Rais John Magufuli
ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Magesa Mulongo kuanzia jana.
Taarifa iliyotolewa na
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa ikimnukuu Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi John Kijazi imesema Rais amemteua Dk Charles Mlingwa ambaye
alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Siha kujaza nafasi hiyo.
Mulongo anakuwa mkuu wa
mkoa wa pili kutimuliwa kazi na Rais Magufuli baada ya Anne Kilango Malecela
aliyekuwa Shinyanga.
Hata hivyo, tofauti na
Kilango ambaye alitimuliwa kutokana na kutoa taarifa potofu kuhusu watumishi
hewa mkoani mwake, Ikulu haikutoa sababu za kutenguliwa kwa uteuzi wa Mulongo.
Mulongo ameondolewa
madarakani miezi sita baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Dk Faisal Issa baada ya kutofautiana na
Mulongo wakati huo akiwa mkuu wa mkoa huo.
Baada ya kumwondoa Dk
Issa na nafasi yake kujazwa na aliyekuwa Kamishna wa Polisi, Fedha na Utawala
(CP) Clodwig Mtweve, miezi miwili baadaye Rais alimbadilisha Mulongo kituo cha
kazi akimhamishia Mara.
Alipoulizwa jana jinsi
alivyoipokea hatua hiyo iliyochukuliwa dhidi yake Mulongo alisema: “Sina
taarifa rasmi.”
Kabla kuhamishiwa Mara akitokea Mwanza, Mulongo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Alishika nafasi hiyo
baada ya kupandishwa cheo akiwa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo.
|
No comments:
Post a Comment