![]() |
JUMAPILI ya
Oktoba 25, 2015, Tanzania inafanya Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge pamoja na
kumpata Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uchaguzi ni
nini? Zipo tafsiri mbalimbali lakini mojawapo na iliyo wazi ni kwamba, hii ni
njia ya kidemokrasia inayotumiwa na watu katika kuchagua viongozi wa kuwaongoza
kwa kipindi fulani kwa mujibu wa Katiba au utaratibu waliojiwekea wenyewe.
Huu ni Uchaguzi
Mkuu wa Tano kufanyika tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza tena mwaka 1992,
lakini ni wa 11 tangu Tanganyika na Zanzibar zilipoungana mwaka 1964.
Uchaguzi wa
mwaka huu una umuhimu wa kipekee kwa sababu kadha wa kadha, mojawapo ikiwa umri
wa miaka 23 tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza.
Huu ni umri
mkubwa, na kwa hakika vijana wengi
waliojitokeza kujiandikisha safari hii ni wenye umri wa kati ya miaka
18 - 35, ikimaanisha kwamba wengi wao walizaliwa kuanzia mwaka 1992. Hawa
wanatengeneza asilimia 57 ya wapigakura wote.
Umuhimu
mwingine ni kwamba, kulinganisha na uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka
1995, safari hii demokrasia imekua na kupanuka kiasi cha kushuhudia wapigakura
22.75 milioni, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini tangu tupate
Uhuru.
Kwa upande
mwingine, hamasa imeongezeka, upinzani umeimarika zaidi na uhuru wa habari
umepanuka ukiwamo ukuaji wa sekta ya habari na mawasiliano, hususan mitandao ya
kijamii.
Haya yote
yanatokea kutokana na kuwapo kwa amani na utulivu, sifa ambazo zimeendelea
kuitambulisha vyema Tanzania hata katika jumuiya za kimataifa.
Uchaguzi
Mkuu ni gharama kubwa kifedha, rasilimali watu na muda, na kama mambo
yatakwenda mrama maana yake nchi itakuwa imeingia hasara kwa kupoteza fedha,
lakini pia itaingia kwenye machafuko ambayo yatatowesha amani iliyodumu kwa
miaka mingi.
Madhara ya
machafuko au Vita – kama tulivyoshuhudia kwa majirani zetu Rwanda na Kenya ni
vifo, ulemavu wa kudumu, kutengana na familia, ukimbizi na kuvurugika kwa
uchumi, jamii na siasa kwa ujumla.
Kwa miaka
yote tangu Uhuru, licha ya uchanga na umaskini kama taifa, Watanzania
hatujazoea maisha ya vurugu na machafuko na ndiyo maana tuna wajibu wa
kuhakikisha uchaguzi huu unapita salama.
Wajibu wa
kulinda amani ya nchi yetu ni wa kila Mtanzania bila kujali rangi, dini, kabila
ama nafasi yake katika jamii.
Tunaposema
hivyo tunamaanisha kwamba, vyombo vya dola vinapaswa kutekeleza wajibu wao kwa
mujibu wa sheria na kuhakikisha Watanzania wanapiga kura kwa amani kuchagua
viongozi wao kwa utaratibu waliojiwekea.
Kimsingi,
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndio wasimamizi wa chaguzi zote, hivyo wana
dhamana kubwa kuhakikisha kila aliyejiandikisha na kujitokeza siku hiyo
anatumia haki yake ya kikatiba kupiga kura bila kubughudhiwa.
Ili kuondoa
utata huo, NEC pia inapaswa kuhakikisha kunakuwa na uwazi kuanzia hatua ya
kupiga kura mpaka wakati wa kutangaza matokeo, ambayo pia yanatakiwa kutolewa
kwa wakati ili kuondoa mashaka miongoni mwa wagombea na wananchi kwa ujumla.
Wanasiasa,
hususan wagombea ama wapambe wao, wanapaswa kutoa kauli za kuhamasisha amani na
utulivu kwa siku hizi chache zilizosalia kuelekea uchaguzi mkuu, siku ya
uchaguzi na baada ya kutangazwa kwa matokeo.
Wanasiasa
wanaaminika kwa wananchi, kwa hiyo kauli yoyote watakayoitoa ama inaweza
kujenga au kubomoa amani iliyopo, hivyo kuondoa utulivu na kuisambaratisha
Tanzania ya sasa iliyotukuka ulimwenguni kote kama kisiwa cha amani na utulivu.
Vyombo vya
habari navyo vina wajibu mkubwa zaidi kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa
usalama na amani na hata baada ya matokeo kutangazwa viendelee kudumisha amani
hiyo.
Hilo
litawezekana tu iwapo vyombo vya habari vitaandika au kutangaza habari kwa
kufuata sheria za nchi, miiko na maadili ya taaluma na fani ya uandishi wa
habari ikiwa ni pamoja na kutoegemea upande wowote, kuepuka lugha za uchochezi
na ushabiki wa kisiasa, kabla na wakati wa kutangaza matokeo.
Kutokana na
umuhimu huo, sisi wamiliki wa mitandao ya kijamii nchini Tanzania (Bloggers)
tumejadiliana na kukubaliana kwa pamoja kuhusu hatma na mustakabali wa taifa
letu kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa wakati na baada ya uchaguzi huu
wa kidemokrasia na kwa kauli moja tumetoa msimamo wetu kuhusu amani ya nchi
hii.
Kwa ujumla,
hakuna anayeweza kujisifu kuwa ana uhalali zaidi wa taifa hili kuliko mwingine,
taifa hili ni letu sote, hivyo wajibu wa kulinda na kudumisha amani na usalama
wa nchi ni wa kila mmoja.
Tunaomba
Watanzania wote wenye sifa wajitokeze kupiga kura kwa amani na utulivu,
wasubiri matokeo kwa amani na utulivu, wapokee matokeo kwa amani na utulivu,
maisha yaendelee kwa amani na utulivu, tusonge mbele kwa amani na utulivu huku
tukijua kwamba kuna maisha baada ya uchaguzi, na hilo ndilo muhimu zaidi.
MUNGU
IBARIKI TANZANIA!
Papo kwa Papo >>>> Pata Picha, Habari za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa kujiunga na mimi hapa…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.
|
Saturday, October 24, 2015

Home
HABARI
UCHAGUZI MKUU TANZANIA 2015:-Tupige kura, Tupokee matokeo kwa Aamani na Utulivu, Kuna Maisha baada ya Uchaguzi.
UCHAGUZI MKUU TANZANIA 2015:-Tupige kura, Tupokee matokeo kwa Aamani na Utulivu, Kuna Maisha baada ya Uchaguzi.
Tags
# HABARI
Sambaza Hii
Chief Editor | Mhariri
HABARI
Labels:
HABARI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Kuhusu Mwandishi
Journalist / Chief Editor / Tanzanian Blogger
Simu: 0756830214 / 0620197747 / 0789925630.
No comments:
Post a Comment