Wanahabari
kazini wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu kuanza kutumika rasmi
kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao na ya Miamala ya Kieletroniki za mwaka 2015.
Ndugu Wandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana,
Napenda
nichukue fursa hii kuwashukuru nyote hasa waandishi wa habari kwa kutenga muda
wenu na kujumuika nasi kwa lengo la kutangaza rasmi kuanza kutumika kwa Sheria
ya Makosa ya Mtandao, 2015 ambayo ilitangazwa kwenye gazeti la Serikali la tarehe 14/08/2015 na kupewa Na. 328.
Pia Sheria
ya Miamala ya Kielektroniki, 2015 ambayo
ilitangazwa kwenye Gazeti la Serikali la tarehe hiyo hiyo na kupewa
Na.329.
Ndugu Wananchi,
Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni nyenzo ya kisasa inayotumika kubeba na
kusafirisha ujumbe, taarifa,takwimu, picha na sauti kwa kutumia njia na mifumo
mbalimbali ya mawasiliano iliyopo, kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine
au eneo moja kwenda eneo lingine kwa uharaka, ufasaha, kwa wakati na kwa
kiwango cha ubora ule ule bila kujali umbali na mipaka iliyopo ya kijiografia.
Matumizi ya
TEHAMA yameleta mafanikio katika kuharakisha, kuboresha na kurahisisha utoaji
wa huduma kwa wananchi na kuchangia kukuza uchumi na kuleta maendeleo nchini.
Mathalani, wananchi
walio wengi sasa wanapata huduma mbalimbali za kifedha, kulipia huduma (leseni,
kodi, Ankara), matumizi ya mitandao ya kijamii, barua pepe na huduma mtandao
kama vile Serikali mtandao, afya mtandao, kilimo mtandao, biashara mtandao,
Elimu mtandao, n.k
Ndugu Wananchi,
Hata hivyo,
pamoja na mafanikio hayo kumekuwepo na changamoto mbalimbali kama vile wizi wa
fedha kwa njia ya mtandao, uvujaji wa taarifa, kusambazwa kwa ujumbe wa matusi,
picha chafu,uchochezi, udhalilishaji, vitisho kupitia mitandaoni.
Vile vile
kuna watu wachache ambao wanaharibu miundombinu ya mawasiliano, kwa mfano
wanakata mkongo wa Taifa wa mawasiliano na mikongo mingine ya mawasiliano na
hili lina athari kubwa sana kwa nchi yetu na kwa nchi za jirani ambazo
zimeunganishwa kwenye mkongo wa Taifa wa mawasiliano.
Ndugu Wananchi ,
Mtakumbuka
kuwa, mnamo tarehe 01 Aprili, 2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
lilipitisha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 na Sheria ya Miamala ya
Kielektroniki ya Mwaka 2015.
Pamoja na masuala mengine, sheria hizi
zinabainisha makosa, kutambua ushahidi wa nyaraka za kielektroniki na pia
kuainisha adhabu zinazokwenda pamoja na makosa mbalimbali ya kimtandao.
Sheria
hizi ni muhimu sana na zina manufaa makubwa kwenye jamii yetu haswa katika
nyakati hizi ambapo matukio ya uhalifu wa mtandao yamekuwa yakiongezeka na
kukosekana kwa Sheria hizi kumefanya Wananchi kutokuwa na mahala pa kukimbilia
pale wanapokumbana na uhalifu kupitia mitandaoni.
Aidha,
ninatambua ya kuwa Sheria hizi zimepokelewa kwa hisia tofauti kutokana na
uelewa mdogo kwa wengi wetu kuhusu sheria hizi.
Vilevile ni ukweli usiopingika
kuwa kumekuwa na tafsiri hasi kwa baadhi ya wananchi juu ya maudhui ya sheria
hizi na kuzifanya zitafsiriwe kama kandamizi zaidi kitu ambacho ni tofauti na
dhana na maudhi ya sheria hizi.
Kwa kutambua
hilo, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia mara baada ya kupitishwa kwa
SHERIA hizi ilianza kuwaelimisha wananchi kupitia vyombo
mbalimbali vya habari na kuwa na mikutano na makundi mbalimbali ya watekelezaji
wa Sheria hizi ili kuwajengea uelewa ikiwemo Jeshi la Polisi, Waendesha
Mashtaka, Wachunguzi,Wapelelezi, Mahakimu na Majaji kuhusu Sheria hizi kwa
pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaani Bara na Zanzibar.
Aidha, ili kuhakikisha kuwa usimamizi na utekelezaji wa Sheria hizi unakwenda
vizuri, Wizara itaendelea kuwajengea uelewa Wadau mbalimbali.
Ndugu Wananchi,
Tanzania
siyo nchi ya kwanza kutunga sheria kama hizi. Kuna nchi mbalimbali duniani
ambazo zimetunga sheria kama hizi, kwa mfano nchi ya Uingereza (UK Computer
Misuse Act, 1990), India (IT Act, 2000), Malaysia (Computer Crime Act), Uganda
(Computer Misuse Act, 2010),Korea ya Kusini (Information and Communications
Network Act na Information and Communication Infrastructure Protection Act),
Singapore (The Computer Misuse and Cyber security Act),Mauritius (Computer
Misuse and Cybercrime Act, 2003),Marekani (Computer Fraud and Abuse Act, 1984)
na nyingi nyenginezo.
Ndugu Wananchi,
Serikali
baaada ya kujiridhisha kuwa maandalizi yote muhimu ikiwemo elimu kwa umma na
kujenga uelewa kwa watekeleza wa sheria hizi yamefanyika. Sasa, Sheria hizi
zitaanza kutumika rasmi tarehe 01/09/2015.
Kwa hivyo,
natoa rai na wito kwa wananchi wote kuwa tuzingatie “Matumizi Salama na sahihi
ya Huduma za Mawasiliano na Mtandao kwa manufaa ya kila mmoja
na kwa maendeleo ya Taifa letu. Mitandao ikitumiwa vema ina faida kubwa
sana katika jamii yetu.
AHSANTENI
KWA KUNISIKILIZA.
PAPO KWA PAPO Pata Picha, Habari za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo
na Nyingine kwa kujiunga na mimi hapa…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia
tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.
|
No comments:
Post a Comment