OFISI ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, imeingia katika kashfa nzito na
kudaiwa kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.
Hatua hiyo
inakuja wakati Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli
inapambana na kudhibiti matumizi makubwa pamoja na vita dhidi ya ufisadi.
Ofisi hiyo
ambayo inaongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Profesa Juma
Assad, imethibitika kufanya matumizi hayo pamoja na matumizi mabaya ya
madaraka.
Tangu
Profesa Assad alipoteuliwa kushika wadhifa huo Novemba 5, 2014 na kuapishwa Desemba
2 mwaka huo na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ofisi hiyo imebariki mambo kadhaa
kinyume na maadili na majukumu yake.
Ukarabati wa
Nyumba.
Kwa mujibu
wa nyaraka zilizovuja, Aprili mwaka jana Ofisi ya CAG ilianza mchakato wa
kukarabati nyumba ya Serikali Plot namba 973 iliyopo Mikocheni, Dar es Salaam
inayotumiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali.
Kwa mujibu
wa taratibu, nyumba zote za Serikali zipo chini ya Wakala wa Majengo ya
Serikali (TBA) na taratibu zote za ukarabati hufanywa na kusimamiwa na wakala
huyo.
“Lakini hapa
kwetu hali ilikuwa tofauti kabisa, ofisi ya CAG iliamua kufanya yenyewe
ukarabati huku ikijua kabisa inakiuka utaratibu na ikatoa kazi hiyo kwa kampuni
bila hata kutangaza zabuni, hata kampuni husika haikuwa na mkataba wowote na ofisi
ya CAG.
“Cha
kushangaza zaidi kampuni hiyo ya M/SAfriq-Engineering and Construction Co. Ltd
si ya kigeni, ni ya Waswahili wenzetu, lakini ililipwa gharama za kazi kwa dola
za Marekani badala ya shilingi ya Tanzania.
“Na si
kwamba ililipwa kwa awamu kama ilivyo kawaida, bali wao walilipwa jumla ya dola
za Marekani 102,570 kwa mkupuo, tena hata kabla ya kuanza kazi, ambapo pamoja
na gharama zikiwamo kodi za Serikali, jumla ilifika Sh milioni 281.8,” kilisema
chanzo cha habari hii.
Kabla ya
Profesa Assad kuingia katika nyumba hiyo, ilikuwa ikitumiwa na CAG aliyestaafu,
Ludovick Utouh.
Ununuzi wa
Samani za ndani.
Pamoja na
hali hiyo ofisi hiyo ya CAG ilikiuka sheria na taratibu za Serikali kutokana na
kiongozi wa taasisi hiyo ya umma kulipwa posho ya Sh milioni 18 kwa ajili ya
kununua samani za ndani ambazo hubadilishwa kila baada ya miaka mitano.
Katika
kutekeleza stahiki yake hiyo, Profesa Assad alikwenda mwenyewe Umoja wa Falme
za Kiarabu (UAE) kwa kwa ajili ya kununua samani hizo za ndani Desemba 27,
mwaka juzi.
Inadaiwa
katika safari hiyo CAG alikiuka sheria na taratibu za Serikali kwa kutumia
zaidi ya Sh milioni 18, ambazo zinaruhusiwa kwa “KUNDI A” la viongozi kwa
mujibu wa waraka wa Idara Kuu ya Utumishi (Ofisi ya Rais) namba 1 wa mwaka
2014.
Baada ya
kununua samani hizo, ofisi yake ililipa fedha za ziada kiasi cha Sh milioni
saba kwa ajili ya kuzisafirisha, pamoja na dola za Marekani 4,265 (sawa na
shilingi milioni 9) kwa ajili ya kodi, visa na gharama nyingine za usafiri.
Ununuzi wa
Shangingi.
Mei 13, 2015
ofisi hiyo ya CAG ilimwandikia barua Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma ya
Ununuzi Serikalini (GPSA) barua yenye kumbukumbu namba FA.242/305/01 yenye
kichwa cha habari; “UNUNUZI WA GARI MOJA KWA AJILI YA MATUMIZI YA CAG TOYOTA
LAND CRUISER GX-V8 200 HIGH.”
Baada ya
Mtendaji Mkuu wa GPSA, J. Mwambega kupokea barua ya ombi hilo, alimjibu kwa
barua ya Mei 15, mwaka jana, yenye kumbukumbu Na. CAD.124/318/01/64.
Sehemu ya
barua hiyo ambayo nakala ilipelekwa kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha inasomeka;
“Napenda kukujulisha kwamba ombi lako la ununuzi wa dharura halikubaliki kwa
sasa kwa sababu upo utaratibu ulioandaliwa na Serikali kwa ajili ya ununuzi wa
magari ya viongozi.
“Kwa
kuzingatia hilo, nakushauri ulipie gharama za ununuzi wa gari hilo US $
84,480.05 kupitia akaunti ya GPSA – UNUNUZI WA MAGARI KWA PAMOJA yenye Na.
0250095100500 ‘US$ Account’ iliyopo benki ya CRDB Bank (Plc) Tawi la Vijana,
Dar es Salaam.”
Pamoja na
maelekezo hayo, ofisi hiyo ya CAG ilikiuka maelekezo ya Mtendaji Mkuu wa GPSA
na kununua gari hilo kwa dharura, ambapo malipo yalifanyika Mei, 15, 2015.
Safari ya
Seychelles, China.
Septemba 5,
mwaka jana maofisa kadhaa akiwamo Profesa Assad walisafiri kikazi kwenda nchini
Seychelles, ambapo Septemba 11, waliondoka nchini humo na kwenda Dubai,
Septemba 12 waliondoka Dubai kwenda Nanjing (China), Septemba 19, waliondoka
Shanghai kwenda Beijing na Septemba 22, waliondoka Beijing kurejea Dar es Salaam.
Uchunguzi
umebaini kuwa ukiacha safari ya Seychelles ambako kulikuwa na mkutano wa
wakaguzi wa hesabu, safari ya China haikuwa na uhusiano na majukumu ya kiofisi,
ambapo tiketi za ndege ziligharimu Sh milioni 26.4.
Mbali ya
CAG, ofisa mwingine kutoka ofisi yake, Edwin Rweyemamu, naye alisafiri kwa
mzunguko kama huo, ambapo tiketi yake iligharimu Sh mil 21.7.
Ofisa wa
tatu ambaye hakwenda Seychelles, lakini aliambatana na CAG kwingineko ni
Elibariki Lyatuu, ambaye tiketi yake iligharimu Sh milioni 21.4.
Wote
walisafiri kwa kutumia daraja la “Business Class” ambapo jumla ya gharama za
tiketi zote tatu ilikuwa Sh mil 69.6, gharama ambazo zinatajwa kuwa kubwa
kulinganisha na gharama halisi za safari kwenda nchi hizo, gharama ambazo
hubadilika kutegemea na msimu wa safari.
Uchunguzi ulibaini fedha hizo zilikopwa kutoka fungu la
fedha za Umoja wa Mataifa (UN) zinazotumika katika shughuli mbalimbali ya
ukaguzi wa hesabu, ambapo ofisi ya uhasibu ilisema katika dokezo.
Dokezo hilo
linasomeka; “Lipa Sh 69,659,200 kwa ajili ya tiketi za safari ya CAG na ujumbe
wake nchini Seychelles na China. Fedha hii ilipwe toka UN, lakini tukumbuke
kuirudisha mara tutakapopokea mgawo wa fedha ujao.”
Kauli ya CAG.
Apotafutwa
Profesa Assad Alhamisi iliyopita ofisini kwake, alikataa kujadili au kuzitolea
ufafanuzi tuhuma dhidi yake.
“Kwanza
unajua ni makosa kuwa na nyaraka za ofisi ya Serikali, sasa kama ukiandika basi
na sisi tutachukua hatua. Pia hayo yote uliyosema mimi sihusiki, watafute
watendaji wakupe majibu,” alisema Profesa Assad.
Pamoja na
kutoa majibu hayo, alisema atahakikisha anampata mfanyakazi anayetoa siri za
ofisi na kumfukuza kazi mara moja.
Baada ya
mwandishi kuagana na CAG na kuondoka, akiwa nje ya ofisi hizo, ofisa mmoja
ambaye alihudhuria mahojiano hayo, alimwita na kumwomba nakala ya nyaraka
husika, ambapo alipewa, lakini hakuna majibu au maelezo yoyote ambayo yalitoka
baada ya hapo.
No comments:
Post a Comment