Picha Mkuu wa Mkoa wa Kagera azindua Mpango Mkakati wa Kulinda Raslimali za Uvuvi ili kutokomeza uvuvi haramu. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Friday, August 26, 2016

Picha Mkuu wa Mkoa wa Kagera azindua Mpango Mkakati wa Kulinda Raslimali za Uvuvi ili kutokomeza uvuvi haramu.



Bw. Gabriel Mageni Akitoa Taarifa Mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Wananchi Mwaloni Malehe.


Mhe. Kijuu Akianza Kuchoma Nyavu Haramu

Mkuu wa Mkoa Kagera,Mhe. Kijuu Akiongea na Wananchi na Wavuvi wa Mwalo wa Malehe

Mhe. Kijuu Akianza Kuchoma Nyavu Haramu

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Meja Jenerali  Mstaafu Salum M. Kijuu azindua Mpango Mkakati wa Kulinda Raslimali za Uvuvi  Mkoani Kagera ili kuondokana na uvuvi haramu na madhara yake yanayosababisha kupungua kwa samaki katika Ziwa Victoria  na kupelekea kudhoofisha uchumi wa Mkoa na Mwananchi mmoja mmoja wanaojishughulisha na shghuli za uvuvi.

Mpango Mkakati huo umezinduliwa leo Agosti 24, 2016 na Mkuu wa Mkoa katika Mwalo wa Malehe Kituo cha Kanyigo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ambapo aliteketeza nyavu haramu zilizokamatwa katika doria mbalimbali kupitia kituo hicho zenye thamani ya shilingi milioni 205, 510,000/- 

Kabla ya kuzindua  Mpango Mkakati huo Mhe. Kijuu alikitembelea Kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki cha Vicfish ili kujionea uzalishaji wa kiwanda hicho ambapo Meneja wa Kiwanda Bw.Nurdin Salum Juma   alitoa  taarifa kuwa uwezo wa kiwanda hicho ni kuzalisha tani 60 kwa siku lakini kutokana na madhara ya uvuvi haramu kiwanda hicho kinazalisha tani 6 hadi 8 kwa siku sababu ukosefu wa samaki.

Naye Kaimu Afisa Mfawidhi Ofisi ya Usimamizi Raslimali za Uvuvi Mkoa wa Kagera Bw. Gabriel Mageni alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa  kuanzia kipindi cha mwaka 2012 hadi sasa Agosti 2016 ofisi yake imefanikiwa kufanya doria na kukamata zana za uvuvi haramu katika Vituo vya Kanyigo, Bukoba na Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kama ifuatavyo:-

Makokoro ya Sangara 192 yenye thamani ya shilingi milioni 96,000,000/-, 

Timba 3,319 zenye thamani ya shilingi milioni 232, 330,000/-, 

Nyavu za Makila 2,410 zenye thamani ya shilingi milioni  24, 100,000/-, 

Nyavu za dagaa chini ya (milimita 88) 25 zenye thamani yashilingi milioni 17,500,000/- 

na Kokoro ndogo za vyambo 16 zenye thamani ya shilingi milioni 3,200,000/-, Jumla kuu ni shilingi milioni 373,130,000/-.

Aidha, Bw. Mageni alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa changamoto kubwa wanayoipata katika ofisi yake ni kuachiwa suala la uvuvi haramu wao peke yao kama Maafisa Uvuvi badala ya Taasisi zote za Serikali na binafsi  na Wananchi kupambana na uvuvi haramu, Pili ni kutopata ushirikiano kutoka kwa viongozi wa Vitongoji, Vijiji na Kata hasa watendaji na Wenyeviti wanaozunguka katika Ziwa Victoria.

Akiwahutubia wananchi na wavuvi katika Mwalo wa Malehe Mhe. Kijuu aliwaeleza kuwa Mkakati aliouzindua utakuwa shirikishi hasa viongozi na wanachi ili kukomesha uvuvi haramu katika Ziwa Victoria, aidha, alitoa rai kuwa kiongozi au Mtendaji yeyote atakayegundulika kuhusika au kukutotoa ushirikiano katika suala la uvuvi haramu atashghulikiwa ipasavyo kisheria.

Aidha, aliwataka wananchi wote wanaojihusisha na uvuvi haramu kuacha mara moja ili kuruhusu samaki kuzaliana na kuvuliwa kwa utaratibu ulio mzuri. 

Katika hatua nyingine aliwahamasisha wavuvi kujihusisha na miradi ya ufugaji samaki katika mabwawa kuliko kutegemea Ziwa la Victoria peke yake.

Mpango Mkakati wa Kulinda Raslimali za Uvuvi  Mkoani Kagera unalenga kuzuia uvuvi haramu katika Maziwa yanayopatikana katika Mkoa kwa kuendesha doria za mara kwa mara na endelevu, kuhamasisha wavuvi kukopa na kuwekeza katika uvuvi wa kisasa, na kutunza mazingira na mazalia ya samaki ili kuongeza wingi na upatikanaji wa samaki hasa katika Ziwa Victoiria.

Mpango huo utawahusisha wadau mbalimbali vikiwemo vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wananchi, Wavuv,i Wenye Viwanda na Viongozi katika ngazi mbalimbali za Serikali hasa kuanzia katika ngazi ya Kitongoji, Kijiji na Kata ili kuhakikisha uvuvi haramu unakomeshwa mara moja katika Mkoa wa Kagera.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad