BUNGENI DODOMA:-Muswada wa Manunuzi na Changamoto za abunge kwa Waziri wa Fedha. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Friday, June 03, 2016

BUNGENI DODOMA:-Muswada wa Manunuzi na Changamoto za abunge kwa Waziri wa Fedha.

Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania, Dk Philip Mpango ,Jumatano ,June 01,2016, alibanwa bungeni baada ya wabunge kutaka maelezo ya kina ya sababu za Serikali kushindwa kuwasilisha muswada wa kurekebisha Sheria ya Manunuzi ambao unalalamikiwa kuwa unachochea ufisadi.

Sheria hiyo imekuwa ikilalamikiwa na wadau, wakiongozwa na Rais John Magufuli, kuwa inatoa mwanya kwa wazabuni kupandisha bei za bidhaa wanapopewa mikataba ya Serikali kwa kushirikiana na watumishi wa umma.

Rais Magufuli alilalamikia sheria hiyo kwa mara ya kwanza Novemba mwaka jana wakati akizindua Bunge, akisema inaumiza Serikali na hivyo itafanyiwa marekebisho.

Juzi, wabunge wa CCM walisimama kidete wakimtaka waziri huyo kuwa na majibu yanayoridhisha na kueleza kuwa asipofanya hivyo, wangekwamisha bajeti yake, ambayo hata hivyo ilipita.

Akichangia hotuba ya Wizara ya Fedha, Mashimba Ndaki alisema Sheria ya Manunuzi imekuwa ikisababisha kero kubwa kwa wananchi na kuwasababishia usumbufu usiokuwa na maana.

Ndaki alisema sheria hiyo haifai, lakini inashangaza kuona Serikali imekuwa kimya. Janeth Mbene alisema haiwezekani kuendelea kufumbia macho jambo hilo tena.

Mbene alisema pamoja na udhaifu wa sheria hiyo, Serikali inatakiwa kuangalia upya kwa kuwa yako mashirika mengi ambayo ni mzigo hivyo akaomba yaondolewe na kufutwa.

Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje alisema sheria ya manunuzi ni mchwa unaotafuna kila mali za umma, lakini Serikali inaonekana kufumbia macho.

"Mimi nimekuwa mjumbe wa bodi ya mashirika mbalimbali, lakini utakuta vitu vinavyonunuliwa na watu moja kwa moja, bei inakuwa chini lakini kwa kupitia bei ya Sheria ya Manunuzi inauwa mara mbili yake, huu ni wizi, alisema Lubeleje.

Mbunge wa viti maalumu (CCM), Ritha Kabati alisema sheria hiyo imekuwa ikiwanyima nafasi wazalendo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad