usafirisha Chakula nje ya Nchi.

Waziri Mkuu Bw.Kassim Majaliwa akitoa nasaha kwa waumini (hawapo pichani) waliohudhuria Swala ya Eid el Fitr na Baraza la Eid Kitaifa kwenye msikiti wa Masjid Riadha mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017. 

(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu wa Tanzania,Bw. Kassim Majaliwa amepiga marufuku usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi hiyo.

Bw Majaliwa amesema yeyote atakayekamatwa akijaribu kusafirisha chakula nje ya nchi hiyo, chakula hicho kitataifishwa na kupelekwa ghala la taifa.

Akiongea wakati akitoa nasaha kwenye Baraza la Eid el Fitri lililofanyika kitaifa kwenye msikiti wa Masjid Riadha, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro mara baada ya kuswali sala ya Eid, Waziri Mkuu huyo alisema serikali imechukua hatua hiyo kuzuia Tanzania isikumbwe na baa la njaa.

"Kuanzia leo, ni marufuku kwa mtu yoyote kusafirisha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi bila ya vibali. Serikali inahamasisha uwekezaji kwenye ujenzi wa viwanda nchini. Kama tutatoa vibali, ni lazima mtu alazimike kusaga nafaka ili kutoa ajira nchini," amesema.

Waumini wa dini ya Kiislamu waliohudhuria Swala ya Eid el Fitr na Baraza la Eid Kitaifa kwenye msikiti wa Masjid Riadha mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro wakimsikiliza Waziri Mkuu Bw. Kassim Majaliwa wakati akitoa nasaha za Eid, tarehe 26 Juni, 2017. 

"Mimi nasema kuanzia leo, yeyote atakayekamatwa akitorosha chakula kwenda nje ya nchi, chakula hicho kitataifishwa na kupelekwa ghala la Taifa na gari lake tutalitaifisha na litaishia Jeshi la Polisi. Tunafanya hayo kwa lengo la kuwalinda Watanzania tusikumbwe na baa la njaa."

Bw Majaliwa amesema kumekuwa na wimbi kubwa la usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi bila kibali.

"Hilo ni kosa kubwa kwa sababu litasababisha nchi yetu kupata baa la njaa huko mbele," amesema.

Amesema mipaka ya Tarakea, Holili, Mwanga, Horohoro, Siha, Namanga na Sirari imekuwa inapitisha kiasi kikubwa cha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi jambo ambalo ni hatari sana.

"Hii ni kwa sababu chakula cha ndani hakitoshelezi mahitaji. Kwa sababu nchi zote za jirani hazina chakula cha kutosha. Tusipokuwa makini, tutabaki tunalia njaa."

Kenya ni moja ya nchi ambazo zinakabiliwa na uhaba wa mahindi.

Bw Majaliwa amewataka wafanyabiashara wa ndani, wachukue mahindi kutoka maeneo yenye mavuno mengi na kuyapeleka kwenye sehemu zenye mavuno kidogo.

"Watanzania tushirikiane, kama ni biashara tutoe huku kwenye mavuno mengi na tuyapeleke Shinyanga na Geita ambako wanayahitaji au tukanunue Sumbawanga na kuyapeleka kwenye mikoa mingine yenye upungufu," alisisitiza.

Post Bottom Ad