Katibu Mkuu wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman
Kinana, amesema kwa sasa viongozi madalali
wanaouza viongozi ndani ya chama hicho hawatakiwi, huku akiwataka
watafute kazi nyingine za kufanya.
Kutokana na
hali hiyo amesema sasa wamejipanga kuhakikisha CCM inaendelea kutawala maisha
yote huku akiwataka wenyeviti wa kata, wilaya na mikoa kutokuwa sehemu ya malalamiko na badala yake wawe
sehemu ya kusimamia Serikali kama anavyofanya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais
Dk. John Magufuli.
Kauli hiyo
aliitoa jana mjini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya miaka 40 ya CCM
yaliyofanyika katika ukumbi wa Dodoma Convention Centre, ambao unamilikiwa na
chama hicho, ambapo Kinana awalitaka viongozi wa chama hicho kuacha kuwa
walalamikaji na badala yake wawe sehemu ya kuisimamia Serikali katika kutimiza
wajibu wake.
“Sasa
hatutaki kuwa na viongozi madalali ndani ya chama, kwa hiyo kama wapo
wajitafakari wenyewe. Ndiyo maana hata sisi tumekubaliana maadhimisho sio
sherehe lazima tuachane na tabia za sherehe ukisema sherehe itabidi pia mlipane
na posho jambo ambalo halikubaliki,’’ alisema Kinana.
Akielezea
sababu za kuendelea kushinda kwa chama hicho katika chaguzi mbalimbali, Kinana
alisema wamekuwa wakisimamia na kupigania haki za wananchi huku akidai kwa sasa
kuna viongozi wamekuwa madalali ndani ya chama hicho.
“CCM ni
chama chenye nguvu wana CCM wamekuwa wamoja na hiyo ndiyo imetufanya tumekuwa
tukiendelea kuaminiwa na wananchi na sababu zipo wazi ni kusimamia na kupigania
haki zao hakuna mwenye kauli wana CCM wanamuunganiko.
“Sababu
nyingine ya kuendelea kuaminiwa ni uwepo wa demokrasia pana na yenye kina kwa
kila mwanachama kuwa na uhuru wa mawazo kwa kusema na hata kushauri.
“Wanaoamua
ndani ya chama ni wanachama wakisema ndiyo ni ndiyo na wakisema hapana ni
hapana katika uchaguzi mwanachama ana haki ya kuchagua na ana uhuru wa kuchukua
fomu na kugombea,’’ alisema Kinana.
Alisema kwa
sasa vipo vyama vitatu pekee duniani ambavyo vinaoongoza kwa maandiko mazuri na
yenye tija ambapo alivitaja vyama hivyo
kuwa ni Chama cha Kikomunisti cha China, CCM na ANC cha Afrika Kusini.
Kinana alisema mwaka 2015 chama hicho kilifanya
tathmini kwa miezi 12 kuanzia katika shina mpaka taifa lengo likiwa ni
kupunguza urasimu na umangimeza, ambayo iliwasaidia kujua upungufu na
marekebisho wanayotakiwa kufanywa.
Kuhusu suala
la Serikali kuhamia Dodoma, alisema Serikali inatakiwa iungwe mkono japo
alikiri kwamba mwanzo utakuwa mgumu.
Pia
aliwataka wanachama wa chama hicho kuchagua viongozi wenye kazi zao katika
uchaguzi mbalimbali utakaofanyika.
“Muwachague
viongozi bora waadilifu wenye shughuli zao zisizotokana na CCM awe na shughuli
ya kufanya,’ ’alisema.
Kwa upande
wake Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, alisema CCM kimehusika kwa
asilimia kubwa katika kuleta amani na utulivu nchini huku akiponda vyama
vingine kuhusika na maandamano kila kukicha.
“Hivi
vingine ni vyama vya maandamano tu, amani na utulivu imeletwa na CCM kumbukeni
zamani tulikuwa tunasema chuo kikuu sasa hivi tunasema vyuo vikuu Udom pekee wanamaliza wanafunzi 36,000,’’
alisema Mangula.
Maadhimisho
ya miaka 40 kwa mwaka huu yamekuwa ya aina yake ambapo yamehudhuriwa na wabunge
wote wa chama hicho, wakiwamo mawaziri wakuu wastaafu, John Malecela na Mizengo
Pinda pamoja na Spika wa Bunge, Job Ndugai.
|
No comments:
Post a Comment