Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji
imetenga jumla ya shilingi milioni 200 katika bajeti ya Mwaka 2016/2017 ili
kupanua mfumo wa maji safi katika Mji wa Kasulu,mkoani Kigoma.
Hayo yamesemwa leo,June 21,2016 Bungeni Mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe alipokuwa
akijibu swali la mbunge wa Kasulu, Mhe. Daniel Nswanzugwako juu ya ukabarati wa
vyanzo vya maji vilivyopo Mjini Kasulu ili maji yafike katika mitaa ya kata za
Mrusi, Mwilavya na Kidyama.
“Serikali inatambua changamoto ya
mtandao wa maji inayoukabili Mji wa Kasulu, katika mwaka wa fedha 2016/17
imetenga Milioni 200 kwa ajili ya kupanua mfumo wa maji safi katika mji huo,”
alisema Mhe. Kamwelwe.
Aidha, Mhe. Kamwelwe aliendelea kwa
kusema kuwa, fedha hizo zitatumika katika kuboresha hali ya huduma ya maji
ikiwemo kuongeza mtandao wa maji Mjini Kasulu ambapo pia kata za Mrusi,
Mwilavya na Kidyama zitapata huduma ya maji safi na salama.
Pia Mhe. Naibu Waziri huyo amesema
kuwa Serikali imekamilisha usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zaburi kwa
ajili ya mradi wa majisafi wa kujenga chujio katika Mji wa Kasulu ili
kuondokana na tatizo la maji kuwa machafu.
Wizara hiyo pia imetenga kiasi cha
shilingi bilioni 1 katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa ajili ya kutekeleza
miradi ya upanuzi wa miundombinu ya usambazaji maji Masasi – Nachingwea kupitia
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Masasi – Nachingwea.
Mradi huo unaohudumia wakazi wapatao
188,250 wa Miji ya Masasi na Nachingwea pamoja na baadhi ya Halmashauri za
Wilaya ya Masasi, Nachingwea na Ruangwa.
Aidha wizara hiyo itaendelea kutenga
fedha zaidi katika bajeti zijazo ili kupanua huduma ya upatikanaji wa maji nchi
nzima.
|
No comments:
Post a Comment