Bunge la Tanzania limepitisha kwa
kauli moja Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 2 ya mwaka 2016
ambayo pamoja na mambo mengine, imeongeza adhabu kwa watu wanaowapa mimba au
kuoa ama kuolewa na mwanafunzi, sasa watafungwa jela miaka 30.
Sheria hiyo ilipitishwa
Jana,June 27,2016 Bungeni mjini Dodoma baada ya Muswada kuwasilishwa Juni 24, mwaka huu,2016 na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambao baadhi ya Wabunge walipata fursa ya
kuuchangia.
Muswada huo ulilenga
kufanya marekebisho katika sheria 21 kwa lengo la kuondoa mapungufu
yaliyobainika wakati wa utekelezaji wa sheria hizo na umepitishwa kuwa sheria.
Sheria zilizopendekezwa
kurekebishwa na sheria hiyo ni pamoja na ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha
Haramu; Kudhibiti Usafirishaji Haramu wa Binadamu; Kanuni za Madai; Usajili wa
Makandarasi; Elimu; Ajira na Mahusiano Kazini na Sheria ya Taasisi za Kazi.
Muswada huo
uliowasilishwa Bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe.George Masaju unatamka
adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela katika marekebisho ya Sheria ya Elimu kwa
watakaompa mimba, kumuoa au kuolewa mwanafunzi.
Awali adhabu
iliyotamkwa katika sheria hiyo ya elimu ni mshitakiwa akibainika kuwa na kosa
kutozwa faini ya Sh 500,000 na iwapo ni kosa la pili anatozwa faini ya Sh
500,000 au kifungo kisichozidi miaka mitatu.
Akiizungumzia sheria
hiyo inayosubiriwa kusainiwa na Rais John Magufuli, Mhe.Masaju alisema inawalinda
watoto wote chini ya miaka 18 walioko na wasio shuleni na kuwa kosa hilo
likifanywa na mtoto atahukumiwa kwa mujibu wa sheria ya mtoto.
Kifungu cha 60 A (i)
kimeeleza kuwa itakuwa kinyume cha sheria katika mazingira yoyote yale kwa mtu yeyote
kumuoa au kuolewa na mwanafunzi wa shule ya sekondari au ya msingi na
atakayekiuka atafungwa jela miaka 30.
Katika Sheria ya
Taasisi za Kazi inataka mwajiri anapokiuka masharti ya sheria ya kazi, ikiwa ni
pamoja na kuchelewesha michango ya waajiriwa, kutoza faini na Ofisa wa Kazi ya
papo kwa hapo isiyopungua Sh 100,000.
Wakichangia muswada
huo, Wabunge wameonesha furaha yao juu ya Sheria ya Elimu inayohusu adhabu ya
miaka 30 jela.
Hata hivyo, pamoja na furaha hiyo, baadhi ya wabunge wametoa
angalizo la kutaka kupimwa kwanza DNA kabla ya kutoa hukumu huku wengine
wakitaka kuwapo kwa nyongeza ya viboko.
Mbunge wa Geita Mjini, Mhe.Constantine Kanyasu (CCM) alipongeza marekebisho hayo na kutaka adhabu ya miaka
30 iongezwe na kuchapwa viboko 12 kila mwezi mpaka aliyehukumiwa anamaliza
kifungo kutokana na wahalifu hao kuwa na mazoea ya kuzoea gereza.
Naye Mbunge wa Viti
Maalumu, Mhe.Subira Mgalu (CCM) alisema pamoja na serikali kuja na marekebisho hayo
pia waangalie namna ya kukabiliana na utoro shuleni ili kuwafanya wanafunzi
kupata elimu.
Kwa upande wake, Mbunge
wa Njombe Kusini, Mhe.Edward Mwalongo (CCM) alitaka sheria imtake anayekutwa na
kosa hilo kuacha fedha za fidia ambazo mama atazitumia wakati mwanaume akiwa
jela.
Akijibu hoja ya
kutumika kwa vipimo vya vinasaba (DNA), Mhe.Masaju alisema kwa sasa utaratibu wa
vipimo hivyo utatumika mahakamani na waendesha mashitaka kuhakikisha hawaachi
shaka kwenye ushahidi kutokana na Tanzania kutokuwa na uwezo wa kumpima DNA
mtoto akiwa tumboni.
Kuhusu Sheria ya
Taasisi za Kazi, Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe.Hawa Chakoma (CCM), alitaka adhabu
hiyo kuongezwa ili sheria kuleta tija na kutaka kazi ya kutoza faini hiyo
isifanywe na Ofisa wa Kazi kama ilivyotamkwa katika sheria badala yake ifanywe
na Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Jamii (SSRA) kutokana na mifumo mizuri ya
ufuatiliaji.
Akijibu hoja hiyo,
Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Mhe.Jenista Mhagama alisema
serikali imekuja na sheria hiyo ili kuwabana waajiri wanaochelewesha michango
ya waajiriwa na kuwa katika kutekeleza sheria waziri ataweka makundi na kuwa
kampuni zenye kipato kikubwa adhabu yao itakuwa kubwa zaidi.
|
No comments:
Post a Comment